Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Dr. Ally Yusuf Suleiman

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Mgogoni

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. DKT. SULEIMAN A. YUSSUF: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu Subhanah Wataala na kumsalia Mtume wake Muhammad Swallalahu Alayhi Wassalam.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaanza mchango wangu naanza kwa masikitiko makubwa kwamba alipokuja Waziri nilidhani anakuja kutuambia kwamba elimu yetu imekwama na kutufahamisha njia ambazo tutakwamuka, lakini badala yake Waziri amekuja hapa, akaja na majibu ya maswali ya kawaida, ukweli hicho si sahihi. Hata hivyo, kwa upande mwingine namshukuru sana Mwenyekiti wa Kamati, ukweli namfahamisha Waziri kwamba atupe zile karatasi zake achukue ushauri wa Kamati, ni mzuri na utamwelekeza pazuri pia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo, naanza mchango wangu kwa kutoa ushauri, nasema kwamba, elimu hapa kwetu imekwama na nadhani Wizara ya Elimu inajua vizuri sana kwamba elimu kwetu imekwama, lakini hatujui ni namna gani tujikwamue kutoka hapo tulipo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo kubwa tunalolifanya hapa kwetu la kusababisha elimu ikawa duni na haina thamani ni kwambakatika udahili tunachukua wanafunzi ambao wame-fail fani nyingine, wameshindwa, tunawachukua wale ndiyo tunawapeleka kwenye ualimu. Tunapanda mbegu mbovu, tunategemea tupate matunda gani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ili tufanikiwe tuwe na elimu yenye thamani, tuchukue wanafunzi ambao wame-pass vizuri sana kuanzia O-level mpaka kufikia A-level na tuwashawishi namna gani ya kuwashawishi hawa, tunaweza kuwashawishi kwa kuwapa mishahara minono kama mishahara ambayo tunawapa Madaktari na fani nyingine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kukwambia kwamba hakuna mtu ambaye ni muhimu baada ya mzazi kuliko Mwalimu. Ndiyo sababu tunapokuja katika ulinganisho, tunasema nani ambaye ni bora Mwalimu ama mzazi. Husemi Mwalimu au Dokta, husemi mzazi au Daktari, husemi mzazi au Mwanasheria bali ni Mwalimu pamoja na mzazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, fani zote ni muhimu, lakini fani ya ualimu ni muhimu zaidi. Ukitaka kuwa Rais ni lazima uende kwa Mwalimu, ukitaka kuwa Waziri Mkuu ni lazima uende kwa Mwalimu, ukitaka kuwa Spika, ni lazima uende kwa Mwalimu, ukitaka uwe Mwenyekiti wa Bunge, ni lazima uende kwa Mwalimu, ukitana uwe Mbunge ni lazima uende kwa Mwalimu, ukitaka Ukurugenzi, ni lazima uende kwa Mwalimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mwalimu ni mtu muhimu kupita kiasi na ndio sababu mshairi mmoja wa Kiarabu anakwambia kumli lmuallimi wafii ttamijina kaadha lmuallimu an-yakuna rasula, alimta akrama au ajalla mina lladhi yubni, wayunshiu jabni, wayunshiu anfusan waankula. Anakwambia msimamie mwalimu na mtukuze kwa hali yoyote ya utukufu, kwa sababu Mwalimu anakaribia kuwa Mtume. Je, unamjua mkaribu zaidi na mtukufu zaidi kuliko yule ambaye anajenga nafsi za watoto na akili zao, kuna mtukufu kuliko huyo? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo la kwanza hilo kama tunataka tufanikiwe katika elimu tuchukue wanafunzi waliokuwa bora kwa kuwapa mishahara minono Walimu wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili hapo hapo kwa Walimu kila siku tunazungumzia upungufu wa Walimu katika vijiiji, kuna shule zina Walimu wawili, kuna shule zina Walimu watatu, jamani sababu yake mnajua. Sababu yake ni kwamba kule vijijini mazingira ni mabovu, kwa hivyo, Mwalimu anapopelekwa kijijini, huyu ni kama anaadhibiwa. Ili kuwafanya Walimu wakae vijijini, ni muhimu sana hawa tukawazidishia mishahara kwanza, halafu kuna posho ya mazingira magumu, ni lazima tuwape. Mahali hakuna barabara, hakuna umeme, hakuna kilichopo, hata kuja mjini ni matatizo, ni lazima tuwanyanyue, tuwape hadhi nzuri hawa ili waishi maisha yaliyokuwa bora kule shamba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo hapo lakini nataka nisizungumze upungufu wa Walimu vijijini tu, nataka Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa, atueleze ni Walimu wangapi ambao hivi sasa tunao, hitajio letu ni Walimu wangapi kwa jumla na upungufu wa Walimu tulionao. Pia atueleze ni jitihada gani ambazo Wizara inachukua ili kuhakikisha kwamba tunaziba lile gape lililopo, nataka akija hapa atujibu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo naelekea katika masuala ya elimu kwa upande wa Zanzibar. Nataka Mheshimiwa Waziri pia atakapokuja hapa anifahamishe ni nini maana ya elimu ya juu, maana yake nashindwa kuelewa elimu ya juu ni ipi, kwa sababu gani? Kwa sababu leo tunakuta mitihani ya form four, mitihani ya form six, Zanzibar inafanywa mitihani kutoka bara na nijuavyo mimi A-level na O-level sio elimu ya juu, siyo mambo ya Muungano, ni kwa nini vijana wale wanafanya mitihani kutoka hapa, wakati hata mitaala inatungwa hapa na mara nyingine inachelewa kufikishwa kule, kadhalika inaweza ikapita miezi sita kabla ya kupewa elimu ya mitaala ambapo hapa Bara tayari wanakuwa watu wameshapatiwa elimu hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, unategemea wale vijana mitihani waifanye vipi kama ni kusema kwamba, wanataka tuwasaidie, ikiwa wanataka kusaidiwa kule Zanzibar hata mtihani wa form four na form six naiambia Serikali ya Zanzibar haifai ikae chini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu masuala madogo madogo kama hayo ni masuala ya mtu kufanya mwenyewe, kwa hiyo, kama hawayawezi basi wakae pembeni wampe mtu ambaye wanamjua ambaye ni Maalim Seif. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kadhalika nataka kujua haki ya Wazanzibar katika mikopo ya elimu ya juu. Kwa sababu elimu ya juu ni suala la Muungano, lakini mpaka dakika hii Wazanzibar hawajui haki yao ni ipi katika mkopo ule bali wanachotewa kama watu waliokuwa wanafadhiliwa tu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini tunafanyiwa vitendo kama hivyo! Nataka atakapaokuja hilo pia anijibu. Nimetoa baadhi ya ushauri na kwa sababu muda umekwenda sana lakini sidhani kama ushauri huu utafanya kazi na sababu kubwa nahisi kwamba Mheshimiwa Waziri kavishwa koti ambalo limemzidi kimo, koti alilovalishwa ni kubwa sana.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivyo kwa sababu Mheshimiwa Waziri alikuwa Katibu Mtendaji wa NECTA. Lakini akafukuzwa kwa kushindwa kazi leo, ghafla anaibuka eti ni Waziri, ni mkombozi huyo, atatukomboa kitu gani! Wanasema waarabu faqidu shei la yuutwi (aliyekuwa hana hawezi kutoa) na yeye ikiwa kashinda pale padogo hapa pakubwa hapawezi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naam halafu kaja tu anafanya mambo Mheshimiwa Waziri kwa kukurupuka anatusifu...
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Suleiman, umemaliza muda wako.
MHE. DKT. SULEIMAN ALLY YUSSUF: Ahsante Mheshimiwa Mwenyekiti, siungi mkono hoja.