Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

Hon. Desderius John Mipata

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nkasi Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Nampongeza Mheshimiwa Waziri Ummy Mwalimu kwa hotuba nzuri ya Wizara ya Afya. Nampongeza Waziri kwa utendaji mzuri na kuiongoza Wizara vizuri. Nampongeza Naibu Waziri, Mheshimiwa Dkt. Ndugulile kwa uchapakazi wake na watendaji wakuu wa Wizara ya Afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Jimbo la Nkasi Kusini kupatiwa gari la wagonjwa liende Kata ya Kala ambayo iko kilomita 150 kufika Makao Makuu ya Wilaya. Umbali huu umesababisha vifo vingi vya akina mama na watoto hasa wanapopata uzazi pingamizi kwa vile huduma zilizopo Kata ya Kala ni za kiwango cha zahanati ambapo wataalam hawapo lakini pia hakuna gari la wagonjwa ili kunusuru wazazi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi Desderius John Mipata tuko Wilaya moja na Mheshimiwa Keissy ambaye alipewa ambulance mbili. Nina wakati ngumu sana wakati kiuhalisia Jimbo langu kijiografia ni gumu zaidi. Kwa heshima na taadhima namwomba Mheshimiwa Waziri anipe gari moja tu la wagonjwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi la pili, watumishi wa afya Wilayani Nkasi ni wachache sana. Pale Wilayani namuona Dkt. Mwakapimba pekee ndiyo yuko active zaidi na mwenye uwezo mzuri wa kielimu na anafanya kazi sana sana. Yeye ni Medical Officer, wapo AMO’s wengine lakini kiutendaji utagundua kuwa MD’s ni muhimu waongezeke asiwe yeye pekee maana Mkuu wa Idara mara nyingi yuko kwenye mambo ya utawala zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, manesi yaani wauguzi ni wachache sana. Pia clinical officer ni wachache sana, zahanati nyingi zinaendeshwa na manesi na wahudumu. Watumishi wa usingizi ni wachache sana Nkasi au niseme hatuna. Naomba suala hili la kupatiwa watumishi lipewe kipaumbele.

Mheshimiwa Naibu Spika, vitambulisho vya wazee kutibiwa bado Halmashauri hawajatoa kipaumbele licha ya kuagizwa na Madiwani mara kwa mara. Naomba uwaagize na kufuatilia hasa Nkasi District Council.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, nawaombea Waziri, Naibu Waziri na watendaji wote wa Wizara Mungu awajalie afya na nguvu ili muendelee kusaidia Watanzania. Kwa ujumla Watanzania wanaridhishwa na utendaji kazi wa Wizara hasa upatikanaji wa dawa, mmefanya vizuri sana.