Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

Hon. Dr. Faustine Engelbert Ndugulile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigamboni

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya njema na kuniwezesha kuwepo katika Bunge lako Tukufu na kuweza kuchangia hoja iliyowasilishwa hapa Bungeni tarehe 07 Mei.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa njia ya pekee kabisa naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuniamini kutumikia nafasi hii ya Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto. Aidha, napenda kumshukuru sana Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais pamoja na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa kwa maelekezo mbalimbali ambayo ameendelea kutupatia katika utekelezaji wa majukumu yangu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa njia ya kipee kabisa napenda kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mheshimiwa Ummy Mwalimu, mimi namwita Daktari kwa ushirikiano wake wa hali ya juu sana na miongozo mbalimbali ambayo ameendelea kunipatia katika utekelezaji wa majukumu. Amekuwa ni nguzo moja muhimu sana na mafanikio haya tunayapata ni kwa sababu ya uongozi wake mahiri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kwa michango yao, maoni yao na ushauri wao kwa kiasi kikubwa sana wamekuwa ni dira na miongozo wetu na tunaahidi kwamba tutazingatia maoni na ushauri wao katika kutekeleza majukumu yetu ya msingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, niwashukuru timu ya wataalam ambao na sisi tunawaongoza, Makatibu Wakuu wawili, Dkt. Zainabu Chaula, Katibu Mkuu wa Fungu 52 na Dkt. John Jingu wa Fungu 53 kwa kazi kubwa na nzuri ambayo wameendelea kuifanya. Kazi nzuri inaonekana kwa sababu na kazi nzuri ambayo wao kama Makatibu Wakuu na Watendaji wote wameendelea kuifanya pamoja na Wakuu wa Taasisi, vyuo vya mafunzo na hospitali zetu zote ambazo na sisi kama Wizara tunazisimamia.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini haya yote yasingeweza kwenda vizuri kama nisingepata support ya wale wananchi ambao wamenileta hapa, wananchi wa Kigamboni na naomba nitambulishe pale juu gallery leo nina viongozi wa Chama cha Mapinduzi natumaini utapata fursa ya kuwatambua kutoka Wilaya ya Kigamboni na Waheshimiwa Madiwani wote kutoka Wilaya ya Kigamboni nao wapo hapa kuja kushuhudia wasilisho la hotuba hii. Niendelee kusema kwamba Kigamboni tunawakilisha vizuri ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo machache sasa naomba nijielekeze katika baadhi ya hoja za msingi ambazo ziliweza kutolewa na Waheshimiwa Wabugne na nianze na hoja za Fungu 53, Fungu la Maendeleo ya Jamii. Niseme tu kwamba moja ya hoja ya msingi ambayo ilijadiliwa sana na Wabunge wengi ni suala la wazee, na suala la wazee sisi kama Serikali tunapaswa tujivunie sana. Katika moja ya mafanikio ambayo Serikali hii imeweza kufanya ni kuhakikisha kwamba umri wa Mtanzania kuishi umezidi kuongezeka, hivi tunavyoongea wastani wa Mtanzania kuishi ni miaka 64.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, maana yake ni nini, ni kwamba ni mafanikio ya mikakati yetu ya lishe lakini mafanikio ya vilevile ya mkakati yetu ya kuhakikisha kwamba Watanzania hawa tunapata huduma nzuri za afya, na ndiyo maana tuna kundi kubwa la wazee ambalo lipo na tunatarajia kwamba kwa hali tuliyokuwa nayo watu wengi watafika zaidi ya miaka 60 ya umri wakiwa na afya njema na kuweza bado wakiwa na nguvu ya kuendelea kutumikia nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna Sera ya Wazee ya Mwaka 2003, tunayo na tunaamini baada na sisi kuingalia tumeiona kwamba tunahitaji tuifanyie maboresho na kuja mkakati sasa ambao utakwenda kutibu baadhi ya changamoto hizi za wazee. Lakini naomba niseme kitu kimoja, Serikali inatambua na kuthamini mchango wa wazee ndani ya Taifa letu, na ndiyo maana sisi kama Serikali tuna makazi 17 ya wazee ndani ya nchi lakini tunawahudumia takribani wazee 510 ndani ya makazi haya 17. Utaratibu uliokuwepo ni mmoja; sisi kama Serikali tunawachukua wale wazee ambao kwanza hawana watoto wa kuweza kuwahudumia, na kama wale wazee hawana watoto basi tunajaribu kuangalia, je, wazee hawa hawana ndugu wa kuwahudumia, na je, kama hawa wazee hawana ndugu wa kuhudumia, je, jamii haiwezi ikabeba jukumu hilo. Kama katika vigezo vyote hivi vitatu havipo basi sisi Serikali tunawachukua wale wazee na tunawagharamia kwa vitu vyote, malazi, makazi na mavazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema idadi ambayo ya wazee ambayo tunayo ni takribani 510 na wazee hawa tunawapa huduma hizo zote za msingi na katika jambo ambalo tunalihakikisha Wizara ni kuhakikisha kwamba, hawa wazee wanapata chakula, malazi na mavazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sambamba na hilo tumeendelea kuhamasisha halmashauri kuzingatia agizo la Serikali la kuwapatia wazee vitambulisho kwa ajili ya matibabu ili wazee wapate matibabu kwa mujibu wa Sera ya Afya ya mwaka 2017 ambayo inasema wazee watapata matibabu bure. Lakini tulienda mbali zaidi na kuhakikisha kwamba hospitali zetu zote zinakuwa na dirisha la wazee, ili wazee wakifika pale waweze kupata matibabu bure.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Sera mpya ya afya ambayo tunayo sasa hivi, tunataka sasa tuende mbali kuona kwamba kuna suala zima la matibabu ya magonjwa ya wazee, kwa sababu wazee hawa kadri kundi linavyozidi kubwa wanakuwa na magonjwa yao ambayo ni mahsusi, geriatric Medicine kwa lugha ya kitaalam nayo tumeshaliona tunaliwekea mkakati ili kuhakikisha kwamba hawa wazee nao tunaweza kuwahudumia vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, moja katika jambo ambalo Mheshimiwa Waziri aliliongea katika hotuba yake, ni pamoja na haya magonjwa sugu ya non communicable disease ambayo tumeona kweli changamoto na mara nyingi wakienda katika hospitali, dawa nyingi wanazokosa ni zile dawa za pressure, za kisukari na nini, hilo tumeliona na ndiyo maana tumeazimia kama tulivyokuwa tuna mapambano na magonjwa mengine kama kifua kikuu, TB na malaria, tunataka tuanzishe Mpango wa Taifa wa Magonjwa Yasiyoambukiza na ambayo sasa yatakwenda kushuka mpaka katika ngazi ya chini ili huduma hizi za msingi za huduma za matibabu utambuzi, matibabu na tiba ya magonjwa yasiyoambukiza iweze kupatikana.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala jingine ambalo nilikuwa nataka kuligusia ni suala la NGO’S, asas zisizokuwa za Kiserikali. Hivi karibuni tulibadilisha Kanuni, mara nyingi tunatambua mchango mkubwa sana wa Mashirika yasiyo ya kiraia katika kuleta maendeleo na kutusimamia kama sisi Serikali, na tunathamini, tunatambua mchango wao. lakini hivyo hivyo kama walivyotaka kutusimamia sisi na kutaka kupata uwazi na uwajibikaji na sisi tunataka tupate uwazi na uwajibikaji katika taasisi zisizo za kiserikali. Ndiyo maana tumebadilisha Kanuni ili sasa kuwepo na uwazi katika fedha ambazo wanazozipata, lakini uwazi katika uwajibikaji katika yale maeneo ambayo walisema wanaenda kuyafanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumekuwa na changamoto kuna baadhi ya NGO’s zimepata fedha nyingi sana, lakini haziendi katika malengo yale ambayo yalikuwa yanakusudiwa. Na baadhi ya NGO’s zimetoka katika malengo na makusudio ambayo yalikuwa yanayafanya, wameenda kujiingiza katika mambo mengine. Wengine wanapata dola milioni 100 lakini zinazofika kwa walengwa ni chini ya dola milioni moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tumeweka utaratibu kwamba fedha zote zinazoingia lazima tuzijue, zinaenda kufanya kazi wapi, lakini tunataka tulete uwiano kwamba kuna baadhi ya maeneo ndani ya nchi yetu huku, zimekuwa na NGO’s nyingi sana lakini kuna maeneo ndani ya nchi yetu hazina NGO’s hata moja na kote huko kuna Watanzania. Sasa tunataka tuweke utaratibu mzuri, tumeanzisha Kanzi data, tuna NGO’s karibuni 9,000 ndani ya nchi yetu, mpaka sasa hivi tumeshaziingiza kwenye Database NGO’s takribani 6,000, tunaendelea na usajili na lengo ni kusudio ni kwamba kila mmoja kule kule alipo hahitaji kuja Dodoma. Tunaweza tukapata taarifa zake tukajua yuko wapi, anafanya nini na fedha alizokuwa nazo kiasi gani, anawajibika kwa utaratibu gani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niendelee kuwatoa shaka ndugu zangu lengo siyo baya, lengo ni kuweka uwajibikaji na uwazi ili kabisa kuhakikisha kwamba hizi NGO’s ambazo na sisi kama Serikali tunatambua mchango wao ili waweze kufanya kazi zao vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo liligusiwa na Waheshimiwa Wabunge ni masuala ya Mitaala ya Vyuo vyetu vya Maendeleo ya Jamii na Vyuo vya Ustawi wa Jamii, haya Waheshimiwa Wabunge tumeyapokea, tutaenda fanyia kazi ili sasa Mitaala hii iendane na mazingira ya sasa na uhitaji wa sasa wa Tanzania ambayo tunaelekea katika Tanzania ya viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa nijielekeze katika maeneo mengine ya Sekta ya Afya hususan Vote 52. Namshukuru sana Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, TAMISEMI amegusia suala la watumishi, rasilimali watu. Na mimi niendelee kuongezea kidogo tu katika hili, pamoja na changamoto hii tuliyokuwanayo ya rasilimali watu, sisi kama Wizara ya Afya hatujakaa tukalala. Tumeangalia ubunifu ambao tunaweza tukatumia kuangalia jinsi gani tunaweza kutumia rasilimali chache, watu hawa tuliokuwa nao ili kuweza kuleta tija katika utoaji huduma za afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, moja ya jukumu ambayo tumeweza kulifanya katika lugha ya kitaalam wanaita task shifting, kwa sababu unaweza ukaenda katika kituo cha afya, daktari yule, kwa mafunzo ambayo tunayo, mimi ninaweza nikachoma sindano, nikafunga kidonda na ninaweza nikatoa dawa. Sasa inawezekana mtu akawa pale amemaliza majukumu yake, anaweza akaenda akafanya jukumu lingine ambapo ndani ya kituo. Tumeona tuweze ku- reorient haya majukumu ili basi huduma kwa mwananchi iweze kutolewa, kwa sababu wataalam wengi wa afya tumeweza kupata mafunzo katika nyanja mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile tumeanza kutumia wataalam wengine ambao sio wataalam wa afya, wamepata orientation, kwa mfano kwa masuala ya upimaji na uchukuaji wa vipimo. Wameweza kupata orientation na wanaweza wakafanya hayo majukumu. Tunataka tufanye orientation ya Maafisa Maendeleo ya Jamii, Maafisa Ustawi wa Jamii, basi nao waweze kutusaidia kutoa huduma katika baadhi ya maeneo ambayo tunaona yana tija. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tumeanza kutumia elimu mtandano (telemedicine). Kwa sasa hivi tunafunga mashine za digitali, dunia nzima ilishatoka huko. Sasa hivi Marekani X- Ray zinasomwa Australia ama inasomwa India. Nasi kwa nini wataalam wetu hawa wachache; na tumeshaanza, pale MOI na Muhimbili tunafunga mashine za kisasa, kutakuwa na screen ziko pale. Mashine zote hizi za X-Ray ambazo tunazifunga Tanzania nzima, itakuwa picha zake zote zinapelekwa Muhimbili na MOI zinasomwa na ndani ya dakika 15 au 20, mtu wa Tunduma, Ruvuma, Mbinga anaweza akapata majibu yake yamesomwa na wataalam. Hizi ni baadhi ya innovation ambazo tunaendelea kuzitumia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa Madaktari wetu Bingwa hawa wachache tuliokuwa nao, tumesema pamoja na kwamba wako katika maeneo ya mjini na katika hospitali zetu kubwa, nami nashukuru sana Hospitali zetu za JKCI, Bugando, MOI, Mloganzila na KCMC wamekuwa wanatoa wataalam wao, wamekuwa wanaenda katika kambi mbalimbali mikoani, wanaendesha kambi za muda mrefu ili wale wananchi wa kule nao waweze kupata huduma hizi za kibingwa na zimekuwa na mchango mkubwa sana na tutaendelea na utaratibu huu kuhakikisha kwamba huduma za kibingwa nazo zinapatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, innovation tunazo nyingi na ndiyo maana unaona kwamba pamoja na changamoto tulizokuwanazo, hali ya utoaji huduma za afya bado zinaendelea kwa ubora ule ule ambao upo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ilitukabidhi Hospitali za Rufaa za Mikoa, nasi tunaendelea kuzipanga. Mkakati wetu wa kwanza ni kuhakikisha kwamba hizi Hospitali za Rufaa katika mikoa ambayo hatuna, ni Hospitali za Rufaa za Mikoa ndiyo tunataka kuanza nazo; Mkoa wa Songwe, Njombe, Geita, Katavi na Simiyu. Ndiyo maana tumeweka nguvu kubwa sana katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, hatua ya pili tunataka sasa katika maeneo ambayo tayari kulikuwa kuna majengo kwa maana ya Mikoa ya Singida, Tanga kule na Shinyanga, tunawekeza nguvu yale majengo yaanze kupata matumizi lakini awamu ya tatu sasa tutajielekeza katika hizi RRH nyingine kuhakikisha kwamba zile huduma za msingi nazo zinaweza kupatikana ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa vifaa na rasilimali watu. Tumewekeza sana sasa hivi katika mafunzo ya wataalam wa afya ili kuhakikisha sasa zile huduma za kibingwa na Madaktari Bingwa wanaweza kupatikana katika maeneo haya.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naamini katika mwaka wa fedha peke yake tumepata kama shilingi bilioni
1.5 kufundisha wataalam zaidi ya 300 na tunataka kwenda mbali. Katika moja ya jambo ambalo tunalitafakari sasa hivi ni kubadilisha mfumo wetu wa mafunzo kwenda kwa utaratibu wa fellowship. Badala ya watu kukaa darasani, watu wanaweza wakaendelea kutoa huduma kule kule tukawapima zile competence zao ambazo tunazitaka na kuwatambua kwamba hawa ni Madaktari Bingwa. Wenzetu wameshapiga hatua kubwa sana katika utaratibu huu, nasi tunaamini ndani ya muda mfupi sisi kama Wizara tutakuwa tumepiga hatua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie na mambo makubwa mawili au matatu kabla sijarudishia Wizara hii, kuna hoja ilikuja hapa kuhusiana na chanjo ya Malaria. Kwa nini wenzetu wa Malawi wamekuwa na chanjo ya Malaria na kwa nini sisi Tanzania tusianzishe chanjo ya Malaria?

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitoe maelezo ya kitaalam kidogo kwamba mpaka sasa hivi hakuna chanjo ya Malaria ambayo imethibitika asilimia 100 kutoa kinga dhidi ya Malaria. Chanjo nyingi tulizokuwa nazo hapa zinacheza kati ya asilimia 20 mpaka 40. Hamna chanjo ambayo imezidi zaidi ya hapo. Kwa hiyo, chanjo nyingi bado zipo katika ngazi ya hatua ya utafiti na naomba niseme kwamba Tanzania tuko vizuri sana katika masuala ya utafiti wa Malaria. Taasisi yetu ya NIMR inafanya kazi nzuri sana ya utafiti na Taasisi zetu za Ifakara Institute nayo inafanya kazi nzuri sana. Pale tutakapobaini kwamba kuna chanjo ambayo inaweza ikawa ina tija, basi na sisi kama Tanzania tutakuwa ni wa kwanza ku-adopt hizo chanjo kwa ajili ya kuwakinga wananchi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie fursa hii kusema kwamba uwepo wa chanjo hauondi dhana ya sisi kuendelea na mikakati mingine yoyote ya kujikinga dhidi ya ugonjwa wa Malaria. Kwa hiyo, tuendelee kwa sababu mazalia haya haya ya mbu ndiyo hayo hayo mazalia ya ugonjwa wa Dengue, Zika, Kichungunya na magonjwa mengi sana ambayo yapo. Kwa hiyo, nami nataka niwaombe Watanzania tuendelee na mikakati yetu mingine, tunapiga hatua katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Malaria lakini tunahitaji tuongeze kasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, chanjo ya gonjwa la ini, tuna tatizo la ugonjwa wa ini ndani ya nchi. Chanjo ya ugonjwa wa ini tunatoa kwa watoto wote chini ya miaka mitano, ni sehemu ya chanjo ambayo tunaitoa na kwa watu wazima tumekuwa tunatoa kwa wale ambao wako kwenye risk zaidi ikiwa ni pamoja na wataalam wa afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, utaratibu ambao tutakwenda nao na tulishakubaliana na Mheshimiwa Waziri ni kwamba kwa yule atakayekuwa anahitaji, tutaweka utaratibu wa chanjo hizi kupatikana kwa gharama nafuu ili mtu mwingine atakayekuwa anajisikia, basi aweze kuchanja kama nasi Waheshimiwa Wabunge tulipata fursa ya kuweza kuchanjwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho kabisa naomba niongelee suala la upimaji. Ni kweli tumekuwa na changamoto kubwa sana ya watu kubainishwa na ugonjwa wa Typhoid na UTI. Nimesema sana na ninaomba nitumie fursa hii kuongea na Bunge lako. Ukienda hospitali na ndani ya dakika tano Daktari akwambia UTI ama una Typhoid, naomba umwulize maswali ya msingi sana huyo daktari. Amejuaje?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa utaalam wetu sisi madaktari inahitaji kati ya masaa 48 mpaka 72 na achukue kipimo cha mkojo na achukue na kipimo cha damu kuja kukwambia wewe una ugonjwa wa Typhoid au una UTI.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nawaomba sana na Waheshimiwa Wabunge mtusaidie kutoa elimu kwa jamii kuwahoji wataalam wetu wa afya kwa sababu wengi sasa wameamua kwa kutumia homa ya UTI na Typhoid kama chanzo cha kupata fedha, lakini kimsingi hatuna tatizo kubwa sana la UTI na Malaria kama inavyosemwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba kumaliza hizi hoja kama nyingi zilivyokuwa zimejitokea na nitoe fursa sasa kwa Mheshimiwa Waziri aweze kuendelea na hoja nyingine. (Makofi)