Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Halima Abdallah Bulembo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. HALIMA A. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa fursa hii ili na mimi niweze kuchangia na ninaomba nijielekeze moja kwa moja katika mchango wangu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunajadili bajeti muhimu kuliko bajeti yoyote nchini. Leo tunajadili bajeti inayohudumia Watanzania wengi kuliko bajeti yoyote nchini na leo tunajadili Bajeti ya Taifa la sasa na hasa hasa Taifa la baadaye. Nitawaonyesha takwimu kuthibitisha maelezo yangu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa Watanzania tunakadiriwa kuwa takribani milioni 50, nusu ya Watanzania wana umri wa miaka 17 kwa maana nyingine nusu ya Watanzania ni watoto. Kwa mujibu wa takwimu ya Taifa ndiyo inasema hivyo, kati ya watoto takribani milioni 25, watoto wetu milioni 12 wako katika shule zetu za awali, shule za msingi na shule za sekondari. Nizungumzie shule za awali. Kwa utafiti wa hali ya uchumi mwaka 2014, inaoneshsa idadi ya wanafunzi wa awali iliongezeka kwa asilimia 1.9 kutoka wanafunzi 1,026,466 mwaka 2013 hadi kufikia wanafunzi 1,046,369. Utafiti huo huo unaendelea kuonyesha idadi ya wanafunzi wanaojiunga na elimu ya msingi inazidi kupungua kutoka wanafunzi 8,202,892 mpaka wanafunzi 8,231,913 sawa na upungufu wa asilimia 0.4.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utafiti huo huo unaendelea kuonesha wanafunzi wa kidato cha kwanza mpaka cha sita, idadi yao imeendelea kupungua kutoka wanafunzi 1,800,056 mpaka wanafunzi 1,704,130 sawa sawa na upungufu wa asilimia 5.5.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Basic Education Statistics yaani BEST, watoto wa Kitanzania milioni nne wako katika elimu ya msingi na watoto wa Kitanzania milioni nne wako katika elimu za sekondari. Kwa maana hiyo hapa tunazungumzia robo ya Watanzania wako mashuleni, robo ya Watanzania wako madarasani na wengine wamekaa chini kwa kukosa madawati, na wengine matumbo yao hayana kitu kwa kutoka familia fukara na shule hazina chakula na wengine wanagombea kitabu kimoja kwa kuwa hatuna vitabu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni dhahiri robo ya Watanzania inafundishwa na walimu wasiokuwa na hamasa na hamasa hii inakosekana kutokana na walimu kutokuwa na mishahara mizuri, kutokupandishwa madaraja katika kazi zao, kutokuwa na makazi yanayoeleweka na wengine kuwa walevi wa kutupa kutokana na stress za maisha. Tunajua kila mtu akiwa na stress zake anaamua pa kwenda wapi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kunauwezekano mamilioni ya watoto wetu wanafundishwa na walimu walevi, lakini leo hii nani ana mamlaka ya kuwawajibisha hawa walimu walevi ilihali elimu haina ukaguzi mzuri, nani ana mamlaka ya kuwaadhibisha walimu hawa kwakuwa hatuwezi kutatua kero zao, nani ana mamlaka? Hakuna. Robo ya Taifa tunaiweka mashakani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, robo ya wananchi wanapata robo ya bajeti. Bajeti ya Wizara ya Elimu ni shilingi trilioni 1.3 kwa pesa za Kitanzania. Tunaambiwa bajeti nyingine ipo TAMISEMI.
Mimi ningeshauri au ningeomba Wizara na Serikali yangu ingeipa bajeti ya Wizara ya Elimu peke yake na bajeti hii ingewekwa kwa uwazi ili tuweze kukokotoa, tujue asilimia 25 ya wananchi wanapata asilimia 25 kweli ya bajeti yao? Tukijumlisha na bajeti inayopelekwa TAMISEMI ambayo tunaambiwa iko TAMISEMI bado bajeti ya Wizara ya Elimu iko chini ya asilimia 10. Tunawakosesha watoto wetu haki ya kuwa na elimu bora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka miwili ya chekechea na miaka mitatu ya elimu ya msingi ni muhimu sana na wote tunajua kwamba elimu ya awali ni muhimu kwa vijana wetu. Lakini vile vile kama Watanzania tunajua Watoto wetu hawa wana matatizo, hawana msaada wa Kiserikali, hawana msaada wa kisera na wala hawana msaada wa kisheria kutoka hizi elimu za mwanzoni. Hali hii inabidi ibadilike kama tunataka kweli kujenga Taifa lililoelimika kwa mujibu wa Dira ya Taifa 2025.
Mheshimiwa Mwenyekiti, matokeo au takwimu za utafiti ya UWEZO inaonesha katika wanafunzi 10 wa darasa la tatu, ni wanafunzi watatu pekee wanaoweza kusoma sentensi ya darasa la kwanza na ni wanafunzi watatu wanaoweza kukokotoa hesabu za darasa la kwanza. Hii inaonesha kwamba Watoto wetu hawapati fursa nzuri ya kusoma huku tangu awali kwenye hizi elimu zao za mwanzoni. Tukitaka kubadili hali hii inabidi tuwekeze. Tuwekeze katika kupata kizazi cha wanafunzi wanaopenda kujisomea, wanafunzi ambao watakuwa na uwezo mkubwa wa elimu, wadadisi na hata wabunifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, asilimia 50 ya vijana wanaomaliza elimu ya msingi hawaendi shule za sekondari na asilimia 75 ya wanafunzi wanaomaliza kidato cha nne hawaendi kidato cha tano na cha sita. Na sera yetu ya elimu sasa hivi inaunganisha elimu ya msingi ya sasa na elimu ya sekondari ya sasa kuwa elimu ya msingi kwa miaka 10. Hawa ambao hawapati fursa za kuendelea wanakwenda wapi? Rasilimali hii ya Taifa inaenda wapi? Na hapa ndiyo tunapokuja kuhitaji ufundi stadi na ufundi mchundo.
Naomba kuipongeza Serikali yangu kwa kuamua kuunganisha Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi na VETA lakini hapo hapo Serikali ya chama changu, Serikali ya Chama cha Mapinduzi iliahidi kujenga Vyuo vya VETA katika kila Halmashauri ya Wilaya tangu mwaka 2005. Mheshimiwa Waziri, mimi ninaimani kubwa na wewe, naomba usimamie suala hili litekelezwe. Zijengwe hizo VETA katika kila Halmashauri ya Wilaya ili tuwape vijana wetu stadi za maisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeomba kutoa ushauri katika suala hili kwamba tuamue kugeuza Jeshi la Kujenga Taifa yaani JKT liwe VETA kwa maana ya kwamba kila kwenye Jeshi la JKT tusajili VETA. Vijana wetu wanapoenda kusoma miaka miwili, mwaka mmoja waweze kupewa skills maalum za maisha na baada ya hapo waweze kupewa mikopo ya vifaa, hii itawajengea wenyewe uwezo wao wa kufanya kazi na tutajenga Taifa la watu ambao wanapenda kufanya kazi wao kwa wao, kujiajiri au kuajiriwa na Mheshimiwa Waziri, ningeomba suala hili la VETA liwe mpango maalum na lisimamiwe na Jeshi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa naomba kuzungumzia walimu. Naomba kuzungumzia walimu wa kada maalum, walimu wa awali kwa maana ya chekechea mpaka darasa la kwanza, kuanzia darasa la kwanza mpaka la tatu. Walimu hawa wawe na mafunzo maalum, wapewe motisha maalum na Vyuo Vikuu vitoe shahada maalum kwa walimu hawa ili tuweze kuwajengea uwezo watoto wetu wanaokua kuanzia chekechea mpaka darasa la kwanza, la pili na la tatu. Na hii tukifanya hivyo tutawapata watu wengi, watoto wetu watakuwa na mwanzo mzuri, wataweza kufanya kazi vizuri kwa bidii lakini pia walimu hawa wa kada maalum wawe walimu maalum na wawe na mishahara maalum siyo wanapewa mishahara ambayo haieleweki Mheshimiwa Waziri. Kwa kufanya hivyo, tutaibadilisha Tanzania yetu katika kizazi kimoja tu kwa kuwekeza kwa walimu, kwa watoto na let us .....
MHE. HALIMA A. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja.