Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Victor Kilasile Mwambalaswa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lupa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia kwenye hoja hii iliyo mbele yetu. Nataka kuchukua nafasi hii kumpompngeza sana Mheshimiwa Waziri, Manaibu Waziri, Makatibu Wakuu, Watendaji wote walioko kwenye Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii imechukua moja ya sita ya bajeti ya Serikali, moja ya sita, karibu trioni tano katika trioni 30, hii inaonyesha umuhimu wa Wizara hii. Wizara hii ndiyo inayoweza kutupeleka kwenye uchumi wa kati, Wizara hii ndiyo ina miundombinu yote ambayo inachochea kukua kwa uchumi. Kwa hiyo, naomba Wizara hii wajue kwamba wanadhamana kubwa sana ya kuivusha nchi hii kwenda kwenye uchumi wa kati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaongelea vipengele vitatu, vinne, cha kwanza niongelee Bandari, naipongeza sana Serikali kwa kuamua kuboresha Bandari zetu, Bandari ya Dar es Salaam, Bandari ya Mtwara, Bandari ya Tanga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kiongozi mmoja wa nchi jirani amewahi kutania, akasema, Tanzania nipeni Bandari ya Dar es Salaam niiendeshe, nitawapeni bajeti yenu yote. Hakuwa anatukejeri, ana maana kwamba, kwa jinsi ya uchumi wa jiografia ulivyo, Bandari zetu zimekaa kimkakati sana. Kwa hiyo, naipongeza sana Serikali kwa kuziboresha bandari hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali, Wizara, tusiboreshe miundombinu peke yake, tuboreshe na huduma. Wizara hii imejaa wasomi wengi waliobobea, wana taaluma, tufanye utafiti, tuangalie je, kwenye bandari ambazo tunashindana nazo, Mombasa, Beila, Duban, vitu gani ambavyo wafanyabishara wanakimbilia kule ili na sisi tuviboreshe kwetu? Kwa hiyo, naomba tusiboreshe miundombinu peke yake, tuboreshe na huduma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee reli. Naishukuru tena vilevile Serikali kwa kujenga reli mpya Standard Gauge na kuboresha reli ya zamani Miter Gauge, naishukuru sana. Naishauri Wizara kila inapowezekana wanunue rolling stock ambayo unaweza ukatumia kwenye reli zote ili kuweza kupunguza gharama. Wanunue rolling stock ambayo unaweza ukatembeza kwenye Standard Gauge na vilevile rolling stock ambayo unaweza ukatembeza kwenye Meter Gauge na vilevile hata unaweza kutembeza kwenye Cape Gauge kwa reli yetu ya TAZARA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii reli ya kati Standard Gauge ikitumiwa vizuri inaweza kubeba tani ya mizigo zaidi ya milioni 20 kwa mwaka na hapo ndiyo itachochea kukua kwa uchumi wetu. Sasa nimefurahi sana kuona kwenye bajeti ya mwaka huu Mheshimiwa Waziri amesisitiza reli hii ya kutoka Uvinza kwenda Msongati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Msongati Burundi kuna Nickel zaidi ya tani milioni tano, tuna Platinum zaidi ya tani milioni sita, saba, reli hii itabeba mizigo hiyo. Namshauri Mheshimiwa Waziri aanze kuwa-engage Mawaziri wenzake wa Burundi na Kongo ili reli ya ina hiyo ijengwe kuto Msongati kwenda kwenye bandari ya Uvira. Hapo tutakuwa tume- capture mizigo ya Burundi na mizigo ya Kongo, wakati hii ya kutoka Isaka kwenda Kigali ina-capture mizigo ya Rwanda na mizigo ya Central African Republic. Umuhimu wa reli hii ni katika kubeba mizigo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee reli ya TAZARA. Reli hii inahitaji maboresho madogo sana, lakini shida ya reli ya TAZARA nadhani ni sheria. Reli hii ilijengwa na Serikali ya Awamu ya Kwanza, lengo lilikuwa kuisaidia Zambia ambayo ilikuwa Landlocked wakati tunapigania uhuru wa nchi za Kusini mwa Afrika, ilikuwa ya muhimu mno, lakini leo inaonekana kwa majirani zetu reli hiyo haina umuhimu, ndiyo maana inatusumbua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Waziri aiangalie sheria na mkataba kwa reli hii ili ikiwezekana alete sheria hapa Bungeni tuweze kuirekebisha iende na wakati ambao tunautaka kwa sababu Tanzania tunaitaka kwa kukuza uchumi wetu. Wenzetu sasa hivi wanategemea Bandari ya Durban na Bandari ya Beira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nakuomba sana Mheshimiwa Waziri aiangalie sheria ailete Bungeni tuweze kuiboresha kwa manufaa ya Tanzania zaidi. Ilikuwa kwa manufaa ya wenzetu, naona wenzetu hakuna umuhimu, sasa tuiboreshe kwa manufaa ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hilo hilo la reli ya TAZARA pale Inyara, Mheshimiwa Mbunge wa Mbeya Vijijini anaiongelea sana. Naiomba Serikali iweze kujenga pale bandari kavu ili mizigo ifike pale, ili baadaye tuweze kujenga reli kutoka Inyara kwenda Itungi Port kwa ajili ya mizigo ya Malawi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alifanya ziara nchini Malawi hivi karibuni. Namshukuru sana, maana yake ziara yake hiyo imerudisha mahusiano ya kibiashara kati ya Tanzania na Malawi kwenye reli nzuri. Ninamshukuru sana. Akiwa huko pamoja na Rais mwenzie walishauri kwamba Mawaziri waunde tume ya mashirikiano ya pamoja. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri anayehusika waunde haraka tume hiyo kwa sababu Awamu ya Kwanza iliisaidia sana Malawi, ilijenga Cargo Centers; Dar es Salaam, Cargo Centers, Mbeya, lakini hizo Cargo Centers hazifanyi kazi. Kwa hiyo, biashara kati ya Tanzania na Malawi imekufa kinyemela nyemela.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Serikali ifufue hizo Cargo Centers haraka ili biashara kati ya Tanzania na Malawi iweze kuendelea kama kawaida. Kuna wenzetu nchi za majirani ambao bandari zao zimepata msuko msuko kidogo. Kwa hiyo, naomba bandari zetu zichukue hiyo kama ni opportunity ili kuweza ku-capture biashara hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee barabara kidogo. Mheshimiwa Rais akiwa Mkoani Mbeya aliongelea barabara ya mchepuko, kutoka mlima Nyoka kwenda Mbalizi, aliongelea na uwanja wa ndege wa Songwe na aliona umuhimu wa barabara hiyo, maana yake aliona msongamano uliopo Mbeya Mjini ni mkubwa sana. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa aweke umuhimu sana kwa barabara hiyo ya mchepuko ya kutoka Mlima wa Nyoka kwenda Mbalizi na vilevile kuboresha barabara ya kati ambayo sasa hivi ina lane mbili aiboreshe iwe lane nne kuweza kupunguza msongamo pale Mbeya Mjini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ziara ya Mheshimiwa Rais nilibahatika sana, Mheshimiwa Rais alifika Chunya kufungua barabara ya Mbeya - Chunya na pia kuweka jiwe la msingi barabara Iinayojengwa sasa hivi kwa kiwango cha lami ya kutoka Chunya kwenda Makongorosi. Wananchi wa Chunya wanamshukuru sana Mheshimiwa Rais, wanamshukuru sana Mheshimiwa Waziri na wanawashukuru sana Watendaji wote wa Wizara hii ya Ujenzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ziara hiyo Architect Mwakalinga na Engineer Mfugale nilikuwa nao pale tukanywa nao chai, waliiona barabara hiyo ambayo wamenizawadia, lakini pale mlimani waliona kuna matundu mawili, matatu ambayo yanachafua barabara hiyo ambayo ni nzuri sana ambayo kwetu sisi ni mboni ya jicho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Architect Mwakalinga na Eng. Mfugale watununulie weighbridge, hata kama ni mobile weighbridge kwa sababu huko Chunya tuna mazao mengi ya misitu, tuna mazao mengi ya tumbaku. Wafanyabiashara huwa wanaweka malori makubwa ya lumbesa usiku, wanapita kwenye barabara hiyo wanaiharibu, wakifika Mbeya ndiyo wanagawa kwenye malori mawili matatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nawaomba sana hawa Mainjia wanisaidie sana, watusaidie Chunya, watununulie hata mobile weighbridge kuweza kuiokoa barabara hii idumu kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi, naunga mkono hoja. (Makofi)