Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Yahaya Omary Massare

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manyoni Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii nami nichangie katika Wizara hii ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, ambayo ni muhimu sana kwa uchumi wa nchi yetu. Niendelee kupongeza kama walivyopongeza Wabunge wenzangu kwa utendaji mzuri wa Mawaziri, Mheshimiwa Waziri Kamwelwe, wasaidizi wake, Manaibu Waziri wote wawili, Katibu Mkuu wa Wizara hii na Watendaji wote katika Wizara hiyo. Wamekuwa wakifanya kazi nzuri, lakini zipo changamoto ambazo tunatakiwa tuwasaidie na kuendelea kuishauri Serikali kuona namna iliyo bora ya kufanya sasa nchi hii iweze kukaa vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii inasimamia suala zima la barabara. Suala la barabara, dhamira ya Serikai na Ilani ya chama cha Mapinduzi ni kuunganisha Mikoa yote kwa njia ya barabara za kiwango cha lami. Tunayo barabara moja katika Mkoa wa Singida inayounganisha Mkoa huu wa Singida na Mkoa wa Mbeya. Ametoka kuzungumza sasa hivi mwenzangu hapa ambaye nimepakana naye, Mheshimiwa Mwambalaswa, kule kwake wanajenga barabara hiyo hiyo kwa kiwango cha lami. Awamu ya kwanza walianza Mbeya kwenda Rwanjilo, ya pili Rwanjilo kwenda Chunya, sasa wanajenga kutoka Chunya kwenda Makongorosi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutoka Mkoa ambao tunapakana nao mwaka 2017 barabara hii ilipata mkandarasi, ilitangazwa mchakato ukaisha. Mheshimiwa Rais alipokuja Itigi mwezi wa Saba tarehe 25 alikuta tatizo katika barabara hii. Mchakato ulionekana una harufu ambayo siyo nzuri, akazuia, akasema kwamba kwa pesa ambazo zinatolewa, aidha, mkandarasi afanye negotiation na TANROADS waongeze kilometa au kilometa zipunguzwe kulingana pesa na mchakato ambao ulikuwa umeingia katika mkataba ule,

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuanzia 2017 mpaka leo hii waliposhindana kwenye mazungumzo mkandarasi mwaka 2018 aliondoka. Mwaka 2018 katika bajeti iliyokwisha ikaoneshwa kwamba barabara hii iko katika mpango wa kujengwa. Katika kitabu hiki ukurasa wa 181 barabara hii imeoneshwa kwa pesa kiduchu ambazo zimeoneshwa katika jedwali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hofu yangu, wananchi wa Mkoa wa Singida Jimbo la Manyoni Magharibi, aidha watanichukua mimi Mbunge wao au wataichukia Serikali yao, kwa sababu hawajaambiwa neno la ukweli toka mwaka 2017. Naiomba Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi, Mawaziri mlioteuliwa, Mheshimiwa Waziri Kamwelwe, mnaaminiwa na Mheshimiwa Rais, barabara hii hata wewe Mheshimiwa Waziri inakufaa sana. Kwenda kwako kule badala ya kupita Tabora utapitia Itigi, utakwenda Rungwa, Rungwa - Ipole, Ipole unakwenda Mpanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii kama hutaijenga Mheshimiwa Waziri maana yake unataka nami mwakani nisiende kuomba kura; au nikiomba kura nitapata taabu sana namna ya kuwaeleza wananchi waelewe. Namwomba Mheshimiwa Waziri barabara hii niliiona humu basi mwaka huu tuone mkandarasi anapatikana na ujenzi unaanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri wataalam wote wako hapa, Katibu Mkuu yuko hapa. Eng. Nyamwanga alishafikisha pazuri sana barabara hii katika kutaka kuijenga, lakini Katibu Mkuu mpya naamini ni msikivu, Eng. Mfugale uko hapa, mimi ndiyo natoka Itigi, siku ile ulikuwepo pale. Naomba sasa masikio yako yarudi yafunguke yaone ahadi ya Mheshimiwa Rais kwa wananchi wale. Tunawategemea ninyi, 2015 tunakwenda katika Uchaguzi wa Vijiji mwaka huu, tunataka tushinde vijiji vyote. Nami naahidi nitasimama imara CCM itashinda vijiji vyote, lakini hili litaweza kuja kutugharimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naona Mheshimiwa Waziri ananiangalia, naamini hili limeingia. Naomba tu mnisaidie, nami sitaongea tena suala la barabara. Tusaidiane, barabara hii ina maslahi mapana na watu wa Mkoa wa Singida, Katavi na Mbeya. Makao Makuu ya Serikali yako Dodoma. Mtu wa Katavi anapokuja Dodoma, akipita Tabora anaongeza urefu wa safari, lakini ukipitia Rungwa - Itigi ni kwepesi, hata Mheshimiwa Mwambalaswa atakuwa hawezi kuzungukia tena Makao Makuu yake ya Mkoa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niendelee kuipongeza Serikali kwa kazi kubwa inayofanya ya ujenzi wa reli kwa kiwango cha Standard Gauge. Sisi watu wa Mkoa wa Singida reli inapita Itigi katika eneo langu. Naomba tu juhudi ziendelee, lakini kwa hakika tunafarijika sana na kazi inayofanywa na Serikali hii kupitia Wizara yenu hii. Hayo mengine tunasema ili nanyi mtuone.

Mheshimiwa Mwenyekiti, liko suala la minara ya simu. Suala hili linaonesha kuna shida kidogo. Mwaka 2018 karibu na bajeti tulipitishiwa makaratasi hapa ya kuonesha mnara utajengwa mahali kadhaa, mahali kadhaa; na mwaka huu umekuja mpango ule ule. Ile ya mwaka 2018 haujajengwa, lakini mwaka huu umekuja utaraibu ule ule. Sasa naomba sana Waheshimiwa Mawaziri mnapokuja na yale makaratasi na kuchukua majina, basi tuone yana-reflect kwa wananchi wetu. Ukishaniambia mimi, nami nikifanya mikutano, nawaambia wananchi hapa Serikali inaleta hiki. Sasa ninapokwenda kwa mara nyingine tena nakuja na story inakuwa haipendezi na hasa sisi wenzenu wa upande huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwa kazi nzuri inayofanya, lakini niunge mkono hoja hii kwa asilimia mia moja ili mkipata pesa mkatekeleze miradi hii ambayo mmeiomba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naunga mkono hoja hii. (Makofi)