Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Daniel Nicodemus Nsanzugwako

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kasulu Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, kwanza nianze kwa kuwapa pole familia ya Mzee Mengi na Watanzania wote kwa kuondokewa na Ndugu Mengi. Kwetu sisi watu wa Kigoma huyu alikuwa Shemeji yetu kwa hiyo tunatoa pole nyingi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini naomba kwa namna ya pekee pia Mheshimiwa Waziri wewe nikupongeze Injinia Kamwelwe na Manaibu wako Injinia Nditiye na Mhasibu aliyebobea Ndugu Kwandikwa, Makatibu Wakuu wote, Architect Mwakalinga ambaye ni mgeni kwenye Wizara ameanza vizuri, anafanyakazi vizuri na Makatibu Wakuu wenzake Ndugu Chamliho na wenzake Mama Sasabo na Jimmy Yonasi wote tunawapongeza kwa kazi nzuri ya kusimamia wenzao katika maeneo hayo. Wizara mko vizuri, Mheshimiwa Waziri mko vizuri, tunawapongeza Watendaji wote kwa maeneo yote, maeneo ya anga, maeneo ya barabara, maeneo ya majini, mawasiliano kwa kweli wako vizuri watendaji, cha msingi ni kuwatia moyo. (Makofi)

Mheshimiwa mwenyekiti, nitakuwa na mambo machache kwa sababu hii ni Kamati yangu na mambo mengi tumeyadadavua kwenye Kamati. Ningependa tu mambo matatu ya haraka haraka:-

(i) Mheshimiwa Waziri asubuhi nilikuuliza swali kuhusu SGR; sisi tunaoelewa vizuri mambo haya, ujenzi wa standard gauge ni mradi wa msingi sana, sana, ndiyo roho ya Nchi, ndiyo roho ya uchumi wa Taifa hili. Nimekuuliza moja ya matawi yake ni kutoka Uvinza kupita Kasulu kwenda Msongati na hatimae Uvira ya Congo kuchukua mzigo mkubwa ulioko katika Jamhuri ya Congo. Ukanijibu kwamba nisiwahishe shughuli kwamba iko kwenye hotuba yako. Kwenye hotuba yako nimeangalia hakuna hata msitari umezungumzia juu ya hilo tawi la SGR. (Makofi)

Mheshimiwa Waziri nikukumbushe tu na watendaji wako; reli hii ya SGR tunayoijenga ambayo ni uamuzi wa busara sana wa Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli ni mradi mzuri sana sana. Lakini faida yake, kazi yake ni kubeba mizigo mizito na mizigo mizito mingi Mheshimiwa Waziri kwa takwimu zilizopo, mzigo mkubwa katika nchi zinazotuzunguka uko katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Ni matumaini yangu kwamba Mheshimiwa Waziri utakapokuja hapa utatuleza hili tawi la Uvinza-Msongati kwenda mpaka Uvira ya Congo mtaanza lini hata angalau basi hata upembuzi yakinifu wa njia hiyo maana hatimaye tunataka SGR hii iwe na maana pana ya kiuchumi kwa Taifa letu.

(ii) Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo jingine ambalo ningependa lizungumze na hili tunalizungumza siku zote ni barabara; Sera ya barabara inajulikana, Mheshimiwa Waziri nikukumbushe tu na Watendaji wako kwamba Sera yetu ya barabara hasa barabara kuu ni kuunganisha Makao Makuu ya Mikoa na Makao Makuu ya Mikoa. Waziri unajua na watendaji wako wanajua kwamba katika Mikoa mitatu ambayo haijaunganishwa Makao Makuu kwa barabara za lami ni pamoja na Mkoa wa Kigoma, Mkoa wa Katavi na Mkoa wa Katavi unaotoka wewe nakumbushwa hapa na Mkoa wa Morogoro kwa maana Morogoro na Lindi. (Makofi)

Mheshimiwa Waziri najua ziko juhudi kubwa sana zinafanywa kutuunganisha sisi na Tabora, ziko juhudi zinafanywa kutuunganisha sisi na Mkoa wa Katavi, ziko juhudi kubwa zinafanywa kutuunganisha sisi na Mkoa wa Kagera pamoja na Shinyanga yake lakini bado bado speed ni ndogo sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia hotuba yako Mheshimiwa Waziri, ukiangalia barabara kwa mfano ya Nyakanazi hiki kipande cha Nyakanazi kuja mpaka Kabingo, barabara imeanza kujengwa kwa miaka kumi lakini mpaka sasa ni asilimia 60 tu basi ya utekelezaji wake na hoja iliyoko hapa Mheshimiwa Waziri ni kwamba mkandarasi yuko site lakini anasema hana fedha. Ushauri wangu kwako na kwa Wizara na kwa Serikali, hamna sababu ya kuanzisha miradi mipya kama miradi ambayo tayari ina Wakandarasi haisogei kwenda mbele kwa sababu ya uhaba wa fedha, kupanga ni kuchangua Mheshimiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi ambayo imeshaanza ina wakandarasi, miradi hii ikamilike ndio tuanze na miradi mingine haina maana kuwa miradi nusu nusu viporo kila pahala wakati haikamiliki, haiwezekani barabara ya Nyakanazi, Kabingo miaka 10 asilimia 60. Halikadhalika barabara ya Kidahwe kuja Kasulu kidogo umepiga ahatua asilimia 70 lakini miaka 10 unajenga kilometa 63 tafsiri yake ni kwamba kila mwaka unajenga kilometa tatu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kwa Serikali na hasa kwa Wizara na Mheshimiwa Waziri naomba hili ulichukue seriously niwaombe sana nasema tena hakuna sababu ya kuanzisha miradi mipya kama iliyopo haijatekelezeka, inakuwa haina maana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafahamu kuna juhudi kubwa ya fedha za African Development Bank kwa barabara ya Kabingo, Kibondo, Kasuli Manyovu ni juhudi kubwa na leo kama kumbukumbu zangu ziko sahihi leo tarehe 9 zabuni zimefunguliwa kuwapata wakandarasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni matumaini yangu kwamba sasa mradi huuutasogea kwenda mbele na haitakuwa tena hadithi kama ambavyo tumezoea, na sisi watu wa Mkoa wa Kigoma tumekuwa tuna mashaka kila mara miradi inaanzishwa lakini inasuasua sana katika ukamilishwaji wake. Nikuombe Mheshimiwa Waziri tumechoka kusubiri watu wa Kigoma wanataka miradi hii ikamilike na wanufaike nayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo jingine ambalo ningependa nilizungumze ni bandari ya Katosho najua kuna juhudi zinaendelea kujenga bandari ile tunataka pia mkandarasi yule nasikia ameshapatikana mkandarasi lakini mpaka leo hakuna ambacho kinaendelea mpaka sasa hivi ni matumaini yangu kwamba ile bandari ya nchi kavu imeshalipiwa fidia ni matarajio yangu kwamba sasa mkandarasi ataingia kazini na bandari ile iweze kukamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikukumbushe Mheshimiwa Waziri ujenzi wa airport ya Kigoma kupitia fedha za European Investment Bank taarifa tulizonazo sisi watu wa Kigoma na kupitia kwenye vikao vya RCC ni kwamba mkandarasi ameshapatikana tangu mwaka 2018 lakini bado hajakabidhiwa eneo la kufanya kazi, matatizo yaliyokuwepo mara ya makaburi yameshakamilika yameshakwisha nafikiri ni jukumu la Wizara sasa kufanyia a thorough follower up ili mradi ule sasa uanze na taarifa tulizonazo ni kwamba wenzetu wa European Investment Bank tayari hawana kikwazo sasa baada ya kuwa mgogoro uliokuwepo umekamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kidogo pia kuhusu bandari ya Dar es Salaam na bandari ya Mtwara. Tulibahatika kutembelea bandari hizi nikuombe Mheshimiwa Waziri jilidhishe na matatizo tuliyoyaona katika bandari ya Mtwara na matatizo ya kiutendaji tuliyoyaona katika bandari ya Dar es Salaam, dawa ya tatizo ni kuliondoa sio kujificha kwenye kichaka na hii tabia ambayo imeanza kuzuka ukisema jambo basi watu wanasema huyu bwana kahongwa kapewa fedha msitafute vichaka vya kujifichia kuna matatizo ya kimkataba katika bandari ya Dar es Salaam, matatizo haya mkae chini kaa na watendaji wako Engineer Kakoko yupo na wenzake mkae mezani muyamalize matatizo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaona matatizo ya usanifu kule Mtwara kaeni na wataalam, kaeni na Engineers waliopo muweze kuyaondoa matatizo haya. Na kama hii dhana ya kuanza kufikiri kwamba kila likisemwa jambo basi mtu amehongwa linakuwa kwa kweli ni kujipofusha sisi wenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ningezungumzia kuhusu Mamlaka ya Viwanja vya Ndege na hiyo kampuni ya PUMA Energy Tanzania. Mheshimiwa Waziri nakupa nakushauri tu pata muda wa kuifahamu kampuni hii ya PUMA Energy nimekuwa Mkurugenzi kwenye kampuni miaka saba na nilikuwa ndio Mwenyekiti wa Kamati ya Ukaguzi, hii ni kampuni ya Serikali asilimia 50 za PUMA Energy ni Serikali ya Tanzania na ni hisa za kihostoria. Hizi hisa alipewa mwalimu Nyerere mwaka 1966 na Malikia wa Uingereza lakini napata shaka kwamba Mheshimiwa Waziri huelewi vizuri kwamba hii kampuni ya PUMA ni kampuni ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeshauri sana Mheshimiwa Waziri una TR, kuna watu wa HAZINA kaeni chini hii kampuni ni ya kwetu imelipa dividend kwa miaka minane mfululizo. Sasa taarifa nilizonazo ni kwamba ina vikwazo vingi sana na Mheshimiwa Waziri umeonesha kutoipenda kampuni hii, sasa nikuishauri tu kwamba usimchukie mtoto wako kaa na Mamlaka, kaa na TR muweze kuelewa vizuri juu ya jambo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nikukumbushe tu Mheshimiwa Waziri naunga mkono hoja hii lakini niseme jambo moja kwa ruhusa yako nusu dakika tu kwamba ahadi zinatolewa na viongozi kuna ahadi zimetolewa 2017 hazijatekelezwa na kuna ahadi zimetolewa 2019…

MWENYEKITI: Ahsante mengine muandikie.

MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Niombe sana Mheshimiwa Waziri jambo hili. Naunga mkono hoja hii. (Makofi)