Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Mary Pius Chatanda

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Korogwe Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia hotuba hii ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasialiano. Kwanza, naunga mkono hoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Waziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu na watendaji wote wa Wizara hii. Vile vile nampongeza Meneja wangu wa TANROAD wa Mkoa wa Tanga kwa kazi nzuri ambayo ameendelea kuifanya ndani ya Mkoa wetu wa Tanga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona kwenye kitabu nimetengewa fedha kwa ajili ya kujenga madaraja; daraja la silabu moja ambalo linakwenda Old Korogwe kwenda Bombo Mtoni ile barabara ya kwenda Bombo mtoni na silabu mbili ambalo ni Maguzoni kwenda Old Korogwe. Naomba nichukue nafasi hii kushukuru kwani nisiposhukuru katika hili, nitakuwa sijamtendea haki Meneja wangu wa Mkoa kwa sababu eneo hili ni sugu na sasa hivi mvua zinanyesha pale Korogwe, huwa mara nyingi kunatokea mafuriko makubwa pale Old Korogwe. Kwa hiyo, kwa kitendo cha kutengewa hizi fedha, niombe sana basi fedha hizi zikitoka iende ikafanye kazi ili kusudi wananchi wa Old Korogwe waondokane na yale mafuriko ambayo wanayapata kila mwaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie barabara inayotoka Old Korogwe - Kwamote kwenda Kwashemshi – Dindira – Bumbuli - Soni, nimeona imeandikwa humu. Marehemu Profesa Maji Marefu alikuwa anaizungumzia sana barabara hii, iliwekwa kwenye Ilani ya Uchaguzi lakini naona wameweka hapa kwa ajili ya upembuzi yakinifu. Niwaombe sana fedha hizi zikipatikana, huu upembuzi yakinifu uende ukafanye kazi kwa sababu ni miaka 15 sasa tunasikia tu upembuzi yakinifu; hata watu wa milimani wanahitaji barabara za lami. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nimwombe Waziri pamoja na kututengea fedha hizi, fedha hii itoke ili kusudi ikafanye hiyo kazi ya upembuzi yakinifu, isiwe kila baada ya miaka mitano inaandikwa tu kwamba upembuzi yakinifu. Niombe sana barabara hii ni muhimu kwa uchumi na utalii. Barabara hii inazalisha kwa maana ya Kata zilizopo kule milimani kwa Korogwe Vijijini wanazalisha hiliki, maharage na chakula chungu nzima, kuna soko kubwa pale chini. Niombe sana safari hii naomba ifanyike hii kazi ili kusudi na watu wa milimani waweze kuonja barabara za lami. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba barabara ya Old Korogwe – Kwa Mndolwa – Bombo Mtoni – Maramba – Mabokweni, nayo iingizwe angalau kwenye upembuzi yakinifu. Hii barabara nayo ni ya kiuchumi, mkitusaidia barabara hii itasaidia masuala ya kiutalii na kiuchumi. Pia ni barabara muhimu sana kiusalama, endapo kunakuwa na jambo lolote kwa hizi barabara zilizopo huku mjini barabara hii itatumika. Kwa hiyo, naomba sana Mheshimiwa Waziri barabara hii muitazame kwa jicho la huruma angalau na yenyewe iingie kwenye upembuzi yakinifu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niombe barabara ya Old Korogwe – Rwengela Darajani – Maguzoni nayo ianze kutazamwa. Barabara hii ikitokea pale Maguzoni, maana akitoka Tanga akija Maguzoni, anakuja Rwengela Darajani anatokea moja kwa moja Korogwe kwenda Arusha. Barabara hii kwanza inafupisha mwendo wa mabasi kuzunguka kutoka Tanga kupitia Segera lakini vilevile ni barabara ya kiuchumi. Engineer wangu Ndumbaro anaijua barabara hii, naomba sana ikiwezekana na yenyewe iwekwe kwenye mpango angalau wa upembuzi yakinifu ili iweze kuwekwa lami, hayo ndiyo maendeleo yenyewe tunayapeleka vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie suala la TBA. TBA wanakabidhiwa miradi mingi ya ujenzi lakini inaonekana kabisa kwamba kazi wanazopewa ni nyingi kuliko uwezo wao. Mimi niko kwenye Kamati ya LAAC, tumekwenda kutembelea miradi pale Kahama, tumekuta kuna mradi ambao wamepewa kuujenga hawajaukamilisha na wameutelekeza hapo na fedha wamepewa wanakwenda kujengea miradi mingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenykiti, kwa bahati mbaya sana TBA wanaonekana hawana fedha, wanasubiri wapewe fedha ndipo waende wakajenge miradi. Kwa kufanya hivyo tunachelewesha miradi, TBA ni lazima iwe na fedha za kwenda kufanyia hiyo miradi siyo wanapewa kazi halafu ndiyo itafutwe fedha waende wakatengeneze ile miradi. Kwa hiyo, naomba sana TBA ikiwezekana wapunguziwe miradi waliyopewa kwa sababu uwezo wa kuikamilisha hawana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nisaidiwe; kutoka pale Kwa Meta kwenda Kwa Mndolwa kumewekwa alama za X kwenye nyumba za wananchi. Nataka nielezwe; hawa wananchi wamewekewa alama za X toka 2016 na mwaka huu tena kuna nyumba zingine zimeenda kuwekewa alama za X, sijajua labda ndiyo hili ombi ninaloomba kwamba mnataka kufanya upembuzi yakinifu kwa ajili ya kuweka lami, kama sivyo basi mniambie mmeweka alama za X kwa ajili ipi na kama hawa wananchi wangu waliowekewa alama za X watalipwa au hawatalipwa? Kwa sababu mmesitisha wasiendelee kujenga kwenye yale maeneo ambayo wamewekewa alama za X, kwa hiyo, wameacha kufanya maendeleo katika nyumba zao. Sasa niombe mniambie kwamba kwa kuwekewa alama zile za X watalipwa ili waweze kuendelea na shughuli zingine? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii kushukuru, nimeona tumetengewa fedha kwa ajili ya kufunga mitambo ya ulinzi na usalama katika viwanja vya ndege pale Tanga. Pamoja na hilo, tunaomba basi tutengewe fedha ili uwanja ule uweze kukarabatiwa kama vinavyokarabatiwa viwanja vingine. Na sisi tunahitaji bombadier itue pale Tanga, tunaihitaji sana. Kwa hiyo, pamoja na kuweka hivyo vifaa vya ulinzi lakini iwe ni pamoja na kufanya ukarabati wa kutosha ili bombadier iweze kutua pale Tanga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nishukuru Serikali kwa kazi kubwa ambayo wameifanya ya ukarabati wa reli ile ya kutoka Tanga – Korogwe – Mombo na kuendelea huko mbele. Tumeona kabisa kazi nzuri ambayo inafanyika, naipongeza sana Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuwa sijatenda haki endapo sitampongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa ambayo amekuwa akiifanya lakini kwa maamuzi ambayo ameyafanya ya uthubutu wa kutekeleza miradi mbalimbali kama vile ya ujenzi wa Reli ya Standard Gauge, ujenzi na ukarabati wa viwanja vya ndege…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Malizia Mheshimiwa Chatanda.

MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, naunga mkono hoja. (Makofi)

Whoops, looks like something went wrong.