Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Riziki Saidi Lulida

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. RIZIKI S. LULIDA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nikushukuru sana na niwashukuru Spika, Naibu Spika, Katibu wa Bunge, wafanyakazi wa Bunge na Wabunge wenzangu kwa kunisaidia na kunitoa huzuni kipindi kigumu cha kupata msiba wa mtoto wangu ambaye alifariki. Nawe Naibu Spika ulikuwa mmoja wapo wa waliokuwepo mpaka tunasafirisha mwili wa marehemu kupeleka Dar es Salaam na tumezika, nashukuru Alhamdulillah. Mwenyezi Mungu awawezeshe na awalinde na Mwenyezi Mungu wote anasema Inna lillah wainnailayhi rajiuun na kila nafsi itaonja umauti (kullu nafsin dhaikatul–maut).

Mheshimiwa Naibu Spika, niwapongeze Waislamu wote Tanzania na wasiokuwa Waislam kwa mwezi Mtukufu wa Ramadhan, nawatakia Ramadhan Kareem na Mwenyezi Mungu atujaalie katika Mwezi Mtukufu huu ailinde nchi yetu iingie katika amani, tusidhoofishwe na mabeberu ambao wanataka kutugawanisha na kutuweka katika mazingira magumu. Tanzania yenye amani inawezekana. Nashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema haya, nitazungumzia suala la barabara, lakini hasa nataka nizungumze kwa dhati ya moyo wangu kuwa, kuna ubaguzi mkubwa unatendeka kwa kupitia Mawaziri wetu katika ugawaji wa barabara. Barabara haitakiwi kuonekana upande mmoja unapewa priority na upande mwingine unaachwa ukiendelea kulalamika kila mwaka. Hii haileti ufanisi na umoja tuliokuwa nao katika Tanzania hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nizungumzie Mkoa wa Lindi katika mikoa nane ya ukoloni, tulikuwa katika mojawapo ya province nane za Tanzania, lakini leo kwenda Liwale, Liwale ni Wilaya ya zamani sana, inakuwa kama wako kisiwani. Watu wa Liwale wako Guantanamo. Leo mvua inanyesha inawachukua miezi mitatu mtu wa Liwale aweze kuja Dar es Salaam, akipata ugonjwa Liwale hawezi hata kwenda Lindi, jamani tufike mahali tusema basi tufunge ukurasa. tumelalamika barabara ya Liwale toka Waziri Mkuu wa Jimbo la Liwale alikuwa Rashid Mfaume Kawawa, wanamuenzi vipi Kawawa katika Jimbo lake? Wanachofanya kipindi cha uchaguzi kutumia nguvu kubwa kutaka Jimbo, lakini je, wananchi wa Liwale wanawafanyia nini? Kwenda Liwale ni kama adhabu na mfanyakazi wa Tanzania akitaka kuadhibiwa mpeleke Liwale. Mfanyakazi wakijiona hawamtaki wampeleke Liwale kwa maana Liwale ni Guantanamo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimezungumza kwa miaka, nimepewa ahadi na Mawaziri kwa miaka, Mheshimiwa Mramba mpaka akasema mama mwaka huu ni wa mwisho nitakupelekea lami Liwale. Kwa masikitiko nataka niseme kitu kimoja kwamba, Bunge tutengue Kanuni ya kushika Msahafu au Biblia kwa kusema uongo humu ndani. Watu wanashika Biblia mwaka huu barabara itapatikana lisemwalo silo! Kwa nini tunashika Quran, kwa nini tunashika Biblia ikatuleta katika uongo, ina maana inatuingiza katika uongo na laana katika Bunge. Tutengue Kanuni, tutumie Katiba badala ya kutumia Quran maana Quran haitaki kusema uongo wala Biblia haitaki kusema uongo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais amezunguka Mtwara pamoja na mama Janeth, amesema kazi aliyoiona kwa barabara za kule kweli amehakikisha kwamba barabara ni mbovu, lakini kuna maeneo yanapata upendeleo, upendeleo kila mwaka, hii mpaka lini? Leo kwenda Liwale unaona Liwale mpaka Nachingwea barabara kubwa kiuchumi katika mikoa inayozalisha korosho, ni mikoa miwili ambayo na wa tatu ni Ruvuma. Wa kwanza ni Mtwara, wa pili Lindi na wa tatu ni Ruvuma. Asilimia 80 ya korosho ambayo ni uchumi mkubwa katika nchi hii inatoka sehemu hizo, lakini hakuna barabara. Wanalalamika kuhusu kangomba, mtu yuko kijijini, anaitoaje korosho yake kijijini kupeleka katika magulio wakati hakuna barabara, sasa wale walanguzi wanakwenda kuchukua kule kwa ku-risk na magari yao kutoka kule mpaka kufika mjini, leo wanawakamata watu kwa ajili ya kangomba, lakini je, wamewawekea barabara? Huwezi kumkata mtu bila kumwekea alternative, kunatakiwa kuwepo na alternative, barabara ziwepo vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo mikoa ambayo ina uchumi mkubwa sasa hivi tumeona LNG inaenda sasa hivi, miradi inakamilika kutaka kujenga liquefied national gas industrial area ambayo itawekwa Lindi, lakini hatuna airport! Ni kilometa 20 only kutoka airport kuja Kilikong’o, hakuna bajeti ya airport, je, hawa wafanyabiashara wakubwa wanaokuja kuwekeza katika mradi mkubwa wa matrilioni wataruka na ndege kutoka Mtwara. Mtwara mpaka Lindi wakati Lindi uwanja wa ndege kwa taarifa ya Bunge wa Lindi ni wa pili katika Afrika. Ndege ya kwanza ilikuwa inatoka London inatua Misri – Alexandria inakuja kutua Lindi inakwenda Afrika Kusini, tuko wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wanawafanyia nini wananchi wa Mkoa wa Lindi? Kwa nini wanatudhalilisha wananchi wa Lindi? Tumefanya nini katika nchi yetu? Keki hii hii ya korosho na vitu vingine wengine wanafaidika zaidi kuliko kuyaangalia maeneo ambayo yana uchumi na uchumi bora katika nchi hii yametupwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Lindi, Mtwara na Ruvuma sasa hivi inabidi iwekewe EPZA yake ifanyiwe kazi kwa vile ndiyo mikoa ya kiuchumi, hakuna barabara. Utasikia barabara zinapeleka maeneo hata uchumi haupo na ubaguzi huu wa kupeleka fund nyingi katika maeneo mengine unauona kabisa. Tufike mahali bajeti isimame bila kuangalia pale paliposimama na maendeleo makubwa pasimame waende kwa maeneo ambayo watu ni maskini ili nao hawa wafaidike na sungura wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Bandari ya Lindi ilikuwa ni bandari kubwa. Leo je, bidhaa zitaanza kupatikana kutokana na miradi ya LNG, bandari iko wapi? Bandari iko Lindi, ukienda uani huwezi kuona utafikiri kichaka fulani tu, watu hata kuweka bajeti hamna, bajeti za kibaguzi, halafu wanakuja kutumia nguvu kubwa wakati wa uchaguzi maana yake ni nini? Haiwezekani! Wamefikia mahali wanawafanya watu wanakwazika kujiuliza na inakuwa ndiyo mahali pa watu kwenda kupiga vijembe, ninyi maskini, mikoa imetupwa, lakini ni kweli mikoa imetupwa. Nenda leo Liwale kuna nini, nenda leo Milola kuna nini? Kutoka Lindi kwenda Milola hakuna barabara. Milola kwenda Nangaru na daraja limevunjika huu mwaka wa ngapi hakuna kinachosemekana. Nawaomba mpaka na Mawaziri kaangalieni mazingira, hakuna mtu anaye-take action nini maana yake? Basi tuamueni turudi Tanganyika yetu, tukakae na Tanganyika yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, tulifikia mahali tuliamua kuchanga kwa ajili ya kusaidia Lindi yetu tukasema haiwezekani, Lindi itachangiwa na Tanzania nzima, kuna nini Lindi? Barabara za Lindi ziko wapi? Nenda vijijini huko watu wanatembea kwa mguu, wanajitwika mitenga ndiyo maana hata wanakuwa wafupi kwa sababu kutwa mtu ana tenga kichwani. Hali hii ya umaskini wanayoipeleka Lindi inasababishwa na Serikali. Naomba barabara zikasimamiwe, nikitoka hapa nataka mguu kwa mguu na Waziri wa Ujenzi twende tukaangalie barabara Lindi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumefika mahali tuseme wazi kuwa kuna maeneo mengine imetosha tupeleke mikoa ambayo iko maskini na mikoa ile barabara ipatikane, maji yapatikane, afya ipatikane, sio kwingine watu wanaburudika wame-leisure sisi wengine kwetu tunahangaika, tunatembea kilometa nyingi kwa miguu, kwa nini na wakati nchi hii ni yetu wote? Uchumi ni wetu wote, korosho yetu na mapato yapatikanayo kutokana na korosho ni ya Tanzania nzima, lakini sisi wenyewe tumewekwa nyuma tumekuwa kama boga, unasuka mkeka mwenyewe unalala chini. Hii haiwezekani na haikubaliki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, gesi sasa hivi naona tayari mikataba inapita maana yake naona ninapoona, lakini cha kujiuliza gesi ile maendeleo yake yako wapi, barabara zake za kupitisha vitu hivyo iko wapi? Inapita maporini humo hakuna kitu, hakuna barabara, mawasiliano yamekuwa magumu.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nasema ahsante imetosha. Tunataka Lindi yetu yenye barabara, Lindi yetu yenye afya, Lindi yetu yenye maji na hii inawezekana. (Makofi)