Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. David Ernest Silinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduma

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kupata nafasi ya kuchangia hotuba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha 2019/20.

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijazungumzia miradi ya kimkakati ya Kitaifa nitazungumzia mambo mawili madogo tu ya jimboni kwangu. Jambo la kwanza pamoja na shukrani ambazo zimetolewa za ujenzi wa Daraja la Momba ambalo limekamilika kwa karibu asilimia 97 na linatumika, sisi wananchi wa Momba tumefurahi sana, lakini tunaomba sasa ile barabara ya kutoka Mlowo – Kamsamba – Kiliamatundu ijengwe kwa kiwango cha lami kama ilivyo Ilani ya CCM ilivyoahidi, kama ilivyo ahadi ya Rais Mstaafu Mheshimiwa Jakaya Kikwete na Mheshimiwa Mkapa, wote waliahidi kujenga hiyo barabara lakini mpaka sasa hawajakamilisha. Barabara ya Kakozi – Kapele – Ilonga ambayo wameipandisha hadhi na hawajaifanyia kazi mpaka sasa, tunaomba ifanyiwe kazi haraka iwezekanavyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nahitai kuzungumzia masuala ya Kitaifa ambayo kimsingi yanaweza yasieleweke vizuri na ndiyo maana unajikuta mara nyingi tumekuwa tukigongana. Mradi wa SGR, thamani ya mradi wote wa reli ya SGR ni dola za Kimarekani 7,000,000,000 na maamuzi yameshafanyika ya kujenga reli yetu kutoka Dar es Salaam - Morogoro mpaka Dodoma kwa awamu ya kwanza kabla ya kwenda kwa awamu ya pili.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi tulishawaeleza Tanzania kwamba hatuna shida na reli inayojengwa, shida yetu ni namna mambo yanavyotekelezwa na nikasema hapa reli ambayo imejengwa, maamuzi ya awali yaliyofanyika chuma chote kinatoka China – nje ya nchi. Chuma kidogo ambacho kimekuwa kikinunuliwa hapa ndani ya nchi wamekuja watu wenye viwanda kwetu, watu wa viwanda vya chuma wamepewa vile vitani kama vya kudanganyishia, tani 1,000 au 2,000 basi, lakini chuma chote kimetoka nje ya nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa haya tunasema ni makosa ambayo tumeshayafanya kabla hatujawaza mapema. Nimeamua kulizungumzia hili kwa sabbau najua awamu ya pili ya kutoka Makutupora kwenda mpaka Mwanza itafuatia, lakini kabla hatujaenda katika huo mradi tuna mradi wa Liganga na Mchuchuma. Liganga na Mchuchuma endapo tungewekeza kwenye kutengeneza chuma chetu maana yake hii fedha ambayo tunaitumia kwa ajili ya reli yetu hapa nchini tungekuwa tunanunua chuma ndani ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa juzi ulisikia ripoti ya IMF. Ripoti ya IMF imeshusha uchumi wa Tanzania kutoka kasi ya kukua ya asilimia saba mpaka asilimia nne na sababu walizozitoa nafikiri kila mmoja amejaribu kuzisoma na Serikali walituambia hapa tusiwahishe shughuli, tukakubaliana na hilo jambo, lakini Serikali wamekuwa wakitaja hizo argument zao huko mtaani kwamba mbona IMF hawaja-include miradi mikubwa kwa mfano reli ya SGR katika uchumi wetu pamoja na ndege.

T A A R I F A

MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba pamoja na kwamba tunapokea taarifa aliyopewa, lakini hicho kilichozungumzwa hakiondoi taarifa zilizokuwepo mle ndani, hakiondoi! That’s the fact! Yaani bado ni asilimia nne, haiwezi kuondoa hiyo fact!

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ambacho nilikuwa najenga, nafikiri Mheshimiwa Waziri ambacho alitakiwa anielewe ni kitu kimoja na hii ndiyo shida ya hili Taifa. Moja ya ambacho nilikuwa nakizungumza maelezo ambayo wamekuwa wakiyatoa kwamba kwa nini hiyo miradi mikubwa haiwi included kwenye ile Taarifa ni kwa sababu kumekuwa na capital outflows kubwa yaani tunatumia fedha ya ndani, tunanunua kila kitu nje ya nchi na ndiyo maana uchumi wetu unashuka kwa sababu hatu-inject fedha ndani ya uchumi wa Tanzania. Tumepata mradi lakini fedha kwenye circulation haipo! Hiyo ndiyo tofauti ya kwetu sisi na Kenya. Kenya…

NAIBU SPIKA: Sawa, sasa Mheshimiwa Silinde ngoja twende vizuri kwa sababu Taarifa uliyokuwa umeizungumzia umesema ni ya IMF na barua tuliyosomewa ni ya IMF. Mimi naomba tuji…

(Hapa Mhe. Esther N. Matiko alikuwa akizungumza na Mhe. David E. Silinde)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Esther muache asikilize Taarifa ninayompa mimi hapa ili aweze kufuata maelekezo, ukimwongelesha atakuwa hanisikii, subiri mimi nimalize na wewe utazungumza.

Mheshimiwa Silinde kwa sababu Taarifa uliyokuwa unaizungumza umeanza kwa kusema Taarifa iliyotolewa na IMF imesema hivi. Taarifa aliyotoa Mheshimiwa Waziri inatoka huko huko IMF ikisema haijasema hivyo, kwa hiyo weka mchango wako vizuri ili taarifa zetu zikae sawasawa. Weka mchango wako vizuri Taarifa zetu zikae sawasawa.

MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Naibu Spika, naona hili jambo, labda kama nchi tuna-complicate sana kwa sababu ya facts ambacho kinaelezwa pale hawajakanusha kuhusu ukuaji wa uchumi wala hawaja- comment juu ya ile Taarifa na sisi hapa tunachojaribu kutaka ku-rescue hili Taifa hapa lilipo, ndicho ambacho tunachohitaji kukifanya. Sijui kama umenielewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ningeweza kumwambia sijapokea, lakini ni taarifa kutoka IMF, ni barua ameandikiwa. Ukisoma ile taarifa yote utaona Maofisa wote wa Serikali wako pale. Sasa mimi najaribu kueleza kwamba tofauti ya kwa nini hawaja-include miradi yetu na ni kwa nini wenzetu Wakenya, mradi wao wao walikopa bilioni 5.5 US dollar wakaingiza kwenye mradi wao, kilichosababisha uchumi wao kukua kwa asilimia 1.5 kwa sababu fedha ilitoka nje ya nchi ikaingia ndani ya Kenya. Sisi Tanzania ni vice versa, fedha inatoka Tanzania, inakwenda nje ya nchi, hiyo ndiyo tofauti yetu sisi na watu wengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, kikubwa hapa ambacho nataka nishauri, makosa yaliyofanyika awali kwenye kutoa fedha nyingi nje ya nchi, ndiyo nataka yasifanyike katika Mradi wa kutoka Makutupora kuelekea Mwanza kwa maana gani? Mradi wa Liganga na Mchuchuma gharama yake unahitaji kama dola bilioni tatu za Kimarekani, lakini ukishaukamilisha ule mradi kwenye mradi wa Liganga utapata chuma, utapata makaa ya mawe, utapata umeme na utachenjua madini mengine. Kwa hiyo tunapoanza kujenga mradi kutoka Dodoma kwenda Mwanza maana yake chuma kitakuwa cha ndani ya nchi. Kwa hiyo hela yetu hii ya ndani itatumika hapa hapa, hatutaendelea kununua tena machuma kutoka huko China. Kwa hiyo hapo hata IMF watakavyokuja watakuambia kwa sababu fedha yote inabaki kwenye mzunguko, maana yake nchi yetu uchumi wetu utakua

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa unaweza ukajiuliza swali dogo, kwa miaka minne mfululizo Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi mpaka sasa tumeiingizia shilingi trilioni 13.8. Mwaka huu wa fedha wanaomba shilingi trilioni 4.9, maana yake in total ni karibu shilingi trilioni 18.7, ndani ya miaka minne. Asilimia 40 ya fedha za miradi yote ya maendeleo ya Tanzania zipo Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sasa jiulize swali, tume- inject fedha inakwenda kwenye shilingi trilioni 18 lakini matokeo ya kiuchumi yanakwenda vise versa. Badala ya uchumi kutoka asilimia 7 kwenda 8, matokeo yake inatoka 7 inakwenda 4, inakwenda vise versa. That is the question tunahitaji kupata majibu yake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunawashauri Serikali kwamba tumieni fedha ambayo inaingia ndani ya uchumi kwa ajili ya kubadilisha maisha ya Watanzania, hicho ndicho ambacho tunakitaka. Changamoto ambayo ipo watu wetu hawa hawapendi kusikiliza ukweli. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, SGR bado inaendeleoa, itatoka Dar es Salaam, itakuja Morogoro, returning on investment ni nini? Hili ni swali ambalo tunapaswa kujiuliza. Je, itabeba tu watu peke yake mpaka Morogoro? Jibu ni kwamba kubeba watu haiwezi kurudisha gharama ya fedha ambayo tumeiweka mle ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunachotakiwa kufanya ni nini? Ndiyo maana nawashauri, sasa hivi wakati reli inakuja jengeni bandari kavu pale Morogoro. Ukishaweka bandari kavu pale Morogoro maana yake mizigo yote ambayo inakwenda nchi za SADC…

MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

MHE. DAVID E. SILINDE: Pamoja na inayokwenda Mikoa ya Kusini reli ile itayopita pale itaibeba. Kwa sababu mradi wote…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Silinde, kuna taarifa.

T A A R I F A

MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Naibu Spika, hamna taarifa hapa, hawataki kusikiliza ukweli tu. Sisi tunajaribu kuwashauri, shida mliyonayo Chama cha Mapinduzi mkishauriwa hamtaki, mkikosolewa hamtaki, mnataka nini? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ambacho najaribu kukieleza hapa ni kwamba kwa sasa mnatakiwa mjenge bandari ya nchi kavu Morogoro ambayo itasaidia kupeleka mizigo yote ya nchi za SADC, hicho ndicho kitu ambacho tunakihitaji kwa sasa. Nimesoma ile package ya kwanza ya mradi kutoka Dar es Salaam - Morogoro - Dodoma, nimeona tuna lengo la kuweka bandari ya nchi kavu hapa Dodoma, sasa kabla hatujaanza hapo, kwa hii awamu ya kwanza tuweke bandari kavu pale Morogoro ili tuhakikishe kwamba return on investment iweze kujibu mapema kabla ya jambo lingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye jambo linguine maana kengele ya kwanza imeshalia ni barabara. Tanzania barabara ndiyo chanzo kikubwa cha ajali kuliko hata uzembe wa madereva, namba moja hiyo. Kwa sababu barabara zetu ni ndogo lakini hazirekebishwi kwa wakati muafaka.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tuwe wakweli, Serikali haiwezi kufanya kila kitu kama ambavyo mmekuwa mkijiaminisha mbele za watu, haiwezekani! Kulikuwa na mradi hapa wa Dar-Moro Express Way, mradi ule ulitakiwa tu uendeshwe kwa mfumo wa PPP ama kuwapa private sector. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi niwaulize Serikali, unapomleta mtu akakujengea barabara, mkopo amekopa mwenyewe akajenga Dar es Salaam - Morogoro, barabara ile wanapita watu hata kwa kulipa fedha. Tunakwenda nchi za watu, tumekwenda South Africa, Ulaya na nchi zote, watu wanalipia gharama (road toll). Sasa mnasema kwa sababu ya reli, hatujengi Dar-Moro Express Way kwa sababu imekuwa taken by event, kwamba kwa sababu kuna reli basi hiyo barabara haiwezekani, yaani unaona ni thinking ya kurudi nyuma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mapendekezo yetu, ukijenga barabara kwa kutumia mfumo wa PPP, ukijenga madaraja kama Kigamboni, sifa inabaki kwa Serikali na haiendi kwa mtu mwingine tofauti. Tofauti yenu na sisi ninyi mnafikiri kwamba Serikali italeta maji, itajenga shule na kadhalika na ndiyo maana miaka yote, tangu mmekuwa madarakani kwa miaka 58 mambo yanakwenda polepole tofauti na kasi inayohitajika na mnataka pongezi kwa vitu ambavyo mnaviweza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nafikiri sasa watu wa TISS wafanye vetting ya watu wanaoweza kuongoza hii nchi ili kuhakikisha wanaipeleka mbele. Kuna watu wanafikiri kijamaa kuliko miradi inavyotaka kutekelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho ni ATCL. Hakuna mtu hata mmoja anayepinga ATCL lakini menejimenti lazima iwe huru, hiyo namba moja, wasiingiliwe wafanye kazi kibiashara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pili, kuna vitu ambavyo sisi tutaendelea kuwakosoa kila siku hapa ndani. Wewe Dreamliner imekuja tangu Julai, 2018, karibu mwaka mzima imepaki pale, tunakaa tunaiangalia pale, ile ni hasara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hii ni sawa na mtu umenunua coaster yako kutoka Japan umeiweka nyumbani kwako unaiangalia, haiingizi kitu chochote. Kwa nini usisemwe, kwamba wewe unafikiri kibiashara au unafikiriaje? Hayo ndiyo tunayolalamikia kila siku. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia watu wa Rwanda, pamoja na kwamba wana Shirika la Rwanda Air lakini menejimenti ya Rwanda wamechukua watu wa Ethiopia, ndiyo wanao-run lile shirika halafu watu wa chini kule ndiyo watu wa Rwanda. Kwa sababu watu wa Ehiopia ndiyo wana uwezo mkubwa wa kuendesha mambo haya. Sasa na ninyi msione aibu kwenda kumchukua mtu Ethiopia, Rwanda akaja kuwasaidia. Hata KQ sasa hivi, miongoni mwa mabadiliko yao wamefanya hivyo. Msifanye maamuzi mkafikiri kwamba kila kitu kinawezekana. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa nafasi hii. (Makofi)