Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Ezekiel Magolyo Maige

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Msalala

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. EZEKIEL M. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Kwanza naomba niipongeze sana Serikali yangu ya Awamu ya Tano kwa kazi kubwa sana inayofanyika ya ujenzi wa miundombinu mingi mbalimbali nchini na pengine tu kabla sijaenda mbali zaidi, nijaribu kugusia kidogo hii hoja iliyotolewa na mchangiaji mmoja aliyezungumzia kuhusu suala la mchango wa Sekta ya Ujenzi kwenye uchumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, utafiti unaonyesha kwamba katika miradi yote ya ujenzi, asilimia isiyozidi 30 ndiyo huwa mchango wa wakati wa mradi, asilimia 70 huwa inapatikana pale mradi unakuwa umekamilika na kuanza kutumika. Jana tulimsikia mzee wangu Mheshimiwa Ndassa hapa alizungumzia kwamba Mji wa Ngudu umedumaa kwa sababu hauna barabara. Ukienda sehemu zote ambazo barabara zimejengwa, hali ya maisha na shughuli za kiuchumi zinakwenda kasi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hivyo, tunavyozungumza kujenga reli ya kiwango cha standard gauge tunategemea reli hii ikikamilika ndiyo itakayoleta manufaa na itakayoonyesha sasa uchumi kukua kwa kasi zaidi kuliko wakati wa utekelezaji wa mradi wenyewe. Faida zinazokuwepo wakati wa ujenzi ni kidogo sana kwa wastani hazizidi asilimia 30.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niseme tu pamoja na kwamba Mheshimiwa Zitto namuheshimu sana lakini ukweli huu anaufahamu ni vizuri tukaliona hilo kwamba investment zinazofanyika leo zina multiply effect kubwa kwa baadaye hasa baada ya sekta tarajiwa kama kilimo na viwanda. Huwezi ukajenga kiwanda leo Kigoma cha cement ambayo huwezi ukaisafirisha kuipeleka kwenye soko Dar es salaam; ukishaweka reli ndiyo utawezesha kiwanda kujengwa kule. Leo hii muulize Dangote anavyohangaika kufikisha cement yake kwenye maeneo ambayo hayana miundombinu ya barabara. Kwa hiyo, miundombinu inachochea uchumi baada ya kuwa imekamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya ufafanuzi huo na pongezi hizo kwa Serikali, niendelee kuipongeza sana Serikali yangu kwa miradi hii mikubwa ambayo pia inafanyika katika Mkoa wetu wa Shinyanga. Kwa muda mrefu sana nimekuwa nikiomba barabara ya kutoka Kahama kwenda Geita ijengwe kwa kiwango cha lami, ninashukuru sana nimeona kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri aya ile ya 28, amesema taratibu za kupata wakandarasi ndizo zinaendelea na kwa bajeti hii ile aya ya 248 ametenga bilioni 5 kwa ajili ya kuanza ujenzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe sana Mheshimiwa, bahati nzuri Mheshimiwa Naibu Waziri Kwandikwa yupo na anafahamu barabara hii umuhimu wake kwamba mchakato wa kupata wakandarasi ambao sasa tunakwenda mwaka wa tatu toka 2016, 2017 na 2018 ukamilike na barabara ianze kujengwa. Ni barabara ya muhimu sana kiuchumi, inaunganisha migodi ya Bulyanhulu na Buzwagi; ni barabara yenye sifa katika zile barabara za kipaumbele kwa sababu inaunganisha Mkoa wa Shinyanga na Mkoa wa Geita. Vilevile ni barabara ambayo ipo kwenye ahadi zetu za kipaumbele. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais mwaka 2017 amefika, ameongea na wananchi wa Segese akawaahidi wananchi wa Bukoli kwamba barabara hii itaanza kujengwa kwenye kipindi hiki na hii ndiyo bajeti ya mwisho ya utekelezaji tunayofanya, bajeti ijayo tutakuja kuipitisha na kwenda kwenye uchaguzi. Ni muhimu sana hizi bilioni 5 tulizozisema na mchakato wa kupata wakandarasi ambao umeanza miaka mitatu sasa ukamilike ili ujenzi uweze kuanza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna barabara nyingine ya kutoka Kahama kwenda Nyang’wale hadi Busisi. Barabara hii haijaguswa kabisa kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri, tuliahidiwa kwenye bajeti iliyopita kwamba ingeanza kufanyiwa upembuzi yakinifu, sasa hivi hata kutajwa haijatajwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia hata ile barabara ya kutoka Kahama – Solwa – Managwa ambayo pia inaunganisha Mkoa wa Shinyanga na Mkoa wa Mwanza, ilikuwemo kwenye upembuzi yakinifu na ilishakamilika lakini kwenye orodha ya barabara ambazo zimetajwa kwamba zimekamilika kufanyiwa upembuzi zinatafutiwa fedha ili zianze kujengwa, haijatajwa. Nilikuwa naomba sana rekodi zikae sawa, muda wote tuwe tunataja tumefika hatua gani ili kesho na keshokutwa tusijetukarudi tena kuanza kuzungumza kwamba tunaomba ifanyiwe hatua fulani wakati ilishakamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe la mwisho, Mheshimiwa Waziri Mpango yupo hapa, nimeona kwenye taarifa ya Waziri kuna ujenzi wa vituo Dakawa na Muhalala; mkandarasi amesimama kwa sababu ya suala la VAT. Nilikuwa naomba suala la VAT ambalo linahusu kuwezesha miradi ya ujenzi kukamilika kwa wakati, mzungumze mlimalize; Mheshimiwa Rais aliagiza akiwa Mwanza wakati ule wa uzinduzi wa ujenzi wa vivuko kule, ninaomba mmalize mkandarasi arudi site, kuna hasara tunapata kwa kutokumaliza mazungumzo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimegongewa kengele ya pili, nisingependa kuchukua zaidi muda. Nakushukuru sana kwa nafasi na naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)