Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Hasna Sudi Katunda Mwilima

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kigoma Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. HASNA S. K. MWILIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru nianze kwa kumpongeza Waziri, pamoja na Manaibu wake Mawaziri na Watendaji wote wa Wizara hii muhimu sana katika majimbo yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze kuzungumzia madaraja, jimbo langu lina eneo moja korofi sana tunaita kwenye kivuko cha Malagarasi kwenye ukurasa wa 167 nimeona mmeelezea kujenga daraja la Mto Malagarasi sasa nilikuwa nataka ufafanuzi Mheshimiwa Waziri atakapokuja, hapa nione je, hili daraja la Mto Malagarasi mnalenga daraja gani, Kwenye ukurasa wa 167? Ndiyo daraja la Ilagala kwa sababu linapita pale kwenye Mto Malagarasi au mnalenga daraja lipi? Kwa sababu nilipomwuliza Mheshimiwa Waziri aliniambia niangalie ukurasa wa 340. Ukurasa wa 340 mnazungumzia kujenga daraja kwenye Mto Rwegere. Mto Rwegere upo kwenye Kijiji cha Mgambazi, unakwenda mpaka kwenye Kijiji cha Rukoma.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naona hapa kuna contradiction ambayo ningependa Mheshimiwa Waziri na Naibu Mawaziri mliangalie vizuri, kama mtakuwa mnalenga Ilagala, basi nadhani ni hili daraja la Mto Malagarasi. Kwa hiyo, naomba kwa faida ya wananchi wa ukanda huo, basi Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anahitimisha ataweza kunifafanulia vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili nizungumzie suala la gati. Tunazo gati mbili kubwa zinazojengwa; gati ya Sibwesa na gati ya Mgambo. Naomba tu gati ile ya Sibwesa sasa ikamilike kwa sababu imekuwa ni muda mrefu sana. Gati ile mara kwenye kitabu mmendika ukamilishaji asilimia 91. Bajeti ya mwaka 2018 mlisema ukamilishaji asilimia 90. Sasa kila mwaka mnapokuja hapa mnaongeza asilimia fulani ya ukamilishaji. Naomba mnisaidie kukamilisha bandari ile. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia nizungumzie suala la SGR. Nimeangalia kwenye ukurasa wa 212, ule mtandao wa SGR mnazungumzia tu Dar es Salaam mpaka Tabora, Tabora – Isaka, Isaka – Mwanza. Tumekuwa tunalia hapa Bungeni mbona hamwoneshi ule mtandao wa kutoka Tabora mpaka Kigoma? Hata kama itachukua miaka mitatu, miaka minne kukamilika lakini tunaomba kwa sababu mpango unatambua huu mtandao wa kwenda Tabora, basi tunaomba Mheshimiwa Waziri aweze kuzingatia kuonyesha na ule mtandao wa kutoka Tabora kwenda Kigoma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie barabara ukurasa wa 164. Ninayo barabara yangu ya Uvinza mpaka Malagarasi kilometa 51.1 na kilometa 36 kutoka Chagu mpaka Kazilangwa. Ninajua kwamba kwenye Mfuko ule wa Maendeleo ya Abudhabi Mheshimiwa Waziri wa Fedha alishatia saini kupokea pesa takribani miaka miwili iliyopita. Sasa ninachoomba ni utekelezaji. Ni lini Serikali itatangaza tenda kwa ajili ya Mkandarasi kuanza ujenzi wa barabara hiyo ya kutoka Uvinza - Malagarasi na hicho kipande cha Chagu mpaka Kazilambwa? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, tunayo hii barabara yetu hii ya kutoka Simbo mpaka Kalya ina kilometa 250. Kila mwaka mnaitengea fedha shilingi bilioni 1.9, shilingi bilioni 1.8 lakini tusipoteze hizi fedha za Serikali, tunatenga pesa nyingi kwa ajili ya kujenga barabara kiwango cha udongo na changarawe, sasa kwa nini tusiende kwenye kiwango cha lami? Hii barabara tangu mmeanza kuijenga ni takribani miaka zaidi ya 20. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri aangalie namna ya kupandisha hadhi barabara hii iweze basi kujengwa kwa kiwango cha lami. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie bandari ya Kigoma. Asubuhi nilimsikia Mheshimiwa Zitto anaongelea bandari. Bandari hii ni kwa faida ya Wabunge wote na wananchi wote ndani ya Mkoa wa Kigoma. Leo ninavyoongea, tunao Mkutano mkubwa pale Kigoma ambao ulikuwa Mheshimiwa Makamu wa Rais awe Mgeni Rasmi, lakini amemtuma Mheshimiwa Kandege kumwakilisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna wafanyabiashara kutoka Zambia, tuna wafanyabiashara kutoka Burundi, tuna wafanyabiashara kutoka Congo na Rwanda; wameanzia jana, wako kwenye mkutano mkubwa wa wafanyabiashara wanaozunguka Ziwa Tanganyika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naiomba Serikali waone umuhimu wa bandari ya Kigoma. Bandari hii ina umuhimu sana. Tunafanya biashara na watu wa Zambia, Congo na Burundi, wanachukua mizigo yao Dar es Salaam wanaipeleka Congo, Zambia na Burundi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa bandari hii, kwa sababu Benki ya Afrika iko tayari kutusaidia fedha, tunaomba Serikali iangalie kwa jicho la huruma ili basi bandari hii na itaiingizia fedha Serikali, ni chanzo cha mapato, yaani...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Hasna muda wako umekwisha.

MHE. HASNA S.K. MWILIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)