Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Omari Mohamed Kigua

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilindi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya jioni ya leo nami niweze kusema machache juu ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Manaibu Waziri wote wawili kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijaanza kuchangia nataka nitoe somo dogo tu, dhana ya uwekezaji katika miradi mikubwa. Serikali imedhamiria kujenga SGR. Huu ni mradi mkubwa sana. Sasa wapo waliozungumza kwamba wanatarajia mafanikio ya muda mfupi. Huu ni mradi mkubwa sana ambao return yake itapatikana baada ya miaka 50 ijayo. Ku-recoup costs zake au payback period ni zaidi ya miaka 20. Kwa hiyo, usitarajie kwamba faida utaipata kwa muda mfupi, lakini lazima tuangalie multiplier effect ya mradi huu. Huwezi ukajenga SGR kwa sababu ya kubeba abiria peke yake, hapana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi Tanzania tunapakana na nchi ambazo hazina bahari; Uganda, Burundi na Rwanda. Tunatarajia SGR ndiyo ambayo itakayoweza kupeleka mizigo huko. Kwa hiyo, lazima tutarajie mafaniko makubwa sana kutokana na mradi huu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuna mtu amesema hapa kwamba suala la mradi huu halina kitu kinaitwa local context, siyo kweli hata kidogo. Naomba nithibitishe kwamba SGR ina mafanikio makubwa sana. Nitataja machache tu eneo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, SGR itakapokamilika, tunatarajia viwanda vyetu vya cement vya ndani vitaweza kuzalisha takribani mifuko milioni 110.2. Vilevile tunatarajia viwanda vyetu vya ndani, vitaweza kuzalisha nondo tani 115,000. Kama hiyo haitoshi, viwanda vya kokoto vitatoa mita milioni 2.7. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho ni suala la ajira. Ajira mpaka sasa hivi, kutokana na SGR ni takribani watu 9,639 wamepata ajira. Hii ni dhana ya local context kwenye SGR. Kwa hiyo, mtu asipotoshe kusema kwamba SGR katika suala la local context haijazingatiwa. Siyo kweli hata kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya utangulizi huo, sasa naomba nizungumzie suala lingine la ATCL. Umuhimu ni mkubwa sana sana. Narudia kusema kwamba faida ya ATCL au katika mambo ya ndege huwezi ukaiona moja kwa moja na wala usitegemee kwamba ATCL irekodi profit katika muda mfupi. Hata Mashirika yale kwa mfano, Rwanda Airlines, Ethiopian Airlines, hawajawahi kurekodi profit hata siku moja, lakini kuna suala la multiplier effect, hili lazima lizingatiwe na umuhimu wa jambo hili ni mkubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hapo sasa naomba nirudi kwenye barabara ambayo inaunganisha Mikoa minne. Barabara hii ni muhimu sana, nayo ni barabara ambayo ipo katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Barabara hii ina kilometa 460 ya kuanzia Handeni, Kibirashi, Kibaya na Singida. (Makofi)

T A A R I F A

MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, siipokei kwa sababu hili ni suala la kitaalamu zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, unapofanya investment…

MHE. ALLY SALEH ALLY: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, unapofanya investment maana yake, return yake hutarajii kupata kwa muda mfupi na maana yake SGR hii faida yake itakuwa kwetu sisi na vizazi vijavyo.

T A A R I F A

MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, siipokei kwa sababu hajataja source ya taarifa ni wapi.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

WABUNGE FULANI: Endelea.

MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niendelee.

MHE. ALLY SALEH ALLY: Reuters, Reuters Financial. (Kicheko)

MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie barabara hii ambayo nimesema ni barabara ya Handeni – Kiberashi - Kibaya na Singida. Barabara hii ni muhimu sana. Kama katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri alivyosema kwamba barabara hii ndiyo ambapo bomba la mafuta litapita, nami nataka niseme kwamba pamoja na kwamba bomba la mafuta kutoka Uganda kwenda Tanga litapita katika eneo hili, pia barabara hii ina umuhimu mwingine ambapo watu wa mikoa hii minne niliyoitaja wanahitaji barabara hii sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona katika hotuba yake Mheshimiwa Waziri ametenga kiasi cha shilingi 1,450,000,000/=, namshukuru sana na ninampongeza katika hilo. Namwomba Mheshimiwa Waziri, barabara hii ni muhimu sana, sana, sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kwamba Serikali ya Tanzania imetenga kiasi hicho nilichokitaja, lakini naomba tuangalie namna ambavyo inaweza kujengwa kwa kiwango cha lami, kwa sababu eneo hili ambalo barabara hii inapita, ina uzalishaji mkubwa sana, sana, sana; na ukizingatia kwamba kuna matarajio ya kutengeneza Bandari ya Tanga, kwa hiyo, ni matumaini yangu kwamba barabara hii ikitengenezwa kwa kiwango cha lami, basi mizigo yote ambayo inatoka Tanga kwenda Magharibi huko itapita katika barabara hii. Nina imani kwamba Mheshimiwa Waziri atazingatia katika hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine naomba nizungumzie huku minara. Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwamba Wilaya ya Kilindi ni miongoni mwa maeneo ambayo yamepata minara mingi sana, lakini lipo eneo moja ambalo linapakana na Wilaya ya Simanjiro, Kata ya Saunye, haijapata minara. Naomba sana Mheshimiwa Waziri kupitia Mfuko huu wa Mawasiliano wahakikishe kwamba Kata hiyo inapata mawasiliano kwa sababu ni eneo muhimu sana, ni eneo ambalo lina mbuga ya utalii, lakini maeneo haya hayasikiki kabisa. Ni matumaini yangu kwamba Serikali itasikia tuweze kupata mawasiliano katika eneo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema maneno hayo machache, nakushukuru sana. Naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)