Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara

Hon. Lucy Thomas Mayenga

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara

MHE. LUCY T. MAYENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi hii angalau nami niweze kuchangia kwenye Wizara hii, ingawa bahati mbaya dakika hizi tano ni chache sana, lakini sina budi kutumia muda huo huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilisimama hapa mara ya mwisho wakati nikizungumza kwenye Wizara hii ya Viwanda na Biashara nikatoa wazo kwamba Mheshimiwa Rais na Serikali kwa ujumla iweze kuihamisha TIC kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara na kuihamishia aidha kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu au Ofisi ya Rais. Ninaomba kwa heshima na taadhima nithibitishe kwamba, Mheshimiwa Rais ni msikivu, ninafahamu kwamba vyombo vyake vimesikia na wamepima wameona kwamba, wazo hilo lililkuwa ni zuri. Ninajua kwamba vyombo vyake vitakuwa vilishafanyia kazi kabla hata sijazungumza na ndiyo maana TIC imehamishwa. Ninampongeza sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo TIC imehamishwa, bado Wizara inatakiwa sasa ifanye haraka na kwa mkakati maalum kuweza kuleta Sheria ya TIC mpya hapa Bungeni. Sheria Namba 26 ya Mwaka 1997 imepitwa na wakati. Yaani miaka imekuwa ni mingi mno kiasi kwamba mabadiliko yanayoendelea sasa hivi duniani hayaendani na hii sheria. Hata hivyo, sheria hiyo ikiwepo itasaidia kurekebisha vitu vingi sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna vitu vingi ambavyo vimezungumzwa na Wabunge kwenye Bunge hili kwamba kuna masuala ya tozo, masuala sijui ya taasisi mbalimbali ambazo zinashughulikia biashara pamoja na uwekezaji. Sheria hii endapo kama ikiletwa, itaweza kurekebisha mambo haya; mambo ya OSHA watu wanalalamika, mambo ya sijui NEMC na kadhalika, kwa hiyo, mambo mengi yataweza kurekebishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile uratibu wa masuala mazima ya uwekezaji angalau yataweza kufanywa na chombo kimoja, maana sasa hivi ni vile kila mtu mkubwa. Kila taasisi inajiona kwamba kubwa. Kila mtu, leo anakuja anasimama anasema hivi, mwingine kesho anakuja anasimama anasema hivi. Kwa hiyo, sheria hii ikiletwa, itaweza kusaidia ili mambo yakae sawasawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile mara ya mwisho nilizungumzia kuhusu habari ya vibali vya kazi pamoja na ukaazi. Mheshimiwa Waziri, yapo masuala mengine hayatakiwi labda mpaka mtu mkae mtafute mwezi mzima muweze kuyafanyia kazi. Hili suala la vibali vya kazi halijakaa sawa sawa katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, haiwezekani sheria hiyo hiyo ya mwaka 1997 inasema kwamba, mwekezaji akija, kwenye sheria imeandikwa kwamba anaruhusiwa kupewa watu watano. Kwa hiyo, huku sheria inasema aruhusiwe kupewa watu watano, lakini akishafika wale watu watano hapewi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hili suala tunaonekana hatuwezi kuaminika. Huu ni uwekezaji, lazima ifike wakati tuone kwamba sisi kama nchi ndiyo tuna shida na wawekezaji na siyo kwamba wawekezaji wana shida na sisi. Tukiwa na mtazamo wa kusema kwamba wawekezaji wana shida na sisi, hatuwezi kufika. Nami nilikuwa naomba Wizara ya Uwekezaji, Wizara ya Viwanda na Biashara inabidi mkimbie maana sasa hivi naona bado mnatembea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nizungumzie kuhusu suala zima la wafanyabiashara. Baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa wakisimama hapa wanazungumzia kwa mfano, kuna hoja ambayo inasemwa na wafanyabiashara sitaki kusema ni wapi; kwamba, kuna mafuta yamekamatwa, yamewekwa huko, meli zimekaa miezi saba. Kama unaulizwa document, TRA kosa lake ni nini?

Mheshimiwa Naibu Spika, tusije tukaja tukakaa mara nyingi tukawa tunaweka mzigo mkubwa sana kwa TRA. Hakuna mfanyabiashara na wala hakuna mkusanya kodi ambaye anapendwa, lazima na sisi tuweze kujiangalia tumekosea wapi? Kama unaambiwa lete kibali original, hamna mfanyabiashara ambaye unaleta mzigo unakosa kibali original, haipo.

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, naomba kumpongeza sana sana Mheshimiwa Rais wangu. Naomba kumwambia maneno yafuatayo: Miradi yoyote ile ambayo inaletwa katika nchi yetu kama haina maslahi au haina tija, naomba kusema kwamba waizuie huko huko wala hata isiendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivyo kwa sababu gani? Tuna imani kubwa, tunaomuunga mkono katika nchi hii na katika Bunge hili tuko wengi. Kwa hiyo, miradi kama inaonekana kwamba ina hitilafu, kwa msimamo aliouonesha Rais wetu; kwanza cha kwanza kabisa hakuna mtu mwenye information katika hii nchi kama Rais wetu. Rais ndio mtu wa kwanza mwenye information za uhakika kuliko mtu mwingine yeyote. Kwa hiyo, akikaa akasema kwamba suala hili haliko sawa sawa, mjue kwamba haliko sawa sawa. Sasa tukikaa tena hapa mtu akasimama akasema unajua suala hili sijui limekaa hivi, mwisho tutakuja kuvunjiana heshima. (Makofi)