Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

Hon. Joseph Kasheku Musukuma

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuuomba mhimili wa Bunge kwamba sisi Wabunge tunapoapishwa kuwa Wabunge ni vizuri sana kama mhimili uone umuhimu wa kuchukua ile miezi mitatu ya mwanzo kutupeleka kwenye Chuo cha Jeshi cha Kunduchi cha NDC ili tuweze kujifunza kuzungumza maneno yanayoilinda taifa letu. Chuo hiki ni kizuri na mimi nina imana kama Bunge litakubaliana na mimi kwamba Wabunge tukapate miezi mitatu ya kufundishwa pale, hii migongano ya maneno ya hovyo hovyo yanayotokea humu ndani haitakaa itokee. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mzuri ni wa leo tu, asubuhi Mheshimiwa Spika ametueleza kuhusiana na Mbunge kijana Mheshimiwa Masele anayetuwakilisha kwenye Bunge la PAP, kijana huyu pengine angekuwa amefundwa pale Kunduchi haya yote yaliyotokea kule PAP yasingetokea. Kwa hiyo, ni muhimu sana sisi kama Bunge tukubaliane twende tukafundishwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nitazungumzia kidogo tu kuhusu SUMA JKT. Sisi Wabunge tunaotoka kwenye maeneo ya migodi, nilikuwa naishauri Serikali maeneo haya ya migodi na hasa hii migodi mikubwa ni vizuri Serikali malindo yale ambayo yanalindwa na vyombo ulinzi vya nje wangepewa watu wa SUMA JKT. Kwa mfano, kwenye migodi mikubwa kama Geita wanalindwa na Kampuni inaitwa G4S, mlinzi mmoja analipwa karibu dola 800 yule mzungu mwenye kampuni na retired officer kutoka huko South Africa. Lakini vijana wetu wanalipwa shilingi 200,000/300,000 na mimi nimeona SUMA JKT wamefanya vizuri mpaka wametoa na gawio kwenye Serikali. Hizi fedha wangelipwa SUMA JKT wangefanya vizuri zaidi hapa wangetupa gawio kubwa zaidi kwa Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaona kule migodini kwa kuwa hawa watu waliopewa hizo kampuni za ulinzi ni wazungu wa South Africa, wanawa-train vijana wetu vibaya na nilishazungumza hata humu ndani, ukienda kule Geita kwenye migodi ile kama GGM na migodi mingine ya Kahama, wale walinzi wa kule wakimkamata kijana aliyeenda kule tu hata kuokota mawe wanawapiga, wanawanyanyasa na hata wanawakamata wanawake wanaenda kuwalalisha na mbwa. Sasa ni vizuri walinzi wale wangepewa walinzi wetu ambao wamefundishwa na wana maadili mazuri ya Kitanzania, nadhani ingekuwa ni vizuri zaidi na Jeshi letu lingeweza kupata fedha nyingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi niombe tu, kiukweli amezungumza kaka yangu pale kuhusuana na kauli zinazotolewa na wenzetu. Mimi niombe tu kwamba kiukweli maadui huwezi kujua wako ndani ama wako nje. Tukianza kulisema Jeshi kwa ubaya kwamba wakae kimya, mambo yakiharibika mimi natoa mfano tu siku moja humu ndani uliwaka moto, kila mtu alikimbia humu. Hebu lijaribu liripuke bomu humu ndani tuone mtu jasiri wa kuweza kukaa humu ndani. Kwa hiyo, mimi niombe tu sisi kama Wabunge kwa Jeshi letu hili la mfano linasifika kimataifa, Wizara kama hii siku inayoletwa humu ndani, tusilifananishe Jeshi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama. Ni watu ambao kiukweli muda wao mwingi wanafikiria kutulinda sisi tukae salama na nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa binafsi yangu nikuombe na Wabunge wenzangu, Jeshi linafanya kazi nzuri, ni watu wanaotakiwa kupewa moyo na mimi ningeomba kama tungeweza kupata muda kidogo tukapelekwa Jeshini kama wiki mbili, ukaona ule msoto ulioko kule halafu bajeti inaletwa humu watu wanaanza kuongea mambo ya hovyo hovyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwapongeze sana ndugu zangu wanajeshi mnafanya kazi nzuri na sisi kama Wabunge tunawaombea endeleeni kuilinda nchi yetu, haya maneno madogo madogo... (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante, unga mkono hoja.

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)