Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

Hon. Hamoud Abuu Jumaa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibaha Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

MHE. HAMOUD A. JUMAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote napenda kuchukua fursa hi kumshukuru Mungu mwingi wa rehema kwa kuniwezesha kufika mahali hapa na mimi nichangie hotuba hii ya bajeti ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ya mwaka 2019/2020. Aidha nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri na watendaji wa Wizara kwa kuandaa hotuba nzuri, hotuba hii inakwenda kutekeleza ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi kama ilivyoainishwa hasa katika masuala mazima ya ulinzi wa Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nianze kwa kuvipongeza vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kwa kufanya kazi kubwa katika kuhakikisha hali ya amani, usalama na utulivu inaimarika. Katika mwaka 2018/2019 Serikali imelitumia Jeshi la Wananchi wa Tanzania kusaidia mamlaka za kiraia katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali kama vile uokoaji wa watu na mali zao pamoja na ujenzi wa Mji wa Serikali katika eneo la Mtumba, Dodoma, hatua nzuri sana na ya kupongezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nalipongeza Jeshi la Wananchi wa Tanzania kwa kuendelea kushiriki kwenye misheni za kulinda amani chini ya mwamvuli wa Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa. Misheni hizo ni MINUSCA huko Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR); MONUSCO Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC); UNAMID nchini Sudan; UNFIL nchini Lebanon; UNISFA huko Abyei na UNMISS nchini Sudan Kusini. Ushiriki wa Jeshi letu pamoja na vyombo vingine vya usalama katika misheni hizo za amani umeendelea kuvipatia uzoefu, kuongeza maarifa na mbinu mbalimbali za kijeshi na kiintelijensia. Aidha, vyombo vyetu vimeendelea kujifunza matumizi ya vifaa vya kisasa na kuanzisha au kuimarisha mahusiano ya kijeshi na nchi nyingine zinazoshiriki kwenye misheni hizo. Jambo zuri ni katika kuimarisha usalama wa raia na mali zao, Serikali imeendelea kudhibiti hali ya ulinzi na usalama nchini kwa kuboresha mazingira ya kuishi askari na kufanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwa kuendelea kufanya juhudi kubwa kwa Jeshi letu, katika mwaka 2019/2020 Serikali imeendelea kuimarisha hali ya ulinzi na usalama, kuendelea kutoa fursa za mafunzo kwa vyombo vya ulinzi na usalama, kuvipatia vifaa na zana za kisasa na kuendelea kushirikiana na Jumuiya ya Kimataifa katika kupambana na makosa yanayovuka mipaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.