Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

Hon. Lucia Ursula Michael Mlowe

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika hoja iliyopo mbele yetu. Awali ya yote niunge mkono hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie mambo yafuatayo. Jambo la kwanza ni bajeti isiyotosheleza. Kumekuwa na tatizo kubwa la upelekaji wa bajeti za maendeleo karibu kila mwaka, maeneo mengine imekuwa inapelekwa pungufu au haipelekwi kabisa. Kwa mfano, Wizara ya Kilimo katika mwaka wa fedha 2016/2017 pesa za maendeleo kiasi cha shilingi bilioni 100.25, zilikuwa zimetengwa lakini hadi kufikia mwaka 2017 zilizotolewa zilikuwa shilingi bilioni 2.2 tu sawa na asilimia 2.2.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tumeona katika mwaka 2017/2018, Wizara hii iliidhinishiwa na Bunge pesa za maendeleo shilingi bilioni 100.2 lakini hadi kufikia mwezi Machi ni shilingi bilioni 16.5 tu zilikuwa zimetolewa sawa na asilimia
11. Tukija katika mwaka wa fedha 2018/2019 fedha iliyotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo katika sekta ya kilimo ilikuwa shilingi bilioni 98.119 lakini fedha iliyotolewa ilikuwa ni shilingi bilioni 41 sawa na asilimia 42.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tumeona huu mtiririko wote wa bajeti ya miradi ya maendeleo kwa jinsi ambavyo imekuwa ikisuasua na kwamba haipelekwi kwa wakati au inapelekwa pungufu hata pungufu ya asilimia 50. Napenda kuishauri Serikali kutokana na tatizo hilo la kutoweza kupeleka bajeti za kutosha kwenye miradi ya maendeleo au kutopeleka kabisa ni vema basi Serikali ikaona namna gani tunawekeza au tunaweka mazingira wezeshi au mazuri kwa wawekezaji ili waweze kutusaidia katika miradi mbalimbali ya maendeleo kama maji, miundombinu na miradi mingine. Hii ingeisaidia sana Serikali angalau kutokuwa na mapengo makubwa kama ilivyo sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba niongelee suala la miradi ya maji. Miradi ya maji imekuwa ni tatizo nchi nzima katika utekelezaji wake. Kwanza miradi mingi imekuwa ikiripotiwa imekamilika lakini kwa uhalisia haifanyi kazi na wakandarasi wamekuwa tatizo. Naishauri Serikali na Wizara ya Fedha tuone namna gani pesa zinazokuwa zimetengwa zipelekwe kwa wakandarasi kwa wakati unaotakiwa lakini wakati huo huo tuwapime hawa wakandarasi maana wakandarasi wengine siyo waadilifu kabisa. Inapogundulika kwamba hawa wakandarasi siyo waadilifu basi watolewe mara moja wasilelewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia suala la maji limekuwa ni tatizo hata maeneo yale ambayo yana vyanzo vya maji vingi tu vya kutosha. Naiomba Serikali tuone namna ya kuwapata wataalamu wanaokuwa wabunifu katika miradi mbalimbali ya maji. Nitoe mfano tu katika Mkoa wa Njombe, ule mji umezungukwa na maji lakini pale Njombe Mjini hakuna maji na tuna wataalamu, kwa nini hao wataalamu wasiwe na ubunifu na kutumia njia nyingine kuhakikisha maji yanaingia pale mjini ukiacha vijijini au ukiacha maeneo mengine ambayo yana ukame. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia suala la maji katika nchi yetu tumeona kipindi cha mvua kunakuwa kuna maji mengi sana na mafuriko. Hivi hatuwezi kupata wataalamu ambao wanaweza wakatuelekeza namna kuvuna haya maji na kuweza kuyatumia wakati wa ukame? Naishauri sana Serikali tuone namna gani tunaweza kuelekeza nguvu zetu kwenye vitu tulivyonavyo kwa sababu haya maji ya mvua tunakuwa nayo na hata sasa hivi kuna maeneo mvua zinanyesha sana lakini haya maji hayavunwi mwisho wa siku maeneo haya yanakujakuwa makame lakini wakati huo huo kulikuwa kuna mvua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni watumishi. Suala la watumishi kwa kweli ni changamoto kubwa. Naiomba Serikali ione namna gani angalau kipindi kilichobakia maana toka tumeingia mwaka 2015 hadi sasa watumishi hawajapandishiwa mishahara angalau hata ya kudanganyishia tu. Watumishi wako katika hali ngumu sana. Nikitoa mfano wa walimu hata nyumba wanazokaa zinatia huruma. Kwa mfano, sasa hivi kuna shule ambazo zinakarabatiwa vizuri sana lakini nyumba za walimu hakuna. Sasa hata kama shule zimekarabatiwa vizuri walimu wanaweza kwenda kufundisha lakini kama wao hawana nyumba nzuri bado haitasaidia. Niombe Wizara ya Fedha tuone namna gani tunawasaidia hawa watumishi hasa walimu kuwajengea nyumba kama tulivokarabati shule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni madini. Naomba kuongelea suala la madini Mchuchuma na Liganga umekuwa wimbo wa taifa. Tumekuwa tukiongea juu ya Liganga na Mchuchuma, tulifikiri kufikia kipindi hiki tungekuwa tayari tumeshaanza kufaidika na mradi ule. Ule mradi ungekuwa na faida kubwa sana kwa Taifa letu, haya mambo tunayohangaika nayo sasa hivi ya pesa pengine ingekuwa ni msaada mkubwa sana mradi ule. Naiomba Serikali kwa kweli ichukue hatua ya haraka kutekeleza ule mradi wa Liganga na Mchuchuma kusudi uweze kusaidia kuinua uchumi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni barabara. Maeneo mengi barabara zimetengenezwa lakini mengine kwa kweli ni tatizo, barabara zimeanza kutengenezwa muda mrefu lakini hadi sasa hazijaisha. Mfano katika Mkoa wa Njombe barabara inayounganisha Ludewa na Njombe Mjini maana ya Itoni –Ludewa, barabara ile kwa kweli ni tatizo, kama ingefanikiwa kwisha ingekuwa msaada mkubwa sana. Hadi sasa hivi ni asilimia 30 tu na tunaambiwa kwamba mpaka mwakani inatakiwa iwe imekamilika. Sasa najiuliza kama mpaka sasa hivi imetekelezeka asilimia 30, je, mwakani inaweza kumalizika kwa hizo asilimia 70 zilizobaki? Niiombe Serikali mtusaidie fedha kwa ajili ya kukamilishia ile barabara. Ahsante. (Makofi)