Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

Hon. Eng. Gerson Hosea Lwenge

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

MHE. ENG. GERSON H. LWENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwanza kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Mpango kwa hotuba yake nzuri na kwa kuwasilisha Mpango mzuri ambao ni sehemu wa miaka mitano ambao tulipitisha Waheshimiwa Wabunge, kwa hiyo nampongeza sana. Pia naomba nipongeze sana Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri ambayo kila moja anaona. Kwabhiyo hata kama yupo anayebeza, anabeza kwa sababu zake, lakini vitu vinavyofanyika vinaonekana wazi wazi. Kwa hiyo niwapongezeni sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu nitajikita zaidi kwenye suala la miundombinu. Katika Mpango ambao umewasilishwa, vipaumbele vimewekwa lakini katika hivi vipaumbele kuna eneo la ujenzi wa barabara za lami na nchi nzima tumeona barabara za lami zinajengwa, barabara za mkoa na barabara kuu zinazounganisha kati ya mkoa na mkoa. Naomba sana kwamba ili kusudi barabara hizi ziweze kudumu ni lazima tuweke mkakati mzuri wa matengenezo yake, tuongeze bajeti ya matengenezo ya barabara hizi ili isiwe barabara inajengwa baada ya miaka miwili inafumuliwa tena inajengwa nyingine. Ili tuweze kufikia maeneo yote ya nch, tuwe na mkakati mzuri wa matengenezo. Kwa hiyo, naomba sana Serikali iongeze fedha kwenye fuel levy kwa ajili ya kupeleka Wakala wa TANROADS na TARURA ili barabara zetu ziweze kujengwa. Tumeanzisha TARURA tukiamini kwamba TANROADS ilifanya kazi nzuri, lakini ilifanya kazi nzuri kwa sababu tuliweka fedha ya kutosha ya matengenezo, kwa hiyo tuweke nguvu sana kwenye matengenezo ya barabara zetu hizi ili ziwe sustained.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia naomba Mkoa wetu wa Njombe ukumbukwe kwenye barabara kuu ambazo ni muhimu ambazo hazijawekwa kujengwa kwa lami, kwa mfano, kwa barabara inayotoka Njombe Makete ifike mpaka Mbeya na barabara kutoka pale Ramadhani ifike mpaka Lyai iunganishe na barabara kuu ya Tazam highway.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba sana katika mpango huu tumeona kwamba kuna usambazaji wa umeme vijijini na kazi nzuri sana inafanyika. Mwaka jana nimechangia, nilisema katika usambazaji wa umeme maeneo mengi ambayo hata yameshajengewa miundombinu yamekuwa siyo sustained kwa sababu kwa muda mfupi unakuta nguzo zimeanguka au transform zimeungua, lakini sababu kubwa kwamba hatuweki bajeti kubwa ya matengeneo. Kwa hiyo naomba sana tuweke bajeti kubwa ya matengenezo katika miundombinu ya umeme ili kwamba hivi vijiji vyote zaidi ya 8,000 vimepata umeme, basi tufurahie kwamba tumeshapata maendeleo unajua mambo ya miundombinu ni kama mishipa ya damu ndiyo uhai wa mwili wa mwanadamu, basi miundombinu hiyo tuliyoijenga kwenye Taifa letu ni lazima iwe imewezeshwa sana hasa kwenye eneo hili la matengenezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo nataka nichangie ni suala la Mradi wa Liganga na Mchuchuma. Mwaka jana pia wengi wamechangia, mradi huu tumeuzungumza miaka mingi toka mwaka wa kwanza wa Mpango huu tumezungumza Mradi wa Liganga na Mchuchuma lakini mpaka leo hakuoneshi progress naamini katika hii sehemu ya mwisho ya mpango huu tutaweka nguvu kubwa, kama ni mradi wa kielelezo, kama ni mradi wa kipaumbele tuone utekelezaji wake tusiishie kusikia bado hatujalipwa hata fidia, sasa huu mradi kama kweli tumeamua kuujenga tuweke nguvu. Taifa lolote haliwezi kuendelea kama hakuna chuma, chuma ndiyo malighafi mama ya viwanda na sisi ndiyo tunasema tunajenga uchumi wa viwanda, kwa hiyo lazima tuweke nguvu katika kutekeleza Mradi huu wa Liganga na mchuchuma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo nataka nilizungumzie, ni sekta ya afya. Ni kweli Rais wetu ameamua kwa nguvu kubwa kujenga vituo vya afya 352 na hospitali za wilaya 69, ni jambo jema mimi nampongeza sana. Naamini kabisa Taifa lolote lazima na watu wenye afya uwe na mpango mzuri kwa ajili ya kuhakikisha Watanzania wanapata tiba iliyoboreka, kwa hiyo naomba sana awamu hii katika Mpango huu pia tuweke nguvu kujenga vituo vingi zaidi. Wananchi wetu katika maeneo mengi tuliwahamasisha, wamejenga zahanati kila kijiji na maeneo mengi kila kata wamejenga vituo vya afya, lakini wamefika mahali wamekwama, yale maboma yamebaki mpaka leo miaka mitano, miaka sita, basi katika mpango huu naomba sana Serikali iangalie namna ya kukamilisha hata angalau hizo zahanati wananchi wamechangia waendelee kuwa na imani na Serikali ili angalau kila kijiji wawe wanaweza kupata huduma ya msingi katika hili suala la afya. Pia huu mpango wa bima ya afya kwa wote, naomba uletwe haraka, ni jambo moja nzuri litakalowasaidia Watanzania kupata afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ninalotaka kuongelea, ni suala la kujenga uwezo wa makandarasi wetu ndani najua miradi mingi inatekelezwa na makandarasi na miradi mikubwa mingi tunatoa kandarasi kwa makandarasi kutoka nje. Tulianzisha Bodi ya Usajili wa Makandarasi ili tuweze kuinua uwezo wa wakandarasi wetu. Ile bodi ina kazi ya kusajili pia na kufuta, kama kuna wakandarasi hawaendi sawasawa na maadili ya ukandarasi ile bodi ina uwezo wa kufuta, kwa hiyo tusiogope kuwawezesha wakandarasi wetu kupata kazi. Suala kubwa ni kwamba kwa sababu naamini kabisa wapo wakandarasi ambao wapo daraja la kwanza, kwa maana kwamba kazi yoyote ile inaweza hata ile Stiegler’s gorge lingeweza kujengwa kujengwa na wakandarasi wetu wa daraja la kwanza, kinachohitajika ni kuwasimamia na kwamba pale ambapo wakandarasi wamefanya kazi, wawe wanalipwa kwa wakati. Wengi wameshindwa kuendelea na kazi ya ukandarasi ni kwa sababu Serikali imekuwa inachelewa kuwalipa kwa kazi ambazo wamekuwa wamefanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kama anakaa miaka miwili, miaka mitatu hajalipwa baadaye tunaanza kusema yule mkandarasi ni mwizi kumbe hajalipwa, kwa hiyo naomba Serikali jambo hili ijaribu kuangalia ili wakandarasi wetu na kwa kweli tutafurahi sana kama kila kazi itafanywa na wakandarasi wetu wa ndani. Nadhani hata ukienda China sehemu kubwa ya wakandarasi wanaofanya kazi kwao kule ni wao wenyewe wa China, hakuna Watanzania wanafanya kazi kule China. Sasa na sisi Taifa letu la uchumi wa viwanda lazima tufike mahali kazi zote zifanywe na wakandarasi wetu wa wazalendo ili tuwezeshe Mfuko huu utoke kutoka Serikalini uende kwa watu wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka kuongelea ni suala la kilimo. Ni kweli tunajenga uchumi wa viwanda, lakini uchumi wa viwanda kama hatujainua kilimo, hautakuwa na manufaa kwa sababu tunajenga reli sawa, lakini mazao ya kupitisha pale yatatoka wapi. Kwa hiyo ni lazima tuwe na mkakati wa kutosha kuhakikisha kwamba kilimo chetu kinakua. Tuwe na pamba ya kutosha ya kuitoa Mwanza kuleta bandarini na tukauza nje, tuwe na chai ya kutosha na mazao mengine ambayo tumeweka ni ya kimkakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nafikiri jambo lingine la kuangalia ni katika kuwezesha wakulima wetu wapate mbolea kwa wakati, lakini mbolea kwa bei elekezi ambayo Serikali imeshaianzisha, naipongeza mpaka sasa wanakwenda vizuri lakini nafikiri tufanye vizuri zaidi, tuangalie yale maeneo ambayo yalikuwa ni matatizo basi sasa hivi tuweze kuyaboresha ili wananchi wetu wapate mbolea kwa wakati na mbegu ili kilimo hiki kiweze kukua. Pia tusaidie wakulima hawa kupata soko kama wenzangu walivyosema, soko limekuwa ni tatizo, mwaka juzi mahindi yalikuwa yanauzwa kwa Sh.20,000 kwa gunia leo yanauzwa kwa Sh.80,000 kwa gunia, napongeza sana hali hiyo. Hii inatokana na masuala ya tabia nchi, kwamba mikoa mingi haikuweza kupata mavuno ya kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana tuweke nguvu katika kujenga miundombinu ya kilimo cha umwagiliaji, hatutaweza kukuza kilimo kwa kutegemea mvua na miaka hii nimeona mvua inapungua mwaka hadi mwaka. Kwa hiyo, niombe Serikali katika Mpango huu tuweke fedha za kutosha kwenye kilimo cha umwagiliaji, tumekuwa tunaweka fedha lakini hazitoki, naomba awamu hii ya mwisho wa Mpango huu zitoke fedha za kutosha, tuone utekelezaji wa kilimo cha umwagiliaji, naamini kabisa ndiyo mkombozi mkubwa wa kutufikisha katika uchumi wa viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa nafasi hii. (Makofi)