Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

Hon. Angelina Adam Malembeka

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

MHE. ANGELINA A. MALEMBEKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Ninaitwa Angelina Malembeka, Mbunge wa Viti Maalum kutoka Mkoa wa Kaskazini, Unguja.
Awali ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kufika hapa. Nashukuru Chama changu cha Mapinduzi na Jumuiya zake zote tatu kwa kazi nzuri iliyoifanya ya kufanya kampeni nchi nzima na kutuwezesha Wabunge wa Viti Maalum kuingia humu ndani, sambamba na Wabunge wa CCM. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naunga mkono kwa nguvu zangu zote hotuba ya Mheshimiwa Rais Magufuli. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wenzangu wamechangia mengi kuhusiana na michezo, wanahabari, elimu, afya, maji, reli, umeme, kilimo uvuvi, rushwa, barabara, utawala bora, biashara, ukusanyaji wa mapato na mengineyo yote nayaunga mkono. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wangu katika hotuba ya Mheshimiwa Rais, napenda kuchangia ukurasa wa 35 paragraph ya pili na ukurasa wa 36 paragraph ya pili; kwa ridhaa yako naomba niyarudie maneno yale. Ukurasa wa 35, paragraph ya pili inasema; “Mheshimiwa Spika, tunaitwa Waheshimiwa kwa heshima ya dhamana tuliyopewa na Bunge hili Tukufu, tutunze heshima hiyo ili tuzidi kuheshimiwa.” Mwisho wa kunukuu.
Ukurasa wa 36 unasema; “Mheshimiwa Spika, nimejitahidi kuzungumza kwa uchache, lakini napenda kukushukuru sana tena, Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa viongozi wote, tuliokaribishwa kuingia katika ukumbi huu na kuhudhuria yaliyojitokeza na mmeona kuna kazi kubwa, kwa sababu bado kuna watoto wengi, mwendelee kuwavumilia na kuwafundisha na Watanzania wamewaona.” Mwisho wa kunukuu na baada ya hapo kilifuata kicheko na makofi. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, hayo ni maneno makali ambayo Mheshimiwa Rais ameongea kwa unyenyekevu mkubwa. Yale maneno ukiyaangalia kwa haraka unaona yanachekesha, lakini maneno hayo ni makali. Humu ndani hakuna watoto! Kuna watu wazima, Waheshimiwa Wabunge, wenye umri mkubwa na wenye busara; lakini kutokana na sababu za wachache humu ndani watu wote tunaonekana watoto. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, humu ndani tumeshindwa kuonesha nidhamu kati ya Wabunge na Wabunge, tumeshindwa kuonesha nidhamu baina ya viongozi wetu wa nchi, tumeshindwa kuonesha nidhamu kwa viongozi wetu wa vyama, tumeshindwa kuonesha nidhamu baina ya Wabunge na viongozi wetu wa Bunge tuliowachagua, lakini pia tumeshindwa kuonesha nidhamu kwa wananchi waliotuchagua.
Mheshimiwa Naibu Spika, humu ndani wanasema siyo shwari. Mimi nasema humu ndani ni shwari, isipokuwa siyo shwari kwa wale wa upinzani. Wamekuwa wakilalamika kwamba Chama cha Mapinduzi tunakula pesa, tunamaliza hela ya Serikali, tunamaliza hela ya umma.
Mheshimiwa Naibu Spika, wewe utakuwa shahidi, wanakuja hapa, wanasaini, wanachukua hela ya wananchi, wanaondoka. Hivi ni nani alienda kuomba kura akisema naomba mnichague nikamzomee Rais? Ni nani alienda kuomba kura akasema, nipe kura yako niende nikamzomee Spika? Ni nani aliyeomba kura akasema, ninaomba kura yako niende nikamzomee Mwanasheria Mkuu wa Serikali? Ni nani aliyeomba kura akasema ninaomba kura yako ili niende nikawazomee Wabunge? Ni nani aliomba kura akasema naomba nichague ili nikisaini posho nitoke? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunalidhalilisha Bunge! Tunakula pesa za wananchi bila sababu. Kama kweli wana uchungu wakae ndani ya ukumbi huu waongee, wachangie hoja, tuzijibu, tushindane kwa hoja, siyo kwa kuzomeana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niseme, wamekaa wanalalamika, Zanzibar siyo shwari. Mimi natoka Zanzibar, Kitope, Kichungwani, Mkoa wa Kaskazini Unguja, Jimbo la Mahonda. Sijatemewa mate, sijapigwa makofi na niko salama, isipokuwa wao kwao siyo shwari, ndiyo maana kutwa wanazomea.
Mheshimiwa Naibu Spika, humu ndani kuna watu wana heshima zao, watu wakubwa sana; tuna watoto wa Marais ambao wako humu ndani, wameingia kihalali kama Wabunge, hawezi kukubali baba zao wanatukanwa tunawaangalia. Kuna watu humu sisi ni shemeji zetu, wajomba zetu, watoto wetu, wakwe zetu, wanatukana humu ndani tunawaangalia. Uvumilivu una mwisho wake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, siku zote huwa wanasema nyoka wa kijani haumi, mimi ninakuhakikishia siku akiuma hana dawa! (Makofi/Kicheko)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa
muda wa Mzungumzaji)
MHE. ANGELINA A. MALEMBEKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nikuhakikishie, kama mtu anasema hataki… (Kicheko/Makofi/Kelele)
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hotuba ya Rais. (Kicheko/Makofi/Vigelegele)