Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge la Kuridhia Mkataba wa Kimataifa wa FAO wa Kuzuia Uvuvi Haramu kupitia Bandari za Nchi Wanachama pamoja na Azimio la Bunge la Kuridhia Mkataba wa Kuanzishwa kwa Ushirikiano wa Kimataifa wa Nishati ya Jua (The Framework Agreement on the Establishment of International Solar Alliance)

Hon. Mbaraka Kitwana Dau

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafia

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Azimio la Bunge la Kuridhia Mkataba wa Kimataifa wa FAO wa Kuzuia Uvuvi Haramu kupitia Bandari za Nchi Wanachama pamoja na Azimio la Bunge la Kuridhia Mkataba wa Kuanzishwa kwa Ushirikiano wa Kimataifa wa Nishati ya Jua (The Framework Agreement on the Establishment of International Solar Alliance)

MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa fursa hii, ili niweze kuchangia kwenye Azimio hili, awali ya yote ninaunga mkono Bunge letu kuridhia Itifaki hii ya kuzuia Uvuvi haramu.

Mheshimiwa Spika, ni ukweli usiokuwa na shaka katika eneo letu la exclusive economic zone (EEZ).

SPIKA: Waheshimiwa katika kuchangia mnaruhusiwa kuchangia ama mojawapo ya Azimio hili ama Maazimio yote katika uchangiaji wako. Lakini pia niwakumbushe Kamati ya Uongozi tukitoka saa saba by saa saba na nusu tuwe pale kwenye Ukumbi wa Spika, Kamati ya Uongozi tukutane Ukumbi wa Spika kuna kikao kidogo, Mheshimiwa Mbaraka Dau endelea.

MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa ufafanuzi huo, nitachangia kwenye Azimio la Itifaki ya Uvuvi haramu, ni ukweli usiokuwa na shaka katika eneo letu la exclusive economic zone EEZ kumekuwa na vurugu nyingi sana ya meli za kigeni zinazoingia kwenda kuvua kule bila ya na vibali na ruhusa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa haina uwezo, ilikuwa haina uwezo wa aina mbili, haina uwezo wa Vyombo vya kwenda kuwazuia kule kwa sababu ni mbali na bahari ni kali sana, lakini la pili tulikuwa hatuna uwezo kwa sababu Mikataba kama hii ya Kimataifa haikuwepo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Itifaki hii inakwenda kujibu swali hilo gumu kwamba sasa tunao uwezo, wale ambao wataingia katika eneo letu la EEZ na tukaweza kuwaona kwenye ile VMS Versa Monitoring System yetu pale DSFA. Tunao uwezo sasa wa kwenda kuwafatilia watakapokwenda kuweka nanga meli zao katika nchi Wanachama hizi sitini, tunaweza kwenda kufatilia kule na kujua kwamba meli kadhaa iliingia katika EEZ ya Tanzania bila ya kibali ikavua na sasa Serikali inachukua hatua.

Mheshimiwa Spika, sasa faida kubwa inayopatikana ni hiyo, na mimi katika faida hiyo nilikuwa na maombi au nyongeza au ushauri kwa Waziri mwenye dhamana wa aina tatu, ushauri wa kwanza, twende tukafanye overall ya regulation zetu, Kanuni zetu za ile Taasisi yetu ya Uvuvi wa Bahari Kuu.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu gani? Kwa sababu sasa tunayo nyenzo ya kujua kwamba kuna meli iliingia kwenye EEZ yetu haina kibali ikaenda kutia nanga labda Seychelles tunatumia Mikataba ya Kimataifa kuikamata kule, Je, tumeshaikamata sasa tunafanya nini? Kwa sababu Sheria inataka ile meli au meli zile zije zihukumiwe kwa mujibu wa Sheria za Tanzania. Sasa ipo haja sasa ya kwenda kufanyia overall zile Kanuni zetu kwamba sasa je, meli ya aina hii inayokamatwa itaingia kwenye kosa lipi? Tunaitaifisha, tunapiga faini, tunafanyaje?

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nilikuwa naomba wenzetu wa, na nimemsikia Mkurugenzi Mkuu hapa wa Mamlaka ya Bahari Kuu yupo wenzetu wa Wizara kwa kushirikiana na Mamlaka ile waende wakaanze kufanyia kazi hizo regulation sasa ili tuweze kunufaika na hii Itifaki.

Mheshimiwa Spika, ombi au ushauri wa pili, Bandari ya Uvuvi limesemwa hapa na Kamati, limesemwa na Taarifa ya Kambi Rasmi ya Upinzani, bila ya kuwa na Bandari ya Uvuvi na nilizungumza hapa nadhani wiki iliyopita, bila ya kuwa na Bandari ya Uvuvi faida hizi zinatutoka kwa sababu hii EEZ yetu kwa wakati mmoja inaweza ika-accommodate meli zaidi ya mia moja, zinavua wakishavua wanakwenda kwa wenye Bandari za Uvuvi Seychelles, Mauritius, Mordait na maeneo mengine huko.

Mheshimiwa Spika, sasa sisi tunakosa haya manufaa tukiwa na Bandari yetu ya Uvuvi zile zile meli zile tutazishawishi zije huku kwenye Bandari yetu zianze kushusha ule mzigo wafanye processing halafu baadaye na biashara yenyewe itaanza ku-boom kama vile ambavyo tulishuhudia biashara ya minofu ya samaki kule Mwanza kipindi kile Ndege zinakuja kuchukua mzigo na kuondoka.

Mheshimiwa Spika, nafasi ile bado tunayo kwa kupitia Itifaki hii na kuweza kufufua au kujenga Bandari yetu ya Uvuvi ambayo itasaidia sana katika kuwavutia sasa hawa wenye meli, tunaweka regulations kwa mfano sasa hivi tuna regulation zinazowataka wale wanaovua katika Bahari Kuu waje katika Bandari zetu, lakini wanashindwa kuja kwenye Bandari zetu kwa sababu hatuna Bandari za Uvuvi, tuna Bandari za Mizigo na Sheria za Kimataifa zinakataa kushusha mzigo wa chakula kwenye Bandari ya Mizigo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naendelea kusisitiza na kumuomba Mheshimiwa Waziri ule mchakato wa kujenga Bandari ya Uvuvi hata hii ya kununua meli inaweza ikasubiri tuanze na Bandari ya Uvuvi, ikijengwa Bandari ya Uvuvi multiply effect yake ni kubwa sana.

Mheshimiwa Spika, kutakuwa na ajira kwa vijana wetu kwa sababu inakuja na logistics centers zile, kutakuwa na ajira, biashara ita-boom kwa maana ya kwamba sasa mizigo itakuwa inakwenda ama kupitia Uwanja wa Ndege au kupitia kwenye Bandari zetu kwenda sokoni na maeneo mengine ya nchi.

Mheshimiwa Spika, kwa kumalizia, pia nina ombi jingine dogo kwa Mheshimiwa Waziri, tumeona kwamba moja ya faida tutakazozipata hapa ni kunufaika na misaada mbalimbali inayotolewa na FAO kwa Tanzania. Kule Mafia eneo la Kitutia ndiyo nursery, ndiyo labour ya samaki zaidi ya asilimia 70 wanaozaliwa katika Bahari ya Hindi, lakini eneo lenyewe la Mafia limechoka, eneo lenyewe halitunzwi, eneo lenyewe wananchi wale ambao wanaitunza ile rasirimali hawanufaiki na chochote.

Mheshimiwa Spika, ningeomba kupitia Itifaki hii na Mheshimiwa Waziri tumeambiwa kwamba kutakuwa na aina hiyo ya misaada mbalimbali, basi tuangalie namna gani lile eneo litakavyoweza kutunzwa vizuri na kuweza kuleta manufaa makubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa fursa hii, na ninaridhia Bunge letu liliridhie Itifaki hii ya Uvuvi haramu katika Bahari Kuu, nakushukuru sana. (Makofi)