Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge la Kuridhia Mkataba wa Kimataifa wa FAO wa Kuzuia Uvuvi Haramu kupitia Bandari za Nchi Wanachama pamoja na Azimio la Bunge la Kuridhia Mkataba wa Kuanzishwa kwa Ushirikiano wa Kimataifa wa Nishati ya Jua (The Framework Agreement on the Establishment of International Solar Alliance)

Hon. Prof. Anna Kajumulo Tibaijuka

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Muleba kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Azimio la Bunge la Kuridhia Mkataba wa Kimataifa wa FAO wa Kuzuia Uvuvi Haramu kupitia Bandari za Nchi Wanachama pamoja na Azimio la Bunge la Kuridhia Mkataba wa Kuanzishwa kwa Ushirikiano wa Kimataifa wa Nishati ya Jua (The Framework Agreement on the Establishment of International Solar Alliance)

MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Mimi pia naomba niungane na waliotangulia kuwapongezeni Waheshimiwa Mawaziri wote wawili waliotuletea mikataba hii ya Kimataifa kusudi na sisi tuweze kuiridhia. Katika uchangiaji wangu, ni jambo zuri na wote kama ilivyosema, hasa ule mkataba wa FAO, nataka kusema kwamba ni mkataba umekuwepo kwa muda mrefu mimi nimeushuhudia wakifanyiwa kazi bado niko huko Umoja wa Mataifa. Sasa niseme kwamba labda ni muhimu sana kusema, kwamba kwa kuwa tumechelewa kidogo kuridhia mikataba hii mimi nimefarijika sana kuona kwamba katika Bunge hili Tukufu inaonekana pande zote tunakubaliana kwamba turidhie, kwa hiyo naunga mkono hoja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa katika kuridhia hilo na Serikali katika kutupa taarifa nina mambo mawili ya kusema. Kwanza naomba Mheshimiwa Waziri wetu wa Mifugo na Uvuvi ajaribu kuangalia kwa wenzake hali tuliyo nayo huko katika bahari kuu. Maana ninachofahamu mimi ni kwamba sisi Tanzania tuna haki ya kupewa eneo zaidi katika bahari kuu ambayo bado tunalidai. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kazi hiyo imekwama kule Umoja wa Mataifa na nadhani sasa Mheshimiwa Waziri Mpina wewe ndiwe mhamasishaji, wewe ndiwe mwenye samaki, wewe ndiwe mwenye viumbe kule baharini. Nadhani ni muhimu kuangalia mchakato wa kudai extended continental shelf ya Tanzania umefikia wapi. Kazi naifahamu kwa sababu mwaka 2012 nikiwa Waziri wa Ardhi niliwakilisha Umoja wa Mataifa New York kwenye kamati husika ya International Convention on the Taw of The Sea, kudai eneo letu. Sasa tusipoangalia tunaweza tukaridhia mikataba hii lakini kuna sheria zinazotawala utawala wa maji duniani, International Law of the Sea. Labda ingekuwa ni vizuri kulijulisha Bunge hili mchakato huo umefikia wapi.

Mheshimiwa Spika, labda kwa kufafanua zaidi; ni kwamba tumesikia hapa, na kamati imezungumza vizuri, kwamba exclusive economic zone ni nautical mile 200 unapewa baada ya maji yako (territorial waters). Lakini Tanzania kwa sababu ya mito yetu, hususan Mito ya Rufiji, Pangani, Wami; ndiyo inalisha viumbe baharibini. Kwa sababu hiyo tunastahili kupewa nautical mile 150 zaidi ndani ya bahari.

Mheshimiwa Spika, sasa hiyo ni hazina kubwa ya Taifa, na ninadhani kwamba Mheshimiwa Waziri wa Uvuvi aangalie na wenzake wanaohusika hususani Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Waziri wa Ardhi kwamba hatupotezi hazina hiyo, kwa sababu unapopeleka maombi Umoja wa Mataifa kuna muda usipofatilia unaweza ukaondolewa kwenye orodha. Kwa hiy ni jambo ambalo nimeona kwamba niliseme na huu ni wakati wake.

Mheshimiwa Spika, tunaporidhia mkataba huu pia tujue utawala wa bahari duniani na tutaweza kudhibiti huo uvuvi haramu katika bahari zetu. Suala la uvuvi haramu nadhani ni suala ambalo wote tunakubaliana kwamba ni suala hatari lakini pia ni suala la teknolojia na sisi kama nchi inayoendelea wakati mwingine tufaidike kwa kuomba misaada pale tunapohitaji. Kwa sababu uwezo pia wa kudhibiti hizi meli kubwa, gharama inayohitajika na teknolojia inayohitajika unaweza kukuta kwamba hatuna. Tukisharidhia mkataba kama huu na sisi basi; na imesemwa na wengine; tunaweza pia kuomba msaada wa wataalamu, vifaa na fedha za kutusaidia kuhakikisha kwamba hapa kwenye bahari yetu kuu si inakuwa shamba la bibi, kwamba kila mtu anafanya anachotaka na hasa uchafuzi wa sumu zinazotupwa katika bahari yetu.

Mheshimiwa Spika, ilifikia kuna mahali pale wala siendi mbali pale Kawe Beach waliwahi kutupa magunia ya sumu hatari kwa hiyo unakuta vitu kama hivi wanaendelea kwa sababu hatujajua...

MHE. MUSSA A. ZUNGU: Mheshimiwa Spika, taarifa.

T A A R I F A

SPIKA: Ndio taarifa tafadhali Mheshimiwa Zungu

MHE. MUSSA A. ZUNGU: Mheshimiwa Spika, naomba kumpa taarifa Mheshimiwa Profesa. Kwanza nimpongeze kwa kazi kubwa aliyoifanya ya kuhakikisha extended ya continental shelf ya Tanzania na kupata hizo km 150. Juzi mimi nilikuwa umoja wa mataifa tumelifatilia hili suala tuko katika namba 59 ya shauri la Umoja wa Mataifa na limekaa vizuri. Tatizo vikao vya Umoja wa Mataifa havikai kutokana nchi wanachama ambao wako kwenye commission ile wanatakiwa walipiwe gharama zao za kuhudhuria vikao na nchi zao kwa vile nchi zao hazilipi gharama ile commission haikai. Kwa kutokukaa justice delayed justice denied tunakosa haki yetu.

Mheshimiwa Spika, vilevile Kenya nao wana shauri na Somalia na shauri lile linaweza likatuathiri kama Somalia wakishinda kutokana na mpaka kati ya Kenya na Pemba. Kwa hiyo nilitaka nimpe taarifa tu kwamba suala liko vizuri Serikali wanalifuatilia na kamati tuko karibu nao kuhakikisha haki ya Tanzania inapatikana. (Makofi)

SPIKA: Asante sana ni kweli Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nje alikuwa UN kwenye General Assembly akifatana na Waziri wa Mambo ya Nje hivi juzi tu. Mheshimiwa Profesa Tibaijuka endelea na mchango wako.

MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA: Mheshimiwa Spika, ninashukuru sana kwa Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nchi za Nje na nimefarijika kusikia kwamba suala hilo linafatiliwa ni muhimu sana. Sasa nikirudi kwenye uwezo wetu wa kutekeleza hii mikataba tukishasaini. Sisi ni nchi inayoendelea, bado tuna haki ya kupata msaada wa hao wenzetu waliotangulia. Kwa kweli wenyewe kwa sababu ya teknolojia zao ndio wana uwezo wa kuchafua na kutumia hizi mbinu haramu ambazo zinakuwa na athari kubwa. Kwa hiyo tusibaki nyuma, Mheshimiwa Waziri usibaki nyuma katika kuweka sasa ufatiliaji ambao ni chanya. Kuna ufatiliaji mwingine ni urasimu tu mtu hana vifaa atakaa anasumbua meli anaweza akaleta kero.

Mheshimiwa Spika, mimi nafikiria kwamba tufanye kazi kwa weledi kwa sababu tunaposema tuweke watu wa kudhibiti, je, wana uwezo wa kudhibiti? Wanakuja kufanya juhudi au kama Mwalimu Nyerere alivyosema, kwamba ni juhudi bila maarifa. Suala hili ni muhimu sana hasa katika vyombo tunavyojiwekea kudhibiti.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili nirudi sasa kwa haraka kwenye suala la mkataba wa umeme wa jua. Umeme wa solar huu na umeme wa jua ni kitu kizuri sana. Naomba kusema kwamba sisi kitu kimoja kinachotukwaza kama taifa linaloendelea na kama taifa lenye vijana na vijana ambao hawana ajira ni kushindwa kuweka utaratibu kwa vijana kuunda kampuni za solar zitakazoweza kuleta teknolojia katika nyumba na kutoa huduma.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, nirudi sasa kwa haraka kwenye suala la mkataba wa umeme wa jua. Umeme wa solar huu na umeme wa jua ni kitu kizuri sana. Naomba kusema kwamba lakini sisi kitu kimoja kinachotukwaza kama Taifa linaloendelea na kama Taifa lenye vijana na vijana ambao hawana ajira ni kule kushindwa kuweka utaratibu kwa vijana kuunda makampuni ya solar yatakayoweza kuleta teknolojia katika majumba na kutoa huduma. Kutegemea TANESCO bila kutumia solar ni kutwanga maji kwenye kinu kwa sasa hivi.

Mheshimiwa Spika, nafikiri ingekuwa ni bora Mheshimiwa Waziri akatueleza sasa anavyojaribu kusaidia vijana wetu hawa ambao tunawaambia wajiajiri wakati sisi tumeajiriwa, lakini hatuwawekei utaratibu wa kwa mfano kuunda kampuni mahususi ambazo zitaweza kueneza umeme wa solar; vijana wanamaliza Engineering wapo kule mijini hawana kazi.

Mheshimiwa Spika, nadhani tunaposaini mkataba kama huu ni fursa muafaka pia kuwapatia teknolojia, lakini na huduma inayotakiwa maana yake unaposambaza kitu kipya kina ukakasi, ukiwaambia watu tukufungie solar yeye anaona nyaya za TANESCO zinapita juu anaona unamsumbua kama unamfanyia shamba la majaribio, kwa hiyo mtu anataka kitu ambacho ana uzoefu nacho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tukiwa na vijana ambao wanaweka makampuni ya kuhakikisha kwamba yanapata soko, sasa kazi yetu nini? Kazi yetu ni halmashauri, kuweka sehemu ili ziwape masoko inaitwa public procurement ambayo ni lazima iwezeshe dissemination ya teknolojia, teknolojia mpya haiwezi kusambaa kama haina Public Procurement Policy inayoi-support yaani kwamba kule kununua kwa upendeleo kabisa kampuni za vijana, ndiyo tutaweza kuondokana na hii ngonjera ya umeme wa solar umeme wa solar, lakini watu hawapo tayari kuwa kwenye majaribio, tuwawekee uwezeshaji.

Mheshimiwa Spika, huo ndiyo mchango wangu, naunga mkono hoja. (Makofi)