Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti Kuhusu Shughuli Zilizotekelezwa na Kamati hiyo Katika Kipindi cha Mwezi Februari, 2019 Hadi Januari, 2020 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma Kuhusu Shughuli Zilizotekelezwa na Kamati Hiyo Katika Kipindi cha Mwezi Februari, 2019 Hadi Januari, 2020

Hon. Mussa Bakari Mbarouk

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Tanga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti Kuhusu Shughuli Zilizotekelezwa na Kamati hiyo Katika Kipindi cha Mwezi Februari, 2019 Hadi Januari, 2020 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma Kuhusu Shughuli Zilizotekelezwa na Kamati Hiyo Katika Kipindi cha Mwezi Februari, 2019 Hadi Januari, 2020

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, labda kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametujalia afya njema na uhai tukaweza kukutana hapa tukaweza kuzungumza mambo mbalimbali yanayohusu Bunge letu na nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze tu kwanza kwenye suala zima la bajeti, bajeti ni makadirio ya mapato na matumizi kwa Serikali au taasisi yoyote ile kwa mwaka au kwa mwezi au vyovyote vile viwavyo. Mara nyingi tumekuwa tunapitisha bajeti ambazo hazitekelezeki, tunapitisha bajeti lakini kwenye upelekaji wa fedha sasa inakuwa kiwango kilichohitajika katika bajeti hizo hakitekelezeki. Vilevile pia, kumekuwa na ucheleweshaji wa fedha katika miradi, kwa mfano miradi inayosimamiwa na halmashauri fedha unakuta inapelekwa katika robo ya mwisho ya mwaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, matokeo yake sasa zikifika katika halmashauri kwa sababu wanaogopa usije mwaka wa fedha ukaisha fedha ile ikarudi Hazina, matokeo yake inapitishwa miradi ya haraka haraka, miradi inakuwa iko chini ya kiwango, miradi haikaguliwi ipasavyo na matokeo yake sasa fedha zile zinakuwa kama tumekwenda kuzitupa. Nashauri Serikali ipeleke fedha mapema pale ambapo imekusudia kupeleka fedha za miradi katika halmashauri zetu na miradi yoyote ile ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni katika halmashauri kuzipora nazo vyanzo vya mapato. Kwa mtazamo wangu naona kama vile Serikali Kuu sasa imeamua kuziua Serikali za Mitaa kwa sababu hapa mwanzo tulichukua property tax ikapelekwa TRA lakini baadaye tena ilipokuja TARURA tukaambiwa parking, mabango na bus stands na mapato mengine yote yanapelekwa TARURA. Ukipatazama hapa TARURA imepewa mamlaka ya kukusanya mapato lakini taa za barabarani, usafishaji wa mifereji bado uko kule kule kwenye halmashauri. Halmashauri watapata wapi fedha ya kununua luku au ya kulipia umeme wa taa za barabarani? Nasema hapa tunaziua Serikali za Mitaa (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilikuwa nashauri, hebu tuziache vile vyanzo vilivyobaki navyo sasa tuache halmashauri iendelee kukusanya mapato. Tumekuwa tukiwang’ang’ania kwamba nyingine zinakuwa zinakusanya chini ya kiwango na kwa mfano jana hapa wakati tulipokuwa tunapitisha taarifa za PAC na LAAC imefika mahali kwamba halmashauri zitakazoshindwa kukusanya mapato kwenye uvuvi inaambiwa waziri atazipoka mamlaka ya kukusanya mapato hayo. Sasa tujiulize halmashauri zitapelekwa vipi! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wasemaji wengi waliozungumza wamesema mpaka madiwani sasa wanakaa vikao bila kulipwa posho zao za mwezi wala hizi sitting au posho zao za vikao. Nasema halmashauri kama tumeamua kuziua tuseme wazi, tuweke wazi yaani tusifichefiche kwa sababu hizi halmashauri ndiyo Local Government, ndiyo Serikali za wenyeji, ndiyo zinazofikia kero zaidi za wananchi kuliko Serikali Kuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo zinazojenga madarasa, ndiyo zinazojenga barabara, ndiyo zilikuwa zinajenga labda shule, mifereji, maji taka na kadhalika lakini tunapora kila uchwao. Nina wasiwasi ipo siku tutakuja kuchukua vyanzo vyote tuwaambie wajitegemee watafute vyanzo vingine au wananchi tuwachangishe sasa kama vile kodi ya kichwa, hii itakuwa siyo sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nashauri hapa halmashauri ikibidi tuzipelekee fedha kwa wakati lakini pia miradi ambayo wameikusudia kuitekeleza ipelekwe fedha ambayo inatosha tusipeleke fedha pungufu. Tunapopeleka fedha pungufu miradi inakuwa imedumaa, utakuta majengo yamekaa muda mrefu hayaezekwi, zahanati zimekaa muda mrefu hazifanyi kazi, kwa hiyo, hapa nilikuwa nashauri fedha zipelekwe kwa mpango maalum.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nilikuwa nataka kusema ilikuwa ni kwenye suala zima hili la kodi kubwa kuwaua wafanyabiashara au kukimbiza wawekezaji. Nchi yetu tunasema tunataka Tanzania ya viwanda lakini ukitazama. Kwa maoni yangu naona kama tunasema hapa mdomoni tu. Hao wawekezaji wanapokuja katika nchi yetu adha wanayoipata wengine wamekuwa wanahama wanakimbilia nchi jirani. Ipo mifano mingi kwa mfano katika Jiji letu la Tanga tulikuwa na mwekezaji pale ana kiwanda cha kusaga unga wa ngano kinaitwa Pembe, Pembe Wet Flower Mill Co. Ltd. Ile iliajiri zaidi ya vijana 1000 pale Tanga lakini cha kushangaza sasa hivi imefungwa tangu mwaka jana mwezi wa tano kwa sababu ya kodi kubwa wanayotozwa na TRA. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, walikuwa na kiwanda tanzu cha kutengeneza vifungashio au visalfet inaitwa Bajeber Packaging Co. Ltd, nao pia wametozwa kodi kubwa wote kwa pamoja wamefunga viwanda, vijana wamekosa ajira sasa hivi ndiyo nasikia kama Tanga mmekuwa mkisikia kuna watoto wa ibilisi. Ni walewale vijana waliokuwa wakifanya kazi Pembe, wakifanya kazi CIC, wakifanya kazi viwanda vingine ambavyo vimefungwa hawana kipato, anategemewa na familia yake, anategemewa na wazazi wake, yeye mwenyewe anataka kutumia hana fedha matokeo yake wamejiita jina la ibilisi. Watoto wa ibilisi wamekuwa wanapora simu, wanawavizia akinamama wanapokwenda kwenye sherehe za harusi simu zinakwenda, cheni za dhahabu, viatu, fedha, vitu vyote wananyang’anya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali kama kweli tumekusudia kuwa Tanzania ya viwanda, wawekezaji wanapokuja tuwanyenyekee, tuwape ushirikiano tuwapunguzie kodi ili waendeshe shughuli za kibiashara, walipe kodi ya Serikali lakini pia waajiri vijana wetu. Kama itakuwa mpango ni huu ni sawasawa na kumkamua ng’ombe maziwa bila ya kumpa malisho matokeo yake sasa maziwa yakiisha tutakuwa tunakamua damu. Tunajisifu tu kwamba TRA wamekusanya sasa hivi trilioni 1.9 kwa mwezi, ni jambo zuri lakini tunajua hii 1.9 trillion inavyopatikana. Leo Dar es Salaam katikati ya Jiji Kariakoo ukitaka fremu pia unapata kwa sababu kodi zimekuwa ni kubwa wafanya biashara wameshindwa wanakimbilia nchi jrani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano, hata wafanyabiashara wa malori sasa taarifa tulizonazo ni kwamba wengine malori yao wameyahamisha Tanzania wameyapeleka Kenya, wengine wamekwenda kuyasajili Zambia, wengine wamekwenda kusajili Burundi, wengine wamekenda kusajili Malawi kwa sababu kodi tunazowatoza ni kubwa na tuna utaratibu ambao haupo dunia nzima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo dereva wa lori pia aambiwa awe EFD mashine, kwamba akipeleka mzigo wa cement labda Mwanza au Arusha akirudi akipakia hata magunia mawili au matenga kumi ya nyanya lazima alipe kwenye EFD. Wakati gari ikiharibika anatakiwa alizibe pancha, alipe njiani, alipe ma-tan boy na kadhalika, sasa wanaona imekuwa ni adha kubwa. Niseme baada ya kuhamisha usajili Tanzania wakapeleka nchi nyingine mapato yanaingia katika nchi hizo, naomba hapa Serikali ipaangalie upya, hebu tupunguze baadhi ya masharti kusudi tukaribishe kweli wawekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ninalotaka kulisema, kuna matumizi mabaya ya fedha za Serikali na vilevile pia, hii inatokana na kutofata demokrasia ambayo ni ya vyama vingi kama ilivyokusudiwa. Labda hapo nitoe mfano, kwenye jiji letu la Tanga kuna madiwani wamerudi kwenye Chama Cha Mapinduzi, ninavyojua na ndiyo utaratibu, kanuni na sheria ilivyo kwamba kiongozi wa kisiasa akihama chama kimoja kwenda chama kingine amepoteza sifa ya kuwa na nafsi hiyo aliyoitumia. Sasa inakuwa madiwani hawa wameshahama kutoka CUF wamehamia CCM wanaingia kwenye vikao vya Kamati ya Fedha, wanaingia kwenye Baraza la Madiwani na wanalipwa posho za vikao na fedha ya mwisho wa mwezi. Haya ni matumizi mabaya ya fedha za Serikali. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mbarouk ahsante sana.

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali iliangalie jambo hili kwa makini kwa sababu huu mchezo ukiendelea itakuwa sasa kama sheria na kanuni tulizozitunga na kuapa kuziheshimu na kuzitekeleza hazina maana yoyote. Ahsante.