Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Martha Jachi Umbulla

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia. Kwanza nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu, kwa kunijalia uzima na kuweza kusimama hapa kuchangia hoja
hii ya Wizara ya Elimu. Naomba na mimi nichukue fursa kama wenzangu nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri wa Elimu Profesa Ndalichako, na Naibu Wake Mheshimiwa Stella Manyanya, aidha nimpe pole kwa msiba wa mama yetu na Mungu ampe subira.
Mheshimiwa Naibu Spika, elimu ni ufunguo wa maisha na lazima Watanzania wapate elimu itakayowafungua katika maisha yao. Aidha, niipongeze sana Serikali ya Awamu ya Tano, kwa sababu imekwisha anza kuhakikisha kwamba Watanzania wanapata elimu wote na wanakuwa na ufunguo wa maisha kwa sababu ya kuanza mfumo wa elimu bure kuanzia shule ya msingi hadi sekondari kidato cha nne.
Mheshimiwa Naibu Spika, elimu ya msingi pamoja na sekondari hadi kidato cha nne ni kama msingi wa nyumba, na kama msingi wa nyumba ni imara basi elimu yetu ya msingi na sekondari itakapokuwa imara tutakuwa na elimu iliyo bora hadi vyuo vikuu na hatimaye Watanzania wote watakuwa na elimu bora Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini elimu bora pia inatokana na walimu walio bora, na wenye moyo wa kufundisha kwa sababu walimu ndio watakaoweza kuboresha elimu yetu na kwa hivyo ni lazima tuhakikishe kwamba changamoto zote zinazokabili elimu ya msingi na elimu ya sekondari tuweze kuzitatua ili dhamira yetu ya kuboresha elimu kuanzia msingi na sekondari iweze kutimia.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nianze kuzungumzia mazingira wezeshi kwa ajili ya walimu wetu hasa wa sekondari za kata. Walimu wetu wa sekondari za kata wako katika mazingira magumu sana, hasa sisi ambao tunatoka katika mikoa ya pembezoni. Walimu wengi wa sekondari hizi za kata wako katika maeneo ambayo hakuna umeme, maji, huduma mbali mbali za jamii, hospitali ziko mbali na hatimaye hata mitandao hizi ambazo vijana wengi wanazitumia hazipo; na kwa hivyo utaona changamoto nyingi zinazowakabili vijana hawa walimu ili waweze kufanya kazi katika Sekondari hizo ama maeneo hayo, inahitajika ushawishi ili waweze kuendelea kufanya kazi katika shule ama maeneo hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nilikuwa naiomba Serikali kwamba iweze kuangalia uwezekano wa kuwapa walimu wa sekondari za kata, na maeneo mengine yenye mazingira ambazo ni mbaya, waweze kupata hardship allowance ili iweze kuwapa motisha. Hili ni muhimu sana, najua walimu wengi wote wana matatizo ya hapa na pale, lakini hawa ambao wako katika sekondari hizi zenye mazingira ambayo sio wezeshi n wanahitaji uangalizi ama huruma ya Serikali kwa kuweza kuwapa motisha waweze kufundisha kwa sababu elimu bora kama ambavyo nilianza ni pamoja na mwalimu ambaye atakuwa na moyo wa kufundisha baada ya kuwezeshwa vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nataka kulizungumzia mengi yameisha zungumzwa. Lakini ni suala zima la kutenga maeneo ya shule ambayo yatawezesha kilimo ya mashamba na bustani. Tuki-refer elimu za hapo awali, shule zetu nyingi zinakuwa na mashamba ama maeneo ambayo wanafunzi wanalima na kilimo hicho kinaweza kikasaidia pia kuwapatia chakula cha mchana, ama matunda ambayo yatawajenga wanafunzi wetu kiakili, kimwili na kiafya. Kwa hiyo, najua changamoto ya ardhi ambayo inakumba nchi yetu hasa kwa maeneo ya mjini lakini bado kwa maeneo ya mikoani tuna ardhi ya kutosha.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo uanzishwaji wa shule ziende sambamba na maeneo ambayo wanafunzi watapata kulima na kuweza kujijenga kimwili na kiafya. Lakini vilevile kupata chakula kwa bei nafuu. Tukisema wazazi waendelee kuchanga kwa ajili ya chakula cha mchana cha wanafunzi, bado ni mzigo na kwa hivyo tutafute namna rahisi ya kuweza kuwapatia wanafunzi wetu chakula cha mchana, kupunguza pia utoro shuleni.
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie pia upungufu wa walimu wa sayansi. Hili limezungumzwa sana. Lakini mkoa wetu wa Manyara una upungufu mkubwa sana wa walimu wa sayansi, najua pengine na maeneo mengine lakini ya kwetu lazima niisemee, hatuna walimu kabisa wa masomo ya sayansi, kwa hivyo tunaomba Serikali iweze kuangalia inapo-allocate walimu, iweze kufikiria maeneo ambayo tayari kuna upungufu mkubwa wa walimu wa sayansi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali itafute kila mbinu, jinsi ambavyo ilipata mbinu ya kujenga maabara nchi nzima, tukaweza kujenga kwa kipindi kifupi. Hiyo ni hatua ya kwanza na tumemaliza, na mimi naipongeza Serikali, wanaoibeza wana lao, lakini tayari tuna maabara zetu, nina hakika kwamba walimu wa sayansi watapatikana. Serikali iweke juhudi ya hali ya juu, kuhakikisha kwamba walimu wa sayansi wanapatikana ili waweze kufundisha masomo ya sayansi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa maabara umefanikiwa, lakini ninajua kwamba suala hili lilikuwa suala kama la zimamoto na imetumia fedha ambazo zilikuwa zimekusudiwa kwa madhumuni mengine. Kwa mfano, huko katika Wilaya yetu ya Mbulu ama Mkoa wetu wa Manyara, maabara tumezijenga katika Wilaya zote, lakini tumetumia fedha ambazo zilikuwa zimetengwa kwa ajili ya miradi kwa hiyo baadhi ya miradi sasa hivi imekwama kwa kukosa fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano kulikuwa na ujenzi wa madaraja muhimu sana katika maeneo ya vijijini kama Daraja la Gunyoda kule Mbulu, ujenzi wa kituo cha afya kule Endagikoti, Mbulu, tayari miradi hii na miradi mingi ya umwagiliaji imekwama kwa sababu ya kukosa fedha, kwa sababu fedha zile zilikuwa diverted kwenda kujenga maabara. Naiomba Serikali iweze kuangalia hili na ihakikishe kwamba fedha hizi zinarudishwa ili miradi hii ya maendeleo iweze kuendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie pia suala zima la matatizo ya walimu wastaafu. Hili ni tatizo sugu na wengi wamelizungumzia, lakini ni kilio cha wastaafu walimu wengi ni lazima Serikali iwe sikivu, wananchi wanapolalamika kwa kipindi kirefu na kilio hiki cha wastaafu ambao hawapati stahili zao ni cha muda mrefu sana. Walimu wengi kipindi kile cha kupandisha madaraja kiliposimamishwa, wengi walikuwa wanaendelea kufanya kazi na huko wanastahili na wanapaswa kupandishwa daraja.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa suala hili lilikuja kufikia kupandishwa madaraja wakati wengi wameshastaafu vilevile, ninaiomba Wizara iangalie walimu ambao tayari walistahili kupandishwa na wamekaa katika cheo kimoja zaidi ya miaka 15, lakini hadi wanastaafu hawakuweza kupata stahili zao. Na sasa wako wengine ambao wamesimama kwa kipindi kirefu, mishahara yao inatofautiana na walimu ambao walikuwa nao wameajiliwa hata baada yao, lakini wana mishahara ambayo ni midogo sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana.