Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Shally Josepha Raymond

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana sana kwa nafasi hii ya leo, ambayo kwangu ni muhimu sana, hata nimeahirisha kwenda kufanya checkup ya afya yangu. Kipekee namshukuru Mungu kwa zawadi ya uhai, kwetu sote tuliokaa hapa tuweze kuzungumzia mambo ya maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, aidha nawashukuru wote waliotupatia sadaka zao, akiwemo Mbunge mwenzetu, lakini pia wako wale watu wa maziwa jana, tumepata maziwa ya ASAS, tumepata maziwa ya Tanga Freshi, asiyejua kushukuru hata hatabarikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Leo nimesimama hapa nizungumzie eneo moja tu la mifugo, na ni eneo la kuku na kuku siyo kuku wote, najikita kwenye kuku wa kienyeji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, msanii aliyeimba supu ya kuku wa kienyeji ni tamu sana, hakukosea ni kweli kabisa, toka tunakua, ukimuheshimu mgeni nyumbani, unamchinjia angalau kuku wa kienyeji ili apate kukarimika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni takribani mwaka wa nne sasa toka nimeingia Bunge hili na kila siku namfuata Waziri wangu wa Mifugo na Uvuvi nikiulizia vifaranga wa kuku wa kienyeji wanapatikana vipi? Niseme kwamba nimekuwa nikijibiwa, napewa namba za simu na kila ninapopiga, ambako amenielekeza sipati simu, lakini hilo haliniondoi kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri huyu kwa kazi zake nzuri ambazo zimeonekana kitaifa yeye pamoja na Manaibu Waziri wake wote, Makatibu Wakuu, Wakuu wa Idara mpaka Madereva wao wanaowaendesha kwa usalama Wizara hii itaweza kusonga mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wizara hii ni muhimu sana kwa wanawake, na hata dakika hii ukichukua sensa ya walio huku Bungeni, ukiondoa wale waliomsindikiza Mheshimiwa Mbunge aliyeapishwa, wengi ni wanawake. Wizara ya Mifugo na Uvuvi ni muhimu kwetu sisi kwa sababu bila Wizara hii hatuna kitoweo na sisi wanawake bila kitoweo nyumbani, hakuna chochote kinachokwenda mdomoni. Ukitaja maziwa, ni kitoweo, ukitaja samaki ni kitoweo, ukitaja kuku ni kitoweo, ukitaja ng’ombe ni kitoweo, ukitaja nguruwe ni kitoweo! Ukitaja yule mkuu wa meza ni kiweo, nitaje kipi ambacho siyo kitoweo, ambacho ni muhimu kwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kwetu wanawake, siyo tu tunataka kile kitoweo, tunataka kitoweo na ziada ya kutuingizia kipato. Ingekuwa wameweka mkazo kwenye kuku wa kienyeji, na kila mwanamke mtanzania au kila familia ikafuga kuku, na wale vijana wanaomaliza shule ambao hawajapata ajira wakafuga kuku, leo tungekuwa hatuna uhaba kabisa wa mayai, ambayo ni protein, tungekuwa hatuna uhaba kabisa white meat, kwa wale ambao hawataki kuongeza uzito, na pia tungekuwa hatuna upungufu wa protein popote pale.

Mheshimiwa Spika, lakini kundi hilo limeachwa na kuku hawa hawana kazi kubwa sana kuwalea, hawa ni scavengers, wanacharukacharuka tu, mtu akitaka kukuonyesha kwamba una harakati nyingine anakwambia wewe acha mambo ya kuku wa kienyeji. Yeye anachakurachakura huku na huku, lakini kuku hao sasa hivi wanafunikwa, wanafutika, utaambiwa kuna guchi, sijui kuna kuroiler sijui kuna crossbreed, ni lini sasa gene hii itatafutiwa utalaam wa kuikuza ili watu wengi zaidi wafuge kuku wa kienyeji? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni takribani miaka 58 sasa toka tumepata uhuru, lakini tatizo la ugonjwa wa mdondo bado ni usumbufu mkubwa, bila ya ugonjwa wa mdondo, ule wa new castle kwa lugha nyingine, kuku wa kienyeji wangezagaa huku. Niwasifu sana wenzetu wa Singida, ambao kwa kweli ukiuliza kuku hii imetoka wapi, Singida. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa najiuliza, niko hapa natamani wanawake wangu wote wa Kilimanjaro wafuge, kila mmoja awe na kuku wake wa kienyeji hata kama atamfugia chini ya uvungu, lakini mbegu haipatikani, napataje mbegu ya kuku wa kienyeji ili nikasambaze Kilimanjaro, kila mwanamke afuge, kila mwanafunzi afuge nikae kwenye geti la shule niwape vifaranga viwili viwili, wafuge kila mtu na shida ya kitoweo iondoke.

Mheshimiwa Spika, utanishangaa na wengine watanishangaa, kwa nini anang’ang’ana kuku wa kienyeji, gharama za kule kuku wa kienyeji ni kidogo sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba sana atakapokuja kujibu Mheshimiwa Waziri, anieleze, kwa nini wanaruhusu hii kutoa chanjo kwa kuku hawa ikawa ni mtu kutaka na isiwe ni mass vaccination ili sasa tufute na tutokomeze kabisa, kwenye mambo yake yake ya kipaumbele nimeyasoma, amesema kwamba natarajia kupunguza na hiyo iko kwenye ule ukurasa wa 13, kudhibiti, lakini naomba atokomeze kabisa.

Mheshimiwa Spika, baada ya kuzungumzia sana hao kuku wa kienyeji na kila mtu kunielewa shida yangu, na wale wanawake wangu wa Kilimanjaro na kokote wanawake wapo, naomba sasa nije kwenye kuwapa miradi vikundi vya akina mama popote walipo.

Mheshimiwa Spika, tukisema mitamba, mtamba mmoja mzuri anakwedna mpaka shilingi milioni moja, hatuwezi wanawake sisi. Nakwenda kwenye ng’ombe sasa, ili ng’ombe tumpate, tumfuge, tupate maziwa, tupate samadi ya kwenye mashamba yetu na kila mahali. Nilikuwa naomba Serikali, kwa vile Serikali yetu ya Awamu ya Tano ni sikivu na inapenda sana pia kutekeleza mambo ya Mwalimu Nyerere, irudi upya, kusambaza mitamba kama Mwalimu Nyerere alivyosambaza mitamba kwenye ile awamu ya kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, endapo tutafuga vizuri, tukakopeshwa mitamba, kopeshwa ng’ombe lipa ndama, tutaweza tena kuibua mbegu mpya ya mitamba mizuri yenye maziwa mengi, kuliko hii tunayofanya sasa hivi, wamesha crossbreed mara nyingi sana wenywe kwa wenyewe, na pia unakuta maziwa yanayopatikana sasa ni kidogo.

Mheshimiwa Spika, lakini pamoja na hayo, nimeona, kwenye kitabu tumeelezwa kwamba idadi kubwa imeongezeka kwenye artificial insemination, lakini basi ningeomba, hiyo artificial insemination ifanyike bure, tuwazalishie watu bure. Mwingine ng’ombe anapata joto anakuta hana hela ya kwenda kulipa, sasa hiyo inapoteza tena, anapoteza muhula mmoja wa kuendeleza au wa kuzalisha ng’ombe. Nilikuwa naomba sana, kama Mheshimiwa Waziri atanielewa ninalowaombea watu wangu wenye uwezo mdogo, tupate…

SPIKA: Malizia Mheshimiwa Shally.

MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Spika, nashukuru, naunga hoja mkono asilimia 100, ahsante sana Spika wangu. (Makofi)