Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Julius Kalanga Laizer

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Monduli

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia Wizara hii, nakushukuru sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti kwanza nianze kwa kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa uamuzi wake wa kiuungwana na wa kiutu na wa kibinadamu ambao haujawahi kufanyika katika historia ya nchi hii, ya kurejesha baadhi ya maeneo ya maliasili kwa ajili ya wafugaji wa nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Niliwahi kusoma maandiko Fulani, kwamba mwaka 1981 Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwalimuwa Nyerere, alisema maneno yafuatayo; Kwamba katika kumbukumbu zote amewahi kuona maeneo yakitengwa kwa ajili ya maliasili wanyama, maeneo kwa ajili ya wakulima, lakini hajawahi kuona mahali pametengwa maeneo kwa ajili ya wafugaji. Rais aliyekuja kutengua kauli hiyo ya Hayati Baba wa Taifa ni Mzee na Rais wetu Mzee John Pombe Magufuli kwa kurejesha maeneo makubwa ya wanyama kwa ajili ya wafugaji wa nchi hii. Tunamshukuru sana, na mimi naamini tutamlipa wema kama alivyotutendea wema huo,. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niwapongeze Wizara kwa sababu kama nao wasingekubaliana na maoni ya Mheshimiwa Rais wangeweza kushauri tofauti, lakini kwa sababu Waziri pamoja na Naibu wake, wote wanatoka katika maeneo ya wafugaji, jambo hili limewagusa na sisi tunaona kuwepo kwenu kwenye Wizara imetusaidia wafugaji wa taifa hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunawapongeza, Waheshimiwa Wabunge wamewapongeza, kazi nzuri, endeleeni kuchapa kazi. Ni mara ya kwanza na ninyi mnaona Wizara hii watu wanasimama wanapongeza ni kwa sababu kuna mabadiliko makubwa na ninyi mmekuwa wasikivu mmechukua ushauri wa Wabunge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini mimi nataka niwapongeze katika hili, najua bado tuna tatizo la wafugaji kuingia katika maeneo ya hifadhi, lakini tunajua kabisa wategemezi wetu ambao ni watalii ni wanaotoka nje ya nchi; hawafurahii sana kuona kila siku moshi kwamba wafugaji wamechomewa maboma. Kwa hiyo mimi nashauri bado hili jambo liendelee kushughulikiwa ndani ya nchi kwa utulivu bila kutumia vyombo vya habari ili kusionekane kwamba kuna uharibifu na kuna uvunjaji wa haki za binadamu kwa sababu inatuathiri sisi kimataifa katika suala la uhifadhi na suala la uwekezaji katika maliasili tuliyonayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijachangia katika maeneo ya kitaifa naomba nilete maombi yafuatato mezani kwa Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti moja wananchi wetu wenye WMA ya Randilen na ambayo unajua inafanya vizuri sana; wanamuomba Mheshimiwa Waziri akawatembelee kwa sababu ya tatizo la single entry. Akitoka katika hifadi ya WMA aje mpaka barabara ya Makuyuni, halafu aende Tarangire ni takriban km 30. Wao wanaomba kwa sababu kuna hoteli za Treetops kule na imekuwa ikitusaidia mapato; tufungue geti dogo ili wao waweze kuingia pale Tarangire. Wao wamesema watagharamikia gharama zote za kutengeneza lile geti dogo liweze kufanya kazi na tuweze kufanya kazi katika eneo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kabla ya kufanya hivyo, ili muweze kufanya tathmini ninaomba Mheshimiwa Waziri au Naibu wako afike akawasikilize wananchi wetu wa WMA ya Randilen ili waweze kufanya kazi yao vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tunaomba kabisa, wako wananchi wetu waliopoteza maisha kwa sababu ya wanyama kama tembo; lakini fidia hii na kifuta jasho vinachelewa sana. Mheshimiwa Waziri naomba upitie faili la wananchi wa Monduli waliopata madhara mwaka 2015, 2016 na 2017; na mwaka huu tunasikitika kwamba tumepoteza tena wananchi wawili, mmoja kutoka Lemoti na mwingine Makuyuni, mwezi wa tatu wameuawa na temba. Mtusaidie basi ili kifuta jasho hicho kitoke kwa wakati ili wananchi wetu waone kwamba uhifadhi huu ni wa kwao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili pia ninaomba, tunayo ahadi ya Mzee wetu Mkurugenzi wa TANAPA Kijazi, na nimemuona hapa na ninaomba anisikie, kwamba aliahidi kutusaidia kukamilisha Kituo cha Afya kilichoko kule Engaruka. Naomba Mzee wangu hili jambo ulitekeleze kwa sababu ni ahadi na mimi nimetangaza kwa wananchi ili tuone uhifadhi ambao ni ujirani wetu unafanya kazi; kama ambavyo mmekuwa mkitusaidia; mmetujengea mabweni, na hili hamshindwi naomba mlitekeleze na mtusaidie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini, Mheshimiwa Waziri, naomba hili pia la nyuki, sisi Monduli maeneo yote mnafahamu, upande wa kwanza tumezungukwa na Tarangire, upande wa pili Manyara, Lake Manyara na upande mwingine Ngorongoro, kwa hiyo jimbo letu tumezungukwa na uhifadhi pande zote. Tunaomba mtupe kipaumbele katika ufugaji wa nyuki hasa kwa wananchi ambao mashamba yao yamezunguka katika eneo hilo ili basi itusaidie kupata chakula, lakini vilevile itusaidie kufukuza tembo ambao wanaharibu sana mashamba yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho Mheshimiwa Waziri ni kuhusu sheria zetu za maliasili na utalii. Mheshimiwa Waziri unafahamu katika Sheria ya Corridor, imekupa mamlaka wewe kuyatoa maeneo ya wafugaji kwa ajili ya kufanya corridor na buffer zone. Hata hivyo Mheshimiwa Waziri unafahamu ardhi nyingi ni za vijiji, ninaomba kwenye kanuni zenu mtazame jambo hili ili katika kutenga maeneo na kuyatangaza maeneo hayo isibabishwe kuchukua ardhi ya wananchi ambao pia imekuwa kidogo sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuna ile Sheria ya Madini, Sheria ya Madini inasema Waziri wa Madini akishatoa leseni, mwenye leseni hiyo anaweza kwenda kuchimba madini mahali popote, na hili pia linaathiri sana mazingira yetu ya utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtazame jambo hilo, ili sheria hizo zisianze kuingiliana, tujue kwamba mwenye mamlaka ya uhifadhi, kama ni Waziri wa Maliasili asimamie maeneo ya maliasili, na kila dheria iweke limit, iwe na categorization; sheria hizi zisiingiliane, kama ni Sheria ya Maliasili, inavyotekelezwa isiingilie kwenye ardhi ya vijiji, na kama ni Sheria ya Madini inapotekelezwa isiingilie kwenye ardhi nyingine ambayo si ya kwake. Kwamba sheria hizi kwa sababu tunatumia ardhi wote ziwe specific na iishie katika mipaka ya sheria nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Mheshimiwa Waziri, na ninaomba katika hili kabisa, tuoneeni huruma, tunao wafugaji wetu ambao ng’ombe wameingia katika hifadhi za Serikali. Wananchi wale walienda Mahakamani, wameshinda kesi Mahakama za Wilaya, Mahakama za Rufaa, mpaka na Mahakama zote za nchi hii wameshinda. Hata hivyo wameshindwa kurudishiwa hawa ng’ombe, sisi tunasema mtufanyie huruma basi, kama wataalamu hawa hawataki kuheshimu hizo sheria na Mahakama zetu, basi mtuonee huruma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu tumeenda kwenye vyombo ambavyo tunaamini vinatoa haki, vimetoa haki hiyo lakini bado Serikali imekataa kuwaachia wale ng’ombe. Mheshimiwa Waziri, kwa unyenyekevu kabisa, kiuungwana, kama hatuheshimu hayo maamuzi ya Mahakama tuoneeni huruma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu jambo hili limefika Mahakamani na tumeshinda mtuonee huruma, sisi ni wafugaji. Mtu ukinyang’anywa ng’ombe 200, kwa bei ya kawaida tu ya shilingi laki tano ni shilingi ngapi hizo? Mwananchi yule amekuwa maskini, ametoa gharama ameenda Mahakamani, Mahakama iliona ameonewa na amepewa haki lakini bado ng’ombe wale hawajaachiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo yangu naomba kuunga hoja mkono, nakushukuru sana.