Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Dr. Dalaly Peter Kafumu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Igunga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi nichangie kidogo. Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri anayofanya, tunampongeza na tunaomba aendelee kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nataka nichangie mambo matatu tu. Kwanza, ukurasa wa nne wa hotuba ya Mheshimiwa Waziri inazungumzia dira, dhima na majukumu ya Wizara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa namshauri Mheshimiwa Waziri kwamba hii dhima na dira zikaandikwe vizuri kwa sababu ukisoma zinafanana. Dira anasema ni maliasili na malikale zinazohifadhiwa kwa manufaa ya Watanzania kwa ajili ya kukuza uchumi; hiyo ni dira. Dhima na yenyewe inasema, uhifadhi endelevu wa maliasili na malikale na kuendeleza utalii kwa manufaa ya taifa. Hivi vitu vinafanana, ni vizuri kuandika dira ambayo inaonyesha tunaenda wapi baada ya miaka kadhaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Lakini, dhima iwe ni tunafanyafanyaje kwenda kwenye hayo mahitaji tunayotaka kuyafikia, kwa namna hii imefanana, naomba nitoe huo ushauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni kwamba, Mheshimiwa Rais aliagiza maeneo yote yenye migogoro ya wakulima na wafugaji yafanyiwe kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na kweli amesema, iliundwa Kamati ya Mawaziri wanne na wameenda na wamemaliza kazi lakini kuna maeneo hawajafika. Kule kwetu Manonga Wembele Game Reserve Mawaziri hawa hawajafika na wananchi bado wanagombana; nilikuwa naomba nako mfike. Pamoja na kwamba tumeanza kufanya mapatano lakini tunahitaji Waziri aje atoe maelekezo mahsusi ili wananchi waache kugombana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jambo la tatu na la mwisho; ninaiomba sana Serikali na hasa Wizara hii, hebu tujaribu pia ku-develop utalii wa mambo mengine badala ya nature reserve peke yake, badala ya baianuai peke yake. Tanzania tumebarikiwa sana kuwa na masalia ya Watemi na nyumba za Watemi. Ukienda kule Igunga, kuna Mtemi Ng’wanansali wa Igurubi, kuna nyumba yake pale, tunaweza kuitengeneza na watalii wakaja kuona. Ziba pale kuna Mtemi Ntinginya na akina Humbi pale, kuna nyumba yao na makaburi yao, tunaweza kuyafanya; na Mikoa mingi tuna mambo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu ukienda Ulaya haya mambo wameya-develop sana. Kwa mfano Ubelgiji, mimi nimekaa Belgium miaka kumi, kuna mtoto mmoja historia yake alikojolea bomu wakati wa Vita Kuu ya kwanza, sasa yule mtoto ametengenezwa na akawekwa kwenye kila mji anakojoa, watu wanakuja kuangalia na historia inaelezwa pale. Kwa hiyo ni kivutio kikubwa kweli cha utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, basi na sisi mambo haya tuya-develop, yako mengi, kwa mfano, tuna njia ya utumwa sisi, kutoka Bagamoyo mpaka Ujiji tungeweza kui-develop hiyo njia vizuri na wazungu na wenzetu watalii wangependa sana kuja kuipita hiyo njia kuangalia watumwa walivyokuwa wanachukuliwa na sisi tulivyokuwa tunabebwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sisi tumeng’ang’ania zaidi utalii unaohusu wanyama, mimea, milima nakadhalika, hebu twende na huo upande mwingine itatusaidia sana tutaalika watalii wengi zaidi kuliko ilivyo sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi, ahsante sana. (Makofi)