Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Magdalena Hamis Sakaya

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Kaliua

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi nikushukuru kunipa nafasi ili niweze kuchangia hotuba hii muhimu sana kwa uchumi wetu, ambayo ipo mbele yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi niungane pia na Waheshimiwa Wabunge kupongeza kazi nzuri ambayo inafanywa na Wizara, kwa kweli Mheshimiwa Waziri kuna kazi inayofanyika, tunaiona na inaonekana. Pamoja na kazi inayofanyika lakini bado kuna mambo ya msingi sana ambayo ni lazima Wizara iangalie tena kwa jicho la pekee sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye taarifa ya Mheshimiwa Waziri ametuambia kuhusiana na kiwango kikubwa sana cha utowekaji wa misitu, speed ya kutoweka misitu Tanzania ni kubwa sana. Mwaka 2015 na mpaka 2018 tumepoteza almost hekta 469,420; kwa mahesabu ya haraka haraka ambayo nimepiga kwa mwaka mmoja tunapoteza hekta 29,000 za misitu ambayo tayari ipo, wakati huo huo speed ya kupanda miti bado ni ndogo sana. Kwa hiyo, kwenye suala la misitu inayoteketea bado lazima tutafutie solution, kwa mwendo tunaoenda nao bado.

Mheshimiwa Naibu Spika, na leo hili linaloongelewa kwenye vitabu wala huhitaji hata kwenda shule sana, ukiangalia spidi ya kukata misitu inayoendelea na mkaa unavyopelekwa Dar es salaam na magunia ambayo yamejaa kila unakopita yamerundikwa inadhihirisha wazi kwamba hali ya misitu yetu inakwenda kuwa hatarini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninachoomba, naomba Wakala wa Misitu wapewe mamlaka. Leo tunazisifia TANAPA na Ngorongoro kwa sababu ni mamlaka, wanatumia sheria ya kuhifadhi ndiyo maana unaona wanafanya kazi kulikoni hata mamlaka nyingine. Kwa hiyo, ukipewa mamlaka unakuwa na nguvu ya kisheria. Naiomba Serikali ione umuhimu kuifanya TFS waweze kuwa ni mamlaka ili wasimamie kikamilifu matumizi ya rasilimali zote za misitu kwa ukamilifu wake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine, kuna tatizo kubwa sana la ukataji wa miti kwenye mashamba yaliyopandwa Iringa na Njombe, miti ambayo haijakomaa, na kwa lugha ya kule wanasema ni kubakwa kwa miti, ,miti inabakwa kabla ya wakati wake. Hili ni tatizo kubwa sana kwa sababu tunaingiza product za mbao kwenye masoko ambazo hazijakomaa; wananchi hatujui mbao ipi imekomaa na ipi ambayo haijakomaa, tunanunua, unakwenda kujenga nyumba siku mbili/tatu upepo ukija paa lote limeezuliwa, ni kwa sababu tumeruhusu miti inavunwa ambayo haijakomaa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunao wataalam wa misitu, nataka nipate majibu ni kwa nini wataalam wa misitu wanakubali mbao ambayo haijakomaa inaingia sokoni? Pia nijue mkakati wa Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nilikuwa nashangaa, huko nyumba ukienda kuuliza mbao ya Sao Hill gharama yake ipo juu sana, ukienda kwenye mbao nyingine gharama iko chini, nikawa nasema ni kwanini tofauti hii ni kubwa sana? Kumbe tatizo ni kwamba mbao ya Sao Hill inakomaa vizuri, mbao za wananchi kwenye mashamba hazikomai vizuri lakini zote ni product ambazo zinatakiwa ziwe zimekomaa vya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo naomba nijue mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba kwanza ni namna gani wananchi watajua mbao isiyokomaa na iliyokomaa sokoni lakini nini mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba wanatatua tatizo hili ambalo ni kubwa sana ndani ya matumizi ya rasilimali ya misitu na hasa kwa ajili ya ujenzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni kuhusu TANAPA; wengi wamelizungumzia. Kiukweli Serikali isipoangalia, leo tunajivunia wanakuja wageni wataalii mara Waisraeli na Wachina wanakuja kuangalia vivutio vilivyohifadhiwa na havikuhifadhiwa kwa siku moja, imechukua muda kuvihifadhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa leo tusipoenda kimkakati tukaendelea kuweka majukumu mazito kwenye TANAPA wakati huo huo bajeti ya mwaka huu ya TANAPA tumeipunguza kwa asilimia 18, lakini wakati huo tumewaongezea majukumu hifadhi nyingine tano ambazo ni mapori yaliyokuwa yamechoka hayana kazi tena. Tumewapa wayahifadhi, waya-groom mpaka yaweze kuwa ni maeneo ambayo yanatembelewa; watengeneze miundombinu na wawe na watumishi wa kutosha kuhakikisha kwamba hifadhi zile pia zinapeleka watalii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ni lazima ikubali, kwa kuwa TANAPA wamepewa majukumu makubwa, ipunguze zile tozo na angalau lile gawio la asilimia 15 lipungue liende kwenye 10. Lakini TANAPA inafanya kazi kubwa kwelikweli, ukienda kwenye Land Use Plan ya Taifa, protection, miundombinu, ujirani mwema kote huko TANAPA inachangia. Kwa hiyo, kazi inazofanya nje ya kazi zake ni nyingi sana. Kiukweli kuendelea kupunguza bajeti yake na kuendelea kuwapa majukumu na tunategemea kwamba majukumu hayo yaweze kuwa na tija huko tuendako tunaenda kuiua TANAPA kama ambavyo tumeua mashirika mengine ambayo yalikuwepo ndani ya nchi hii miaka ya nyuma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Ngorongoro; Kamati tumewahi kuleta maoni ya kwa muda mrefu sana, kwamba sheria hii iliyotengeneza Ng’orongoro miaka hiyo inawezekana leo ikawa inahitaji maboresho. Leo ukienda kule Ngorongoro wananchi wanalalamika na ni hifadhi pekee nadhani duniani ambapo ni multiple plan land use ambapo wananchi, wanyama na mifugo wapo huko huko, ni kitu kizuri kwelikweli. Kwa nini Serikali haileti Sheria ya Ngorongoro tuweze kuifanyia mabadiliko ili Ngorongoro iweze kuwepo sustainably lakini pia jamii inayoishi kule iweze kuridhika na kuendelea kuishi vizuri na kuendelea kutunza huu utamaduni wa kuweza kuwepo na multiple land use kwenye eneo la Ngorongoro. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni suala la tasnia ya uwindaji wa kitalii. Kwa mwaka 2017 tasnia hii imeyumba kidogo na mpaka sasa hivi nadhani haijasimama vizuri kutokana na kwamba Serikali itaenda kuingiza mfumo wa kugawa vitalu kwa njia ya mnada katikati ya muhula wa uwindaji, matokeo yake vitalu vingi vikarejeshwa Serikalini.

Mheshimiwa Naibu Spika, tafsiri ya vitalu kurejeshwa Serikalini ni kwamba vile vitalu havina ulinzi, hakuna watu wanaovilinda kwa sababu sheria ni kwamba unapewa kitalu kwa ajili ya uwindaji pia unaweka askari kwa ajili ya kulinda rasilimali iliyopo kule. Sasa vile vitalu vyote ambavyo vimerejeshwa havipo salama lakini Serikali inakosa mapato and at the same time wale wanyama kule wanawinda kiholela kwa kuwa hakuna anayetunza.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba Mheshimiwa Waziri atakavyokuja ku-wind leo atuambie amefikia wapi kuhusu mchakato wa kuhakikisha kwamba tasnia hii ya uwindaji wa kitalii inakuwa sustainable, lazima tupate majibu. Tukiendelea ku-dilly-dally kwanza wale wawekezaji wanaondoka lakini pia yale maeneo yanakuwa hayapo salama sana kwa ajili ya kuhakikisha kwamba yanaendelea kuleta kipato lakini pia yaendelee kuwa eneo salama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Kuhusu Suala la Migogoro ya Ardhi Kwenye Maeneo ya Wananchi na Maeneo ya Hifadhi. Hili ni lazima tuliseme kila siku kama wimbo kwa sababu ni kitu ambacho kinagusa jamii ya chini kabisa ya wananchi wetu. Mimi nashukuru kwa mara nyingine Mheshimiwa Rais ameunda tume; na mimi nashukuru kwamba hii tume ina Mawaziri ambao tuna imani nao. Sasa hivi tunaambiwa kwamba wamekamilisha kazi na wanaandaa ripoti, lakini maeneo mengi hawajafika.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ninasema kama Mawaziri hawa wataenda kukaa maofisini na watendaji wakapata taarifa za ofisini, tatizo la migogoro hii halitakwisha, watakuja na ripoti hapa still kule matatizo yataendelea kuwepo. Mimi nawaomba maeneo ambayo hawajafika, wafike wakaangalie haya maingiliano ya maeneo ya hifadhi waone ili watakapokaa mezani kutoa mapendekezo na kuandika ripoti wampelekee Rais kitu ambacho ni reality. Leo unakwenda kukaa na watu wa TAMISEMI wa Wilaya ambapo hao hao ndio wamesajili vijiji ndani ya hifadhi, unategemea kupata nini? Ukienda kukaa na watu wa mkoa ambao na wenyewe pia wameshiriki unategemea kupata nini? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hawatapata uhakika (reality) mpaka waende kwenye maeneo ambayo yana migogoro wakaongee na wale wananchi na wenyewe waone ule muingiliano, wanaweza kukaa chini wakatoa taarifa ambayo ni nzuri na itaweza kusaidia kuondoa migogoro hii ambayo imedumu kwa muda mrefu lakini pia kiukweli inaleta madhara makubwa sana kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni suala la hoteli zetu. Tulikuwa na utaratibu huko nyuma ulianzishwa na nitapenda Mheshimiwa Waziri aje atuambie, ya kuweza ku- grade hoteli zetu. Lazima tuwe na grade ya hoteli zetu zote, tujue five star ikoje, four star, three star mpaka mwisho. Leo unaweza ukaenda kwenye hoteli unaambiwa hii ni hoteli haifanani hata na guest, unavyoenda kwenye hoteli ujue hii ni hoteli, hii ni lodge na hii ni guest house; lakini leo mtu anajiandikia tu, chumba cha ajabu hakina hadhi anakwambia hii ni lodge.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba Serikali ituambie utaratibu wa kufanya grading ya hoteli zetu zote, leo sasa tunaanza kupata wageni wengi, mgeni anaweza akaja akaingia kwenye chumba ambacho alijua ni hoteli, mazingira yale ya hoteli tu yatamfanya next time asije tena au picha anayopeleka kule ikawa siyo nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba zoezi la ku-grade hoteli zetu maeneo yote lilianzwa vizuri sana na Mheshimiwa Shamsi nadhani kipindi hicho, mpaka leo hatujui limefikia wapi. Naomba sana hoteli zetu zote zipatiwe grading kwa kuwa ni sehemu moja wapo ya utalii. Mgeni anavyokuja ukimwambia hii ni lodge ajue ni lodge, guest ama five star hotel. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa muda, yangu ni hayo machache, ahsante sana. (Makofi)