Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Madini

Hon. Sebastian Simon Kapufi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mpanda Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Madini

MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru, na mimi nimpongeze Waziri na Naibu Waziri kwa kazi nzuri wanayofanya.

Mheshimiwa Spika, na mimi pia nakumbuka hiyo tarehe 22 na 23 Januari nilikuwepo pale Dar es Salaam wakati akiwepo Mheshimiwa Rais akikaa na wachimbaji wadogo. Kati ya mambo aliyoyaongea Mheshimiwa Rais ilikuwa ni pamoja na haya yafuatayo; Aliwaomba watendaji akiwepo Waziri kwamba yeye kama amefunga mlango wao waangalie hata namna ya kufungua dirisha. Alipolisema hilo alikuwa anamaanisha haiwezekani yeye Mheshimiwa Rais akafanya mambo yote, kuna baadhi ya mambo wamsaidie, watendaji hawa.

Mheshimiwa Spika, nikilisema hilo namaanisha mimi ninafsi kwanza nikiri mbele yako ni moja kati ya wachimbaji wadogo wa madini, nchimba madini ya dhahabu. Limekuwepo tatizo moja la kitu wanaita makinikia. Naomba nikiri, katika mgodi wangu pale Mpanga tunayo makinikia ya kutosha ambapo naamini Serikali hii ilikuwa na uwezo wa kupata kiwango kikubwa cha fedha. Makinikia yale yamekuwepo kutokana na sheria ya zamani kabla ya sheri ampya kupitishwa hapa Bungeni. Sasa anapokuja kuadhibiwa mtu kwa sheria ya zamani ambayo ilimpa nafasi ya kufanyia hiyo kazi nilikuwa naomba Mheshimiwa Waziri utusaidie katika hili na najua Mheshimiwa Waziri nimekuwa nikipita kwako kwa muda mwingi nikikueleza kuhusiana na suala hili.

Mheshimiwa Spika, katika hili niseme, katika mgodi kwa mfano huu wa Katavi-Kapufi, kuna makinikia ya kutosha ambayo hayo, mbali ya makinikia hayo, kuna ajira za Watanzania wenzangu, zaidi ya Watanzania 400, wameajiriwa pale, lakini suala ambalo linatukabili sasa hivi ni hiyo kuzuia kuyasafirisha makinikia haya ambayo yalikuwepo kutokana na sheria ya zamani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hilo namwomba sana Mheshimiwa Waziri, atusaidie na hata pale ambapo anaonyeshwa kwamba mchango wa dhahabu ni asilimia 86.07, bado mchango wa dhahabu ungeweza kuwa mkubwa zaidi. Nikilisema hili, niendelee kusema, kwa wale wote ambao hata wana makinikia ya kopa ya sheria ya zamani, ndiyo maana Mheshimiwa Rais alisema hivi, kiwepo kipindi cha mpito, wakati ambapo watu wanajipanga kwa ajili ya kuja na smelter na refinery. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, siyo suala la mara moja, ni uwekezaji mwingine mkubwa, kwa hiyo, kama kuna watu wamefanya uwekezaji mkubwa, wengine wakishirikiana na watu wa nchi za nje, leo unapomwambia ashughulikie suala la smelter na refinery, hakuna mtu anakataa hilo, lakini siyo suala la usiku mmoja, it takes time, vipi watu hao wasipewe kipindi hiki cha mpito? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nitoke hapo, nije katika suala lingine, ni kweli tunazungumzia wachimbaji wadogo, lakini naomba sana jitihada ambazo zinaendelea kufanywa na Wizara, kuendeleza tafiti nyingine na kuhakikisha tunaendelea kujenga uchimbaji wa kati na uchimbaji mkubwa pia. Kwa sababu mchimbaji mdogo, ukimfanyia mazingira mazuri, atakua, akishakua anaweza kwenda kuwa mchimbaji wa kati na baadaye akaja kuwa mchimbaji mkubwa, kwa hiyo, maeneo yote hayo na bila kuacha tafiti. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la mwisho, madini yanakuwa na thamani ukiyatoa ardhini, lakini wakati yakiwa bado yako ardhini, ni mwamba kama mwamba mwingine wowote ule. Kwa hiyo, Watanzania kwa ujumla wake, Baba wa Taifa alifanya kazi nzuri ya kusema kwamba, hatuchimbi mpaka Watanzania watakapokuwa tayari. Wasiwasi wangu, tusipojitahidi tukachimba, kwa Baraka hizi alizotupa Mwenyezi Mungu, tutajisifu tuna dhahabu tuna nini, lakini kama bado iko chini ya ardhi, haina thamani, thamani yake ni pale itakapotoka ardhini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niseme, kwa nini tusi-take advantage ya madini haya tuliyonayo kuhakikisha yanachimbwa kwa kadri tutakavyoweza, halafu tunakwenda kwenye uwekezaji mwingine tofauti. Nchi zenye mafuta na gesi, wanahakikisha kwa sababu ina under go law of diminishing return, madini yanakwisha. Kwa hiyo, kabla ya hayajakwisha, tuhakikishe yametusaidia katika maeneo mengine, huo ndiyo ushauri wangu kwa Serikali yangu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru na naunga mkono hoja. (Makofi)