Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Madini

Hon. John Wegesa Heche

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Tarime Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Madini

MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hi ya kuchangia. Kwanza napenda nimpongeze sana Mheshimiwa Kapufi, nimemsikiliza vizuri sana, amezungumza kwa kweli mambo mazuri kwa ajili ya nchi yetu na nilipokuwa namsikiliza nilifikiri anarejea Sera ya CHADEMA ya Julai, mwaka 2018 inayozungumza kuhusu madini.

Mheshimiwa Spika, wenzetu kule Norway wanapochimba gesi yao na mambo ya madini, wameweka benki, wanaweka akiba kwa ajili ya vizazi vijavyo na sisi kuendelea kuwa na kauli hizi kwamba madini yabaki chini hayaozi hayafanyi nini, siafiki utaratibu huo, ninachokubaliana nacho, ni kwamba, madini haya yanayochimbwa, yachimbwe vizuri na fedha zinazotokana na madini haya zitunzwe kwa ajili ya vizazi vijavyo.

Mheshimiwa Spika, sasa hivi almasi duniani, 40% ya almasi inayovaliwa duniani ni almasi ya kutengenezwa. Sasa tunapokwenda kuendelea kusema sijui tuna almasi, wao watu wanaonunua haya madude baadaye wakija waka, hasa haya ya mapambo, wanaweza kuja kuyabadilisha wakaanza kutumia vitu vingine ukabaki na tanzanite na almasi ambazo hazina thamani yoyote. Kwa hiyo, nafikiri tuangalie lakini tuna-insist kwamba, kila tunapotoa rasilimali hizi zibaki kwa ajili ya vizazi vingine, tusitumie sisi wenyewe na tukamaliza.

Mheshimiwa Spika, suala la pili ambalo nahitaji maelezo kutoka kwa Mheshimiwa Waziri, wachimbaji wadogo, wanalipia environmental impact assessment, milioni tatu mpaka milioni sita, lakini kuna mtu wa mazingira yuko halmashauri, kazi yake ni nini yule mtu wa halmashauri pale, mpaka hawa watu wanalipia hizo fedha. Mbona mtu wa kilimo tunapokwenda kuomba consults hatulipii na tusipofanya environmental impact assessment, ambayo nakubali ifanyike, unapigwa faini. Kwa hiyo, nataka kujua kwa nini wachimbaji wadogo wanalipia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la tatu, sumu iliyotiririka kwenye Mgodi wa Nyamongo, nimeizungumza vizuri kwenye hotuba na ningependa hotuba yangu nzima Mheshimiwa Waziri ajitahidi kuisoma na aijibu. Kuanzia mwaka 2017, watu wamekufa, mali za watu zimepotea, Mto Tigite uliharibika na huu mto unatiririka mpaka Mto Mara, pote kwenye maeneo karibu ya kata sita. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, miaka yote hii, tumekuwa tukiambia Serikali, kwa ushahidi, kwamba kuna watu wanababuka ngozi kwa kuoga maji, viumbe vinakufa, nyasi zinakauka, wakati wote huo Serikali ilikuwa ikisema, hakuna kitu, hakuna kitu, hakuna kitu. Mheshimiwa Waziri alikuja pale akaona maji yanavyotiririshwa, eneo la Kwinyunyi, Kwimange na kule Kegonga, kitongoji kizima watu wamehama, wameacha maeneo yao, hayazalishi chochote kwenye kilimo. Eneo ambalo ulikuwa unalima unapata labda gunia 100, leo ukilima hupati hata gunia 10 kutokana na madini, tembo kuathiri lile eneo.

Mheshimiwa Spika, asa nataka, Mheshimiwa Waziri, kwanza, Serikali wamepiga faini pale, hivi wao wameathirika nini? Kwa sababu walioathirika ni wananchi wanaoishi yale maeneo. Tunataka hizo fedha walizopiga faini, ziende kulipa wananchi ambao wameathirika, wananchi wa Tarime ambao wamekunywa maji ya sumu, ndiyo wakalipwe fidia. Ng’ombe waliopotea, watu waliokufa na tunataka ifanyie assessment mpya, kujua madhara ni kiasi gani na wale wananchi wapate fidia inayostahiki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Waziri ni rafiki yangu, nimekuwa nikimshauri kufuata sheria, Sera ya Madini ya Mwaka 2009, inasema, unapohamisha watu kutoka eneo la mgodi, unawalipa fidia, compensation, unawajengea makazi, yaani unafanya reallocation na unawalipa gharama za kuwahamisha. Hakuna, watu wote waliolipwa fidia Tarime, imekuwa ni kidogo na mgodi umekuwa ukisema, ooh ni kubwa sana, lakini hakuna mtu ambaye amewahi kufanyiwa resettlement kwa kujengewa nyumba na kupewa makazi, watu wachache tu waliofanyiwa resettlement, halafu hawakulipwa fidia, wakajengewa vinyumba tu, Waziri aliviona na Kamati ya Waziri Muhongo ilisema, vibomolewe na vijengwe upya, ukipiga teke kanadondoka. Sasa tunataka kujua ni kwa nini, hawa watu hawafanyi hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la Mchuchuma na Liganga, amelizungumza vizuri sana ndugu yangu hapa Neema. Kampuni ya Hongda Sichuan, mwaka 2019 ilisaini mkataba na Serikali na mkataba wa zaidi ya dola bilioni tatu, ambazo ni trilioni 6.8, ambazo zilikuwa zimekuja kufanyiwa investment hapa, Watanzania zaidi ya elfu tano walikuwa wanakwenda kupata ajira za moja kwa moja kwenye huu mgodi. Mpaka sasa imekuwa ni kizungumkuti, Serikali ime-delay fedha hizi zote ambazo zingekuja kusaidia uchumi wa nchi yetu, nataka Waziri atuambie, ni kwa nini kumekuwa na delay tangu mkataba huu usainiwe na Wachina na tukaunda kampuni. Kwa nini mpaka sasa investment hii haija-take off! Tunataka kujua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, service levy; makampuni yanayofanya kazi pale kwenye mgodi na mgodi wenyewe, umekuwa ukilipa 0.03% ya service levy kwenye halmashauri, lakini kampuni ambazo zinalipwa fedha nyingi sana ni kampuni za insurance. Insurance wanachukua fedha nyingi, wana-insure kuanzia dhahabu, mitambo yote mbayo ni ya gharama kubwa na migodi yenyewe, lakini kampuni zote za insurance, hazilipi hata senti moja ya service levy kwenye maeneo ambayo halmashauri zinatoka.

Mheshimiwa Spika, sasa nataka Waziri aje atuambie, kuna vikampuni vya Watanzania, mtu anafanya kazi ya kujenga kadaraja pale kwenye mgodi, kazi ya milioni 100, analipa 0.03% na siku hizi halmashauri kwa sababu hazina mapato, hata kwenye maduka tu, haya ya wananchi, mtu ana kioski cha milioni mbili, anafukuziwa na 0.03% ya service levy. Ni kwa nini makampuni makubwa ya insurance ambayo yanachukua matrilioni ya fedha kutoka Tanzania, hayalipi service levy kwenye migodi! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la mwisho ni kuhusu smelter. Kwa nia njema kabisa sisi tulizungumza hapa wakati sakata la makenikia linakuja mnatuambia mtatuletea Noah, na Watanzania hawajasahau na tunataka mjibu Noah ziko wapi? Kwa sababu tuliambiwa mambo mengi hapa tukaambiwa na smelter inajengwa, mwaka 2017 hakuna smelter. Amezungumza Mheshimiwa Kafupi pale, watu wanazidi kupata hasara; 2018 hakuna smelter, 2019 hakuna dalili, 2020 hakuna dalili; smelter mtajenga lini hapa? Kwa sababu tuliambiwa hapa tumeibiwa sana makenikia haziendi na sisi tunasema thank you very much, now we want a smelter here, tunataka smelter na watu waanze kufanya uchenjuaji wa madini hayo hapa tuone faida kwenye nchi yetu hii. Kwa sababu hizi kauli za kisiasa ambazo zimekuwa zikifanyika kila siku kufanya kuwahadaa Watanzania sisi ni wazalendo kuliko watu waliokuwepo sijui na nini, tunataka sasa uzalendo huo uonekane kwa vitendo, na tunataka wananchi waanze kunufaika na madini hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na nazungumza hivi kwa sababu watu wanaotoka kwenye maeneo ya madini wameathirika sana. Jana tulikuwa kwenye semina fulani hivi na mtu mmoja akaanza kusema pale, sitaki kumtaja, ni Mbunge na alikuwa Waziri hapa anasema eti tuambiwe benchmark ya faida ni nini, kama hatujanufaika tumepata sijui kodi ya trilioni moja. Hivi mzee Ryoba Ilondo ambaye ng’ombe wake zaidi ya 500 wamekufa unamwambia mgodi una faida gani kwake?

Kwa sababu yeye alizoea ng’ombe wale asubuhi anafunga kwenye jembe anakwenda kulima pale Matongo, anavuna, anakamua maziwa watoto wake wanakula; maisha yanaendelea. Alikuwa kwenye nyumba ambazo zimeezekwa kwa majani fine, lakini yeye maisha yake yalikuwa yanaendelea, hawajawahi kulala njaa; lakini leo ng’ombe wake wamekufa analala njaa; unamwambiaje mgodi una ufaida, na madini haya yanafaida? kwa hiyo Mheshimiwa Waziri hayo ni mambo serious tunaomba majibu kwa ajili ya watanzania,ahsante sana.(Makofi)