Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati

Hon. Magdalena Hamis Sakaya

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Kaliua

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati

MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia hotuba ambayo ipo mbele yetu; na nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi ya kuweza kusimama tena kwenye Bunge lako Tukufu. Naomba pia niungane na Wabunge kupongeza kazi ya REA inayofanyika maeneo mbalimbali ya kuweza kuongeza juhudi za umeme hapa Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati Mheshimiwa Waziri anazindua REA III mwaka 2017 kwanza alisema kwamba itaenda speed, alisema hata kwa wakandarasi aliokuwa anawapa maagizo; na pia kwamba ile REA III itakwenda mpaka kwenye vitongoji tofauti na REA awamu ya kwanza na REA awamu ya pili. REA hii awamu ya tatu kwanza inakwenda taratibu sana; na ingawa Mheshimiwa Waziri anatembelea maeneo mbalimbali lakini akishafika kule akitoka bado speed inakwenda slow vilevile.

Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo langu la Kaliua tulipewa vijiji saba tu REA III, lakini mpaka napoongea huu ni mwaka wa pili kilichowaka umeme ni kijiji kimoja tu na imewekwa transfoma moja tu; vijiji vingine vitatu wamepeleka nguzo nyaya bado na vijiji vingine 3 bado kabisa hawajafika. Sasa kwa speed hii tunayokwenda nayo Mheshimiwa Waziri itachukua miaka mingapi hata kwa hivyo saba tu kukamilika? Achana na vingine ambavyo bado.

Mheshimiwa Naibu Spika, speed ya REA bado ni ndogo. Fedha hii ya REA ni ring fenced, iko pale, haifanyi kazi nyingine, lakini speed imekuwa ni ndogo sana kila siku kuna vikwazo. Kwanza walikuwa wanasema ni nguzo, nguzo zikija wanasema ni nyaya, nyaya zikija wanasema ni tranfoma, kwa hiyo kila siku ni matatizo. Namwomba Mheshimiwa Waziri, speed ile ambayo mlikuwa mmeanza nayo mara ya mwanzo kushinikiza wakandarasi wafanye kazi kwa muda wafuatiliwe wafanye kazi kwa muda. Mwaka jana wakasema ni mvua nyingi mwaka huu mvua haziko nyingi. Kwa kweli tunasikitika kwamba speed ya REA ni ndogo pamoja na kuwa fedha ya REA iko ring fenced kazi yake ni hiyo moja tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili, ndani ya Wilaya ya Kaliua umeme umekuwa ni kizungumkuti, imekuwa ni kumulimuli. Mheshimiwa Waziri kila siku ya kwa Mungu, hata leo, tunakosa umeme masa sita mpaka nane, kila siku. Kwa hiyo kwa maana nyingine ule uwepo wa umeme hauonekani, maana umeme ukiwepo usaidie jamii kunufaika, mashine zifanye kazi, welding wafanye kazi, saluni zifanye kazi, vile viwanda vidogovidogo vifanye kazi. Sasa kama wanafunga kwa muda wa masaa nane kwa siku hauna faida.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri tulikuwa na shida ya nguzo kwenye maeneo ambayo ni mbuga, ukaagiza tangu mwaka jana zibadilishwe; mpaka leo shida ya Kaliua katika umeme iko pale pale. Hivi navyoongea leo kuanzia saa moja asubuhi mpaka saa nane walikuwa hawana umeme; na huu ndio utaratibu, hiyo ndiyo historia ya Kaliua. Mheshimiwa Waziri umeme ni maendeleo, umeme ni uchumi; leo uchumi wetu hauwezi kupanda kama vijana kwa masaa nane kwa siku hawafanyi kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni suala la kujenga substation. Kwenye bajeti ya mwaka jana Mheshimiwa Waziri alituambia kwamba vinajengwa vituo viwili kati ya Kaliua na Urambo na Kaliua na Uvinza; na nina imani kabisa inawezekana kujenga hiyo substation ukaweza kusaidia angalau umeme labda wakapokelea pale kwenye hiyo ki- substation ukawa umeme wa uhakika. Naomba, vile vituo Mheshimiwa Waziri havikujengwa kwenye bajeti ya mwaka jana, mwaka huu unapokuja ku-windup utuambie, je, mwaka huu vitajengwa? Ili angalau tuweze kuondokana na shida ya umeme. Leo umeme ni uchumi lakini kwa mwendo tunaoenda nao Kaliua, maeneo ya Urambo na maeneo mengine bado hatuoni faida kubwa sana kwa sababu tunaona nguzo na nyaya tu lakini umeme hautumiki kama inavyotakiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala linguine, Mheshimiwa Waziri amekuwa anatamka hapa Bungeni, nje ya Bunge na hata ndani ya Bunge kwamba pale REA inapoishia TANESCO ipeleke umeme kwa shilingi 27,000 vijijini, lakini hilo halitekelezwi, sasa sielewi kwamba maagizo haya hawajapewa TANESCO? Wilaya ya Kaliua tuna zaidi ya watu 160 wameomba wafungiwe umeme, wamefanya wiring hawapelekewi umeme na shilingi 27,000 wanayo. Hiki kingine ambacho TANESCO wanasema kwamba lazima kuwepo na nguzo, Mheshimiwa Waziri inakuwa ni double standard.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama REA imepeleka umeme mpaka maeneo fulani halafu kuanzia pale mwananchi anaambiwa alipe nguzo 338,000, kama ni nguzo mbili ni 480,000, kama ni nguzo tatu ni 900,000 ilhali mwenzake hapa jirani tu kafungiwa umeme kwa shilingi 27,000; hiyo ni double standard. Naomba Mheshimiwa Waziri utuhakikishie unapokuja ku-windup kesho hapa, utuambie namna gani wananchi wa vijijiini maeneo ambapo REA imeishia wanaweza kupata umeme kwa gharama ile ile unayosema kila siku, 27,000, kwa sababu ni haki ya kila mmoja kuweza kupata umeme kwa bei ambayo ni standard na ambayo itakuwa ni haki kwa wengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, limekuwepo tatizo lingine kwenye uwekezaji kwenye sekta ya mafuta. Tumekuwa tunalalamika kwamba kuna vikwazo vingi vingi kwenye masuala ya uwekezaji hapa Tanzania kwenye maeneo mbalimbali. Hata kwenye sekta ya mafuta pia lipo tatizo la uwekezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, unapotaka kuwekeza kwenye sekta ya mafuta aidha kujenga kituo cha mafuta kuna milolongo mingi sana ya kupitia, pia kuna vibali vingi sana vya kupitia. Ukianza na NEMC wanachukua mwaka, ukienda halmashauri unaomba kibali miezi sita, ukitoka tena ukienda EWURA miezi 6, useme uende OSHA miezi sita. Miaka miwili na nusu unahangaika tu na kibali huujakipata uanze kujenga kwa mwendo huu mwekezaji yeyote aliyejiandaa ataweza? Hawezi kwa hiyo tunaomba kuwepo na one stop center, kama ni masuala yafanyike kwa pamoja ili mtu anapokuwa na lengo la kuwekeza aweze kuwekeza kwa kirahisi kwa sababu uwekezaji ndio uchumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine pia ambalo ni tatizo ni faini kubwa sana wanazopigwa watu wa mafuta. Sekta hii unakuta kwamba wale ambao ni wakubwa ndio wanaoweza kuwekeza tu, wale wadogo wanaojichomoza hawawezi; kwa sababu mtu mkubwa ana mitaji mikubwa, anaweza akawa anasubiri vibali huku anaendelea na mambo mengine; lakini kwa yule ambaye anayechipukia ambao ndio tunaowalenga, Watanzania wa chini wenye uwezo mdogo, waweze kunyanyuka, wanakwama.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tunaomba; wakati mwingine kuna faini kubwa sana zinapigwa kiasi kwamba mtu ana mtaji wa milioni 10, anapigwa faini milioni 20, umemuulia pale pale na bado unamdai. Faini tulizokubali ziwepo pale mtu anapofanya kosa ziendane na hali halisi kwa sababu tunapenda hawa wenzetu ambao ni wa chini pia waweze kunyanyuka kwa ajili ya kuhakikisha kwamba wanachangia uchumi na ni sehemu ya maendelo ya taifa lao.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni hizi criteria za kampuni za mafuta au watu wanaofanya biashara za mafuta. Kumekuwepo na criteria mbalimbali, kuna watu wanaitwa CODO, kuna wengine wanaitwa DODO, na wengine ni wale wa chini kabisa. Unakuta mtu ambaye anaagiza mafuta kwa jumla na yeye pia anaruhusiwa tena kwenda kuuza kwa rejereja. Kwa hiyo wale wanaoagiza mafuta kutoka nje wanakuja wanauziana kampuni madogo ndogondogo nao pia wanaruhusiwa kufungua vituo vidogo vya mafuta wanauza reje reja; kwa hiyo ile fair competition inakosekana. Wakati huo umemuuzia mtu mdogo mdogo reje reja pembeni yake wewe unakwenda kufungua tena kituo kwa bei ya reja reja. Kwa hiyo wewe una faida kwa sababu kwanza ulishauza kwa bei jumla, pili unawezo wa kupunguza bei kwa sababi tayari unapata faida mara mbili. Mheshimiwa Waziri, kwa nini Wizara inaruhusu haya? Matokeo yake wale ambao ni wadogo hawawezi ku-compete kwenye biashara, mara nyingi unakuta wameondoka.

Mheshimiwa Naibu Spika, na ndiyo maana ukisoma kwenye kitabu cha Mheshimiwa Waziri unakuta kuna mahali kuna vituo 73 baada ya mwaka vimefungwa vitano kwa sababu wanaofunga ni wale wadogo ambao wanashindwa ku-compete na biashara. Tunaomba hizi criteria ziheshimiwe; Kama mtu anaagiza mafuta nje; kama yeye ni mtu mkubwa na ana uwezo wa kuagiza mafuta nje abaki kuagiza mafuta nje. Mheshimiwa Waziri wale ambao ni CODO wanaoagiza mafuta nje akishamuuzia mwenzake na ile criteria nyingine waweze kuhakikisha kwamba wao wanawaachia kwenye sekta ile tena wauze. Wale wa chini kabisa kule ambao ndio DODO waweze kuwa na uwezo wa kuweza kuuza pia…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa kengele ya pili imeshagonga, ahsante sana.

MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana ahsante.