Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati

Hon. Rashid Mohamed Chuachua

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Masasi Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati

MHE. RASHID M. CHUACHUA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na mimi nipate fursa ya kusema kidogo kwa ajili ya kuchangia Hotuba ya Waziri katika Wizara hii ya Nishati. Nianze na kumpngeza sana Mheshimiwa Dkt. Kalemani; ni mchapakazi kwelikweli yeye na Naibu Waziri wake wanafanya kazi usiku na mchana kuzunguka Tanzania kwenda kutatua matatizo ya wananchi wetu wanyonge.

Mheshimiwa Naibu Spika, niipongeze Wizara kwa jumla kwa kazi kubwa wanayofanya, na niwapongeze sana kwa sababu ukisoma hotuba yao ukurasa wa 63 wanaonyesha wazi kwamba Tanzania kwa sasa ni nchi ya kwanza katika Afrika ya Mashariki katika kusambaza umeme vijijini; hili ni jambo kubwa sana, hatuwezi kukaa bila ya kuwapongeza. Pamoja na pongezi hizo ningependa nimfahamishe Mheshimiwa Waziri kwamba katika mikoa anayoishughulikia kwenda kusambaza umeme hafahamu usiku na mchana anapotembea kwamba umeme katika Mkoa wa Mtwara umesambazwa katika vijiji vichache sana ukilinganisha na mikoa mingine. Huu ni ujumbe ambao Mheshimiwa Waziri anatakiwa awe anatembea nao wakati wote ili atuangalie kwa macho mawili katika Mkoa wa Mtwara namna ambavyo vijiji vichache sana vimepata umeme wa REA.

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri, katika ziara yake aliyofanya kwenye Mkoa wa Mtwara amefika kwenye Wilaya ya Masasi na amefika kwenye jimbo langu. Mheshimiwa Waziri amewasha umeme katika Kijiji cha Mombaka katika Kata ya Mombaka pia kwa niaba ya wananchi amezungumza mambo mengi na matarajio makubwa ya kuhakikisha kwamba wananchi wanapata huduma ya umeme.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri umetoa maelekezo ambayo nakuomba sasa uendelee kuyasimamia. Umetoa maelekezo kwamba umeme utapatikana kwa shilingi 27,500, uwe unasambazwa kwa njia ya REA au unasambazwa na TANESCO; naomba hili pia ulisisitize sana katika Bunge lako. Pia umetoa maelekezo kwamba wananchi wa Kata ya Sululu katika Kijiji cha Sululu washushiwe umeme, maelekezo haya naomba uendelee kuyasimamia.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia Waziri ametoa maelekezo katika Kata ya Chanikanguo, wananchi wa Kijiji cha Namakongwa wapelekewe umeme, aendelee kuyasimamia maelekezo hayo. Pia Mheshimiwa Waziri ametoa maelekezo wananchi wa Kata ya Mombaka, Kijiji cha Namikunda A na Namikunda B wapewe umeme, maelekezo hayo naomba Waziri aendelee kuyasimamia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo naomba nimwambie Mheshimiwa Waziri kwamba, katika Halmashauri yangu ya Mji wa Masasi ambayo ina vijiji takribani 31 na ina mitaa zaidi ya 48, ukijumlisha tuna maeneo mengi lakini zaidi ya maeneo 40 ukijumlisha na vijiji 20 hatujapata kabisa umeme na zipo Kata ambazo hazijapati umeme hata kijiji kimoja. Sasa hivi kuna mkandarasi anaendelea kufanya kazi lakini ana vijiji sita (6) tu, hii inaonesha wazi kwamba kasi ya kusambaza umeme katika Jimbo langu hairidhishi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitoe ushauri; kwanza Wizara wanapopanga mipango yao wanaipanga kwa kuzingatia Tawala za Kiwilaya jambo ambalo wanatakiwa waende mbele zaidi. Wanatakiwa watambue kwamba wanapochukua vijiji kwenye wilaya, ndani yake kuna halmashauri na ndani yake kuna majimbo; kwa hivyo basi, wanapofanya mipango yao waende mbele zaidi wasiishie kwenye Wilaya kwa kuchagua vijiji, wanaacha tawala nyingine zenye uwakilishi. Kuna majimbo ndani ya kila wilaya lakini kuna halmashari, ili kuweza kugawa hizo rasilimali sawasawa wasiishie kwenye wilaya peke yake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)