Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati

Hon. Athumani Almas Maige

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tabora Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati

MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kuniruhusu nichangie hoja hii ya Wizara ya Nishati iliyoko mezani kwetu sasa hivi. Kwanza natoa shukrani sana kwa Wizara hii na watendaji wa Wizara, Mheshimiwa Waziri Kalemani, Mheshimiwa Mgalu na Mheshimiwa Mwinyimvua kwa kazi nzuri ambayo mnaifanya katika kazi kubwa ya kueneza umeme na kuondoa blanketi la giza katika nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, Wizara hii imeondoa mgawo ambao ulikuwa tatizo kubwa sana miaka iliyopita na kwa kweli, wanastahili sifa kubwa, lakini pia nimshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, kwa kuthubutu kujenga Kituo Kikubwa cha Umeme pale Mto Rufiji. Suala hili litatatua matatizo yote na itakuwa mfano katika nchi za Afrika Mashariki, nchi yetu itakuwa na umeme wa kutosha kwa hiyo, kwa uwekezaji wa viwanda na kukidhi haja ya kuwa na siasa ya viwanda mwaka 2025 na kuwa siasa ya nchi ya kati kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wameongelea Wabunge wengu kuhusu suala hili la kinu cha umeme huko Rufiji, leo nijikite katika kituo katika Mradi wa REA. mradi wa REA ambao Wizara hii inausimamia ni kichocheo kikubwa sana cha maendeleo vijijini, laki I mradi huu hauendi vizuri, mradi huu sasa umekuwa ni tatizo la Waziri, Waziri amekuja kwangu ameubeba mradi huu kama wa kwake mara tatu, lakini akiondoka Mheshimiwa Waziri huyu namshukuru sana, wakandarasi wanalala. Hatuoni maendeleo ya mradi huu vijijini kwetu, sehemu kubwa ya vijiji vyangu vyote havina umeme na sehemu ndogo iliyotiwa umeme haujawashwa.

Mheshimiwa Spika, pamoja na nguvu za Mheshimiwa Waziri kuja kwetu, lakini wakandarasi wanamuangusha na ningependa atakapokuja Mheshimiwa Waziri kufanya majumuisho aje anieleze katika Jimbo la Tabora Kaskazini au Wilaya ya Uyui vijiji gani vina umeme au vina mpango wa kuviwekea umeme kwa sabbu, imekuwa kero tunausikia umeme wa REA kwa wenzetu sisi kwetu hatuuoni umeme huu, hata nguzo haziji. Nimeshaongea na mkandarasi ananiambia tatizo kubwa ni nguzo, lakini nguzo zimeshapatikana, tatizo ni nini katika kuendeleza mradi wa umeme katika eneo langu?

Mheshimiwa Spika, wananchi wanalalamika sana, wanafurahi wanapomuona Mheshimiwa Dkt. Kalemani amekuja, tunamshangilia, karibu tumpe na mke na mbuzi tumpe, akiondoka umeme unapotea. Tunaomba Mheshimiwa Dkt. Kalemani utakapokuja kuongelea mwisho wa majumuisho yako utuambie Umeme wa REA katika Wilaya ya Uyui na hasa Jimbo la Tabora Kaskazini mpango ukoje? Mbona hatuoni unaendelea?

Mheshimiwa Spika, naipongeza sana Serikali yetu ina mipango mizuri na kama ilivyoweka kipaumbele katika kitabu hiki cha bajeti. Mipango yote ikikamilika nchi hii itakuwa mfano mkubwa wa kuwa na kiasi kikubwa cha umeme nchini, lakini pia tutapata faida kubwa kuuza umeme huu nchi za nje, jirani zetu, lakini vilevile sehemu kubwa ya umeme huu utachochea maendeleo ya viwanda ambapo Serikali itapata mapato, lakini utaleta maendeleo kwa wananchi wote.

Mheshimiwa Spika, sikuwa na mambo mengi zaidi ya malalamiko hayo ya REA, lakini kuipongeza Serikali hii ya Awamu ya Tano kwa mpango mzuri wa kuleta umeme katika nchi yetu. Ahsante sana. (Makofi)