Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati

Hon. Abdallah Ally Mtolea

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Temeke

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati

MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kuniona, na nianze kwa kuunga mkono hoja, lakini hata hivyo na mimi nisijifanye kuwa mpofu wa kutoona kazi nzuri inayofanywa na Mheshimiwa Waziri na Naibu wake, pamoja na timu nzima ya Wizara hii ya kuhakikisha wanaitoa Tanzania gizani na kuiweka kwenye mwanga safi wa umeme, tena umeme ulio nafuu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Pamoja na kazi nzuri inayofanywa na Wizara na Serikali kwa ujumla, changamoto huwa haziishi, na kwa dakika hizi chache nilipenda niwasilishe changamoto ya kukatika katika kwa umeme katika Jiji la Dar Es Salaam.

Mheshimiwa Spika, imekuwa ni kero kubwa hata baada ya ile ya migao ya kawaida kumalizika, migao ile ya umeme tuliyoizoea miaka ya nyuma, bado Dar Es Salaam kumekuwa na tatizo la kukatika katika kwa umeme. Ni ngumu sana ukae siku nne mfululizo bila kusikia umeme umekatika. Niliwahi kuuliza maswali hapa mara kadhaa, Mheshimiwa Waziri mwanzo alisema kwamba kwa kesi ya Temeke wanajenga substation nyingine Mbagala na Kurasini ambazo zitaondoa tatizo hili. Hata hivyo, Substation ya Mbagala ilimalizika na ndani ya mwezi mmoja tu ikawa tayari imeshazidiwa. Sasa hivi ukiuliza wanasema kwamba tunasubiri Substation ya Kurasini ambayo ilikuwa imelenga kusaidia watu wa Kurasini na watu wa Kigamboni; sasa maana yake ni kwamba bado hatujapata dawa ya kulitatua tatizo hili, na Dar Es Salaam ndilo soko kubwa la umeme ambao TANESCO wanaouza.

Mheshimiwa Spika, utagundua kwamba sasa hivi kuna megawatt 600 kati ya megawatt 1,600 zipo Dar Es Salaam. Sasa kama watumiaji wenyewe bado wanaendelea ku-experience kukatikakatika kwa umeme maana yake kuna tatizo la msingi ambalo ni lazima Wizara ije na mpango mzuri wa kuhakikisha kwamba inakwenda kulitibu. Ukipiga simu kwenye vituo hivyo vya TANESCO wanakwambia kwamba eneo hilo umeme unakatikakatika kwa sababu Transformer imezidiwa, huko kwa sababu kuna nguzo imedondoka; tafsiri yake ni nini? Ama hatujui tuna idadi gani ya wateja wanaohitaji umeme Dar es Salaam na je, ongezeko la wateja katika Jiji la Dar es Salaam ni wangapi kwa mwaka? Ili tunapoweka Transformer iweze angalau kuhimili ongezeko hilo la wateja angalau kwa miaka miwili mitatu; sasa badala yake kila kitu kimezidiwa.

Mheshimiwa Spika, lakini uchakavu wa hizo nguzo na miundombinu yote ya umeme katika Jiji la Dar Es Salaam ni tatizo. Kwa hiyo ni vizuri Wizara wakati inafanya kazi nzuri ya kuongeza umeme na kusambaza katika mikoa mingine pia iwe na mpango wa kuhakikisha kwamba itanarabati miundombinu ya kusambazia umeme kwenda kwa wateja katika Jiji la Dar Es Salaam, ili wateja wa Dar Es Salaam waiingizie fedha nyingi TANESCO; kwa sababu kwa uwekezaji huu mkubwa ambao Wizara na Serikali unaifanya ni lazima TANESCO ifanye kazi kibiashara, kuuza umeme kibiashara, ili ipate faida kwa sababu hatimaye mtakuwa na jukumu la kuilea hiyo miundombinu yote ambayo leo inajengwa.

Mheshimiwa Spika, sasa msipofanya kazi kibiashara na mkatengeneza faida, mkaliachia soko lenu liwe linapoteza mapato maana yake na ninyi pia mnapoteza; kwa sababu umeme unapokatika Dar Es Salaam, kwenye eneo lolote hata kwa nusu saa tu maana yake na TANESCO mnapoteza kwa sababu umeme utakuwa hautembei. Kwa hiyo zile gharama zitakuwa haziongezeki, Kwa hiyo ni vizuri mkaliangalia hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Ningependa mpango madhubuti kabisa wa kuhakikisha tunakwenda kulitatua tatizo la kukatikakatika kwa umeme Dar Es Salaam. Tunapokuwa na umeme wa ziada kwamba tuna umeme mwingi tuliozalisha kuliko tunaoutumia, lakini kama bado umeme huku unakatika katika wananchi hawawezi kuona hicho tunachokizungumza; kwa sababu kama kweli tuna umeme wa kutosha kwa nini basi unakatika katika?

Kwa hiyo hizi sababu ndogo ndogo, za miundombinu za Transformer, tuhakikishe tunazimaliza ili watu waendelee kuutumia umeme, tena umeme wa uhakika.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)