Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon. Julius Kalanga Laizer

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Monduli

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Spika, nami nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia jioni hii, nitumie pia nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rasi wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa nia yake ya dhati ya kujaribu kusimamia rasilimali za taifa hili kwa ajili ya vizazi vya sasa na vijavyo kwa ajili ya maslahi ya taifa letu.

Mheshimiwa Spika, lakini kwa dhati ya moyo wangu kabisa, nimpongeze sana Waziri pamoja na Naibu wake na watumishi wote wa Wizara ya Ardhi kwa kazi kubwa ambazo wanafanya, ndiyo maana leo ukisema tumalize sa hivi, kila mtu anasema tumalize. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hii ni historia, sisi tulikuwa tunafuatilia Bunge nje, wewe ni mzoefu katika Bunge hili, ni kwa mara ya kwanza Wizara hii inapata kupita kwa Wabunge kuchangia kwa nia njema ya kujenga na kuishauri Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumekuwa na migogoro hii mingi na katika muda mfupi ambao Serikali hii imeingia madarakani, hata mauaji yale ya Kilosa na maeneo mengine ya wafugaji, si kwa kiwango hicho; kwa nini tusipongeze? Na kumpongeza mtu anapofanya vizuri ni kumtia moyo afanya vizuri zaidi; tusiwe na huruka ya kukosoa tu kila siku na kulalamika kila siku. Katika Wizara hii pamoja kwamba sisi ni wadau wazuri wa ardhi, ukianzia Kongwa, Kondoa yote mpaka Arusha na kule Kaskazini, lakini kwenye hili kwa leo sina malalamiko yoyote, naipongeza Wizara kwa kazi nzuri wanayofanya na kwa kuanzia Monduli wamefanya kazi kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sisi miaka hiyo ya 1988 ardhi yote ya Monduli ilichukuliwa, wakapewa wawekezaji wakubwa, kwa hiyo hatukuwa na ardhi. Leo nikisoma hatua ya kambi ya upinzani wanalalamika Rais kurejesha ardhi, mashamba makubwa ya pori, kuwarudishia Watanzani; najiuliza, hawa wanawatetea watanzania wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wamefika mahali katika kurasa zao wanaeleza mpaka kuhoji mamlaka ya Rais aliyopewa kwa mujibu wa Katiba, kusimamia ardhi yetu kwa niaba ya Watanzania; wanataka Bunge hili liunde kamati ikafanye nini? Na ninashangaa kama wenzetu hata utaratibu wa kufuta mashamba makubwa hawajui; wanauliza hapa, wanasema tuambiwe ni utaratibnu gani unatumika? si inaanza kwenye halmashauri?

Mheshimiwa Spika, lakini bahati nzuri aliyesoma hotuba hii anatoka mjini, ambao wao kazi yao wakishaona ghorofa wamemaliza. Sisi ardhi ni muhimu sana kuliko vitu vyote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tumtie Rais moyo kwa kuthubutu kurejesha mashamba ya watu waliyomiliki. Ukisoma Sera ya Ardhi ya Nchi yetu, inasema kugawa ardhi kwa haki na kwa usawa kwa raia wote. Ninyi wengi mnafahamu…

TAARIFA

SPIKA: Mheshimiwa Laizer kuna taarifa, Mheshimiwa Wilfred Lwakatare nimekuona.

MHE. WILFRED M. LWAKATARE: Mheshimiwa Spika, ningependa kumpa taarifa mzungumzaji anayezungumza hivi sasa, naomba arejee vizuri kwenye hotuba ambayo tumewasilisha hapa. Suala ambalo limezungumziwa ni kwamba ni kutaka kujua transparence, utaratibu unaofuata kwa sababu kuna malalamiko kwamba zoezi hili halina transparence lakini tumeunga mkono sheria yenyewe jinsi ilivyo tumeiunga mkono. (Makofi)

SPIKA: Taarifa hiyo Julius unapewa, unaipokea?

MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Spika, malalamiko kutoka wapi, aliyefuta mashamba ni Rais, wao wanapeleka malalamiko kwa Lwakatare, basi akawaundie tume. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sisi tunachosema, kwa mtu ambaye haridhika na uamuzi wa Serikali afuate utaratibu wa sheria uliopo kudai haki yake. Kulalamika uvunguni maana yake kitu unacholalamikia hakina haki wala hakina usawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, haya malalamiko yanayokuja kwenu tu lakini sisi hatuyaoni, tusipoteze muda, tuendelee kurejesha mashamba yale ambayo ni mapori, watanzania watumie. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hatuna mashaka na uadilifu wa Mheshimiwa Rais wetu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni Rais wa wanyonge, hawezi kuwa sehemu ya kumuonea mtu yeyote, lakini na wengine wasiwaonee wengine, hili ni genge tu walianza mwaka jana, kutaka kushawishi kwamba, kwa nini watu wanyang’anywe mashamba, tutaendelea kunyang’anya kwa mujibu wa utaratibu ili wote tuwe na haki ya kutumia ardhi hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunasema tunaungana na Serikali, kwamba mashamba mengi ambayo hayajaendelezwa warudishiwe watanzania wanyonge waweze kulima, waweze kufuga na sisi tujione hata tusio na fedha ya kumiliki makubwa Serikali inaweza ikatutetea tukapata madogo, tukaweza kutumia kwa maslahi mapana na nchi yetu. Songeni mbele, tumpongeze Rais, tunaungana Bunge hili kwa ajili ya kazi anayofanya. Amethubutu kupunguza mashamba ya wakubwa ili wanyonge tufaidi ardhi yetu ya nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, labda niseme moja na ninaomba Serikali ilichukue. Mwaka 1974 aiyekuwa Mbunge wa Monduli wakati huo, Hayati Edward Molinge Sokoine, akishirikiana na Rais wa wakati huo, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere walitoa ardhi kubwa ya watu wa Monduli ili iwe chini ya jeshi iweze kutumika kwa mafunzo ya kijeshi na malisho ya mifugo ya wananchi wa Monduli, na tukaridhia jambo hilo!

Mheshimiwa Spika, mwaka 1988 baada ya kurudishwa tawala za mikoa na kuwepo Wakuu wa Mikoa, baadhi ya watu waliingilia kwenye ardhi ile na kujimilikisha kinyume na utaratibu. Mwaka 2014 wakati Mheshimiwa Jenista na Kamati yake ile mliyounda wakati ule na akina Sendeka wakaja Monduli, tukaita Mkutano Mkuu wa wananchi wa Monduli, tukasema ardhi yetu ile ni salama ikiwa chini ya jeshi kuliko kuacha ikiwa wazi. Wale watu wameendelea kuzunguka katika Wizara mbalimbali wakitafuta kulipwa fidia; na baadhi ya watumishi wasio waaminifu, wanashirikiana nao. Mheshimiwa Waziri wa Ardhi usikubali, ardhi hiyo tulitoa kwa jeshi mwaka 1974, walioingia mwaka 1988 walivamia. Sisi tunafikiri tuko salama tukiwa kwenye mikono ya jeshi letu la ulizni na usalama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na Monduli ni sehemu ya majimbo machache ambao sisi tunaheshimiana sana na jeshi, msituletee manyang’au na wezi wa ardhi yetu, ardhi ibaki chini ya jeshi. Leo tusingekuwa na mahali pa kulisha.

Mheshimiwa Spika, ukienda Monduli, kutoka Makuyuni, mpaka Dukabovu, upande wote wa chini, mpaka Rockdale kwenda Tarangile, ni eneo ambalo wanajeshi wanafanyia mazoezi na sisi mifugo yetu imeponea maeneo hayo wakati wote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hao wanaotafuta fidia wako 42, hawawezi kuhatarisha uhai wa wananchi wa Monduli wanaozidi laki mbili, haiwezekani. Kwa hiyo, kwa sababu hatukutani nao kwenye hizo corridor, si maamuzi ya Monduli wala wananchi wa Monduli. Sisi tunachosema ardhi ibaki kuwa chini ya jeshi…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Julius Karanga, muda wako umeisha.

MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Spika, kuhusu utaratibu.

MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.