Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon. William Vangimembe Lukuvi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ismani

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa heshima uliyoipa Wizara yetu ya kuwa kwenye kiti kuanzia asubuhi mpaka jioni na kusimamia Mkutano huu wa leo, nakushukuru sana. Nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa heshima kubwa waliyotupatia, nataka kuwahakikishia kwamba tutaendeleza kasi yetu ya utendaji na ushirikiano kama tulivyoanza, Mungu atusaidie.

Mheshimiwa Spika, pia namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa nguvu anayotupa maana hii nguvu yote tunapumua, tunaishi na tunafanya kazi kutokana na msimamo na nguvu anayotupa. Kama yeye angekuwa hatupi nguvu, tusingekuwa na nguvu, kwa hiyo sisi tunapata nguvu kutokana na kiongozi wetu kwa nguvu anayotupatia na msimamo alionao, sisi tunafuata humo humo, barabara anayopita na sisi kwa sababu ya nguvu yake na imani aliyonayo kwetu ndiyo maana na sisi mnatuona tunachacharika. Kwa hiyo, nawashukuruni sana Wabunge wote kwa shukrani, wengine hawakusema lakini wamepiga makofi, tunashukuru sana, Mungu awabariki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nawashukuru sana wale waliopata nafasi ya kusema leo asubuhi na mpaka jioni. Labda nianze na wachache niliowaandika hapa; Mheshimiwa Yussuf namshukuru sana kwa shukrani zake, lakini amesema machache hapa, nataka kumwambia kwamba tutayazingatia na ushauri mwingi aliosema ila nataka nimhakikishie kwamba ni kweli kama alivyosema migogoro kati ya wilaya na wilaya na vijiji na vijiji, hata maelekezo ya Mheshimiwa Rais ameagiza kwamba Viongozi wa Mikoa na Wilaya lazima washughulikie kutatua migogoro hii ya mipaka ya wilaya na wilaya na vijiji na vijiji. Sisi kama Wizara tutaendelea kusimamia jukumu hili.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Saed Kubenea nashukuru kwa ushauri wake wa National Housing, lakini juu ya kiwanja hicho cha 20,000 ambacho amesema binafsi nilimwalika, aje anikumbushe kidogo ili tuweze kuona kama tunaweza tukakishughulikia, tupo hapa hapa wiki nzima ijayo tuonane hapa. Si vizuri jambo lake binafsi nikalizungumza hapa ndani, tutaonana.

Mheshimiwa Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Mabula kwa pongezi zake na suala la urasimishaji nakubali kwamba Nyamagana wanafanya vizuri sana na yeye amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kwamba watu wake wote wanamilikisha zile squatter. Sasa asilimia kubwa ya wananchi wa Wilaya ya Nyamagana hawaishi kwenye squatter, wanaishi kwenye mazingira halali na wamepata na hati za kumiliki. Sasa hilo tatizo la milimani namwahidi nitakwenda huko milimani, tutali-solve huko huko milimani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia namshukuru sana Mheshimiwa Hawa Ghasia kwa shukrani alizonipa na ushirikiano wake aliotuwezesha kupanga master plan ya kwanza. Kwa Awamu hii ya Tano tumepanga master plan kule Mtwara, lakini Mheshimiwa Hawa Ghasia alitupa ushirikiano mkubwa, tumepanga master plan nzuri ambayo imeshirikisha Mtwara Mjini na maeneo mengine ya Mtwara Vijijini.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Dkt. Kiruswa na Mheshimiwa Julius wasiwe na wasiwasi, habari ya mipaka ya Longido, Arumeru na Monduli itashughulikiwa. Bahati nzuri aliyekuwa msimamizi wa masuala ya upimaji wa mkoa nimempandisha cheo, ndiyo Mpimaji Mkuu wa Tanzania sasa na kazi anaijua, atarudi kule kwenda kuhakikisha mgogoro wa mpaka kati ya Arumeru, Monduli na Longido anahuisha pamoja na mgogoro wa kijiji cha Mheshimiwa Julius lazima ataukamilisha. Kwa hiyo, nashukuru sana asiwe na wasiwasi Daktari tutakwenda kukamilisha huu mgogoro, lakini ushauri mwingine alioutoa, tutaushughulikia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Julius namshukuru sana, naomba tu watu wa Monduli wakamilishe, tumefuta mashamba 15, watupe mapendekezo wanataka kuyatumia namna gani, lakini nashukuru sana kwa ushirikiano. Kila nilipokwenda Monduli nimemkuta Mheshimiwa Julius tumeshirikiana naye na nashukuru kwa ushirikiano wake na tutafuatilia kuhakikisha kwamba hii ardhi ya Jeshi la Wananchi inakuwa mali ya Jeshi na hatutoi fidia kutokana na ushauri wake kwa sababu ni maoni ya Halmashauri ya Wilaya ya Monduli siyo maoni ya Mheshimiwa Julius. Halmashauri yenyewe ilishaandika kwamba wangependa hili eneo liwe mali ya Jeshi kwa sababu wananchi hawakatazwi kuchunga ndani ya eneo la Jeshi. Kwa hiyo, nawashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Devotha Minja namshukuru kwa ushauri wake. Wakati mwingine mimi shemeji yako awe ananidokeza huko nje halafu anakuja, kwa hiyo asinichukie nikienda kule, huwa nakwenda wakati mwingine ananiambia.

Mheshimiwa Spika, Morogoro nimechukua hatua wiki iliyopita nimeamua kuwaondoa watendaji wote wa ardhi wa Mkoa wa Morogoro kwa sababu mimi ni mtu mzima, siwezi kuagiza leo, nikirudi yanafanyika yale yale. Pamoja na uhamisho ninaofanya kwa watendaji wa sekta nzima ya ardhi, lakini wa Morogoro wote lazima watoke. Hata kama sina ushahidi kwamba hawafai, nitawatafutia kazi, siwafukuzi kazi, lakini watoke kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka nianzishe Kanda Maalum ya Morogoro, ardhi ya Morogoro ina rutuba, iko katikati ya uzalishaji, nitaweka kanda maalum lakini pia na watendaji watakuja wapya ili tuipange na tuisimamie vizuri Morogoro. Kwa hiyo, nashukuru kwa ushauri wake Mheshimiwa Devotha Minja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunafanya haya tunajituma kwa sababu Mheshimiwa Rais wetu ametutuma twende kwa watu. Kwa hiyo, siwezi kukaa ofisini, lazima niende kwa watu na nitakwenda tena Morogoro nitafunua hayo mafaili machafu, ataniona tena, kwa sababu sisi lazima tutoke twende kwa watu. Kwa hiyo, isimkere sana akiniona nakwenda kwa watu, lazima niende.

Mheshimiwa Spika, bomoabomoa ya Ubungo – Kibamba Naibu Waziri ameshaelezea na Waziri wa Ujenzi alishawahi kueleza hapa na aliwahi kuja na hukumu kwamba wakati mwingine Serikali sikivu hii ya Awamu ya Tano lazima isikilize na itii amri ya mahakama, kama watu wameshindwa kesi mahakamani unafanyaje?

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rhoda namshukuru kwa ushauri wake, lakini bado narudia kwamba, pamoja na kwamba kuna matatizo kati ya maeneo ya Jeshi na wananchi huko Mpanda, lakini mara nyingi utafiti wetu umegundua, sehemu nyingi wananchi wanafuata maeneo ya Jeshi kwa sababu hiyo hiyo kwamba maeneo ya Jeshi hayana mipaka na hayana alama zinazoonekana. Mimi nimeelekeza taasisi zote za Serikali ziweke mipaka inayoonekana, wapime maeneo yao na waweke alama zinazoonekana ili kila mwananchi ajue ni ardhi ya Serikali/ taasisi inaanzia wapi kwenda wapi, lakini kutokuona alama isiwe kisingizio kwa watu kuvamia ardhi za maliasili, jeshi au mali za taasisi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Rhoda kama anajua kwamba watu wamekaa kwenye ardhi ya Jeshi, awashauri tu waondoke kwa sababu sisi tusingependa wafanye hivyo, ardhi ya jeshi kwanza inakuwa ni ardhi ya akiba kwa wote, Jeshi linatunza tu ardhi, lakini kuna installation kwa ajili ya manufaa ya Watanzania. Kwa hiyo, najua migogoro ya mwingiliano wa Jeshi na wananchi.

Mheshimiwa Spika, katika Kamati yetu na Mheshimiwa Mwinyi, Waziri wa Ulinzi amejitahidi sana kupitapita katika maeneo mbalimbali. Kule ambako Jeshi limevamia ardhi ya watu, kuna mpango wa kuwalipa fidia lakini maeneo ambayo wananchi wamevamia ardhi ya jeshi hawatalipwa fidia.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rashid nashukuru sana kwa ushauri wake, hivi viwango nilivyosema vya Sh.150,000 ni vya urasimishaji ambao wanakubaliana kwenye mitaa kila mtu anachangia ili apate hati, siyo kodi ya ardhi. Kodi ya ardhi inatozwa kulingana na thamani ya ardhi kwa kila eneo la Tanzania; kodi ya ardhi ya Dodoma haiwezi kuwa sawa na Tunduru. Kwa hiyo, Sh.150,000 ni viwango vya sasa, tulianza na Sh.300,000 kwa makampuni binafsi, sasa ni Sh.150,000 na fedha hizi zinatunzwa na Kamati za Urasimishaji za maeneo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunafanya uchunguzi kwa sababu tumegundua sehemu nyingine wanarasimisha kwa Sh.100,000 na wengine chini ya Sh.100,000. Mungu akipenda Bunge lijalo watagundua viwango hivi vimepungua zaidi, tunataka kufanya utafiti ili tupunguze gharama ya urasimishaji kwa wananchi. Hivi karibuni tutatangaza gharama za upimaji wa mashamba maana hawa warasimishwaji ni nyumba za mijini, tutatangaza gharama za upimaji wa mashamba ili watu wajue kwa sababu gharama za mashamba za upimaji zinapaswa kuwa ndogo zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, huu ni urasimishaji, lakini kodi ya ardhi kwa ushauri wake kama alivyotuahidi, tutafanya utaratibu ili Maafisa Ardhi waweke viwango hata huko kwenye notes board za Wilaya kwamba ukiwa na square meter kadhaa, kodi ya ardhi ni kiasi fulani, wataweka. Hii ni kwa sababu kuna kodi zinatofautiana, maeneo ya biashara ni tofauti, maeneo ya makazi tofauti na maeneo ya mashamba ni tofauti na ni kwa mujibu wa sheria.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbarouk nashukuru sana kwa ushauri wake. Maeneo ya Jeshi haya nimeyasikia, nilikwenda pale nilimjibu siku ile, bahati mbaya sikuwa nimemwona, lakini Mheshimiwa Ummy alinialika kwenda pale, alinialika nilishakwenda pale na haya maneno yote ya Tanga nilishayasikia, lakini nikipata fursa siku nyingine nitarudi. Maneno mengi tulizungumza siku ile nilipokwenda, nilipoalikwa na Mheshimiwa Ummy Mwalimu, Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Tanga, tulizungumza pale na nikafanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Tanga kuna matatizo mawili, hayo anayozungumza na airport. Jambo la airport linashughulikiwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa kwa sababu ipo tabia na iko fununu kwamba yupo Mwenyekiti wa Mtaa pale aliuza yale maeneo kwa watu, kwa hiyo, hatuwezi kuingia kichwa kichwa kulipa fidia kwa watu wakati tunajua kuna mtu nyarubanja pale alijifanya ni ardhi yake akauzauza. Kwa hiyo, uchunguzi unafanywa na Kamati ya Ulinzi na Usalama kwanza ya Mkoa ili wahakikishe kwamba wale waliojenga ni wananchi ndiyo, lakini walipataje. Hatuwezi kuwalipa fidia wao wakati wao kuna mtu mwingine alinufaika kwa njia haramu. Kwa hiyo Kamati ya Ulinzi na Usalama inashughulikia na mengine haya tutakuja kushughulikia pamoja na hilo eneo la Ramsim.

Mheshimiwa Spika, shamba la Ramsim lote ni la Umoja wa Vijana. Nilikwenda kwenye mkutano shida yao ilikuwa wanataka kujua gharama tu za urasimishaji na nini, lakini wananchi walikiri kwamba lile ni shamba la Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Susan Kiwanga nashukuru sana kwa kutufariji kwa kufiwa kwa hawa vijana, lakini nataka nimuhakikishie kwamba nilichokisema mimi ni kwamba, kuna tofauti kati ya mipango miji, nimetumia sheria inayonipa madaraka ya kupandisha hadhi maeneo ya vijiji kuwa ya mipango yaani yapangwe kimji, lakini sina mamlaka ya kutangaza Mamlaka za Miji. Kwa hiyo, asishangae kuona kwamba Mlimba kuna vijiji vimetangazwa vipangwe kimji na watu wapewe hatimiliki lakini mamlaka ni ya kijiji.

Mheshimiwa Spika, hata maeneo yote niliyotangaza humo 455 kwenye mikoa yetu, mamlaka bado ni za vijiji ila vijiji vyenyewe vimepata hadhi vinapangwa kimji, yaani upangaji wake ni kama upangaji wa mjini siyo vijijini na wamiliki wa maeneo hayo tunawapa hatimiliki za miaka 99 siyo hati za kimila. Kwa hiyo, mwenye mamlaka ya kutoa utawala au mamlaka ya kujitawala katika miji ni TAMISEMI lakini sisi tunatoa hadhi ya upangaji wa ardhi. Kwa hiyo, sisi tumetoa upangaji wa ardhi vijiji 455 tumevipandisha hadhi, mamlaka ni vijiji lakini ardhi inapangwa kimji.

Mheshimiwa Spika, maeneo mengine ya Stiegler’s tutaoa taarifa baadaye maana haya maeneo anayosema Mheshimiwa Susan ndiyo zile Ramsar site ulizosema juzi. Hii miradi tumeshirikiana na Wizara ya TAMISEMI pamoja na Halmashauri zote, ni kweli waliwaondoa watu ambao walikuwa wamevamia kwenye maeneo oevu, maeneo ya TAMISEMI lakini mradi wangu huu unashughulika sana vilevile na kuondoa migogoro. Si kweli kwamba wakifika migogoro wanaiacha, hapana, Mheshimiwa Susan atakuwa hawatendei haki, wamejitahidi sana kusuluhisha migogoro labda huo mmoja anaoujua, lakini sehemu kubwa tumetatua migogoro ya mipaka ya vijiji, hata migogoro ya mashamba kwa sababu tusingeweza kuwapimia watu hati zao bila kutatua migogoro. Kwa hiyo, sehemu nyingi tumeweza kutoa sasa hati 200,000, tusingeweza kutoa hati za kimila za mashamba 200,000 kweli bila kuwa na migogoro ya mipaka, kwa hiyo tumejitahidi sana. Akikaa nao aendelee kuwapongeza, asiwavunje moyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Agnes namshukuru sana na kwa kweli mipaka ya hifadhi na ndiyo maana nimezungumza kwenye mambo ambayo yalikuwa yana hitilafu katika Wilaya zile za Tarime, Serengeti na Bunda, ni ule mpango wa buffer zone ambao kwenye Kamati yetu tumeuangalia na nafikiri wakati ukifika majibu yakitoka tutatoa taarifa, lakini nashukuru kwamba kweli migogoro imekwisha na leo tunapanga matumizi bora ya ardhi Bunda, Serengeti na maeneo mengine.

Mheshimiwa Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Serukamba kwa pongezi zake na ushauri wake mkubwa kuhusu National Housing tutauzingatia juu ya namna ya kujenga nyumba za kupangisha na za kuuza na masuala yote ya micro financing.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rose Kamil tutafuatilia hayo mashamba, lakini ufutaji wa mashamba yasiyoendelezwa ni kazi ya Halmashauri, ndiyo inaanzaisha hiyo process. Fursa ya kwanza imetolewa na Halmashauri yenyewe kufanya ukaguzi juu ya mashamba yaliyomilikishwa katika Halmashauri kubaini kama yamekiuka utaratibu, watu hawalipi kodi na hayaendelezwi.

Mheshimiwa Spika, pale kwenye Halmashauri ya Hanang tumewapelekea mtu anaitwa Afisa Ardhi Mteule, yule ni Kamishna pale ndiye mwenye jukumu pekee la kutoa notice kwa yule mwenye shamba ili aweze kujieleza hatimaye lifutwe, asipotekeleza yeye, wasipotupa jicho lao kwanza kule, mimi siwezi kuchukua hatua. Kwa hiyo, ningependa arudi na maelekezo yangu kwa Afisa Ardhi Mteule kwamba yeye amesema Bungeni, lakini nimewatupia mpira halmashauri, amwambie Mkurugenzi wayakague, wamtume Afisa Ardhi Mteule achukue hatua, hizo hatua wakichukua ndiyo zitakuja kwangu, nampelekea Mheshimiwa Rais anayafanya hayo mambo kwa mujibu wa sheria. Kwa hiyo, ningependa mambo hayo kidogo tuanzie kule Wilayani, yakifika kwangu inakuwa rahisi, mashamba haya yote aliyoorodhesha waende wakafanye ukaguzi watuandikie kisheria. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Mnzava, nitapita kwenda Tanga hivi karibuni kuangalia hayo mashamba aliyoniambia. Namshukuru sana Mheshimiwa Mnzava, lazima tushirikiane. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Selasini kwa pongezi zake, tutaendelea kushirikiana. Hana matatizo sana kule kwake lakini tutakwenda kuangalia hayo matatizo. Napokea ushauri juu ya Wakala wa Nyumba ila kwa bahati mbaya mimi na Wizara yangu tumeamua kwamba tutaendelea kufanya kazi kidogo za uwakala kupitia Shirika la Nyumba kwa sababu Shirika la Nyumba nalo limeshafanya utafiti na kujua aina ya nyumba zinazoweza kujengwa vijijini na nini, lakini ile taasisi tunataka tuipeleke Chuo Kikuu itafanya vizuri zaidi kuliko ikibaki kwetu. Nakubali kwamba standard za ujenzi ndivyo zinavyokuwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunaposema tunatoa kibali cha ujenzi nyumba yoyote ya mjini tunakupa kibali cha ujenzi lakini tunakutajia na aina ya nyumba, tunajua kabisa. Tunapopanga miji na master plan inajulikana kabisa eneo hili unatakiwa ujenge nyumba ya ghorofa moja, eneo hili nyumba ya ghorofa mbili; eneo lililopangwa kujengwa nyumba ya ghorofa moja huwezi kujenga nyumba ya ghorofa mbili hata kama una hela, hutapata kibali.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ni mahali ambapo wale watoa vibali wamelegea, ndiyo maana hawazingatii standards, lakini kwa mujibu wa ujenzi wa nyumba mijini unaenda kwa standards na ndiyo maana hapa Dodoma Mjini ukijenga sasa hivi unaambiwa na bati weka rangi fulani, hizo ni standards za wapangaji miji lazima na CDA zamani walikuwa unataka kujenga mahali, ramani hii hapa nenda kajenge. Kwa hiyo, tutaendelea kuelimishana juu ya ushauri wake kwa sababu ni muhimu sana huu ushauri katika upangaji wa miji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Pallangyo karibu sana, namkaribisha sana na nampongeza sana kwa ushindi, tutafanya kazi pamoja. Tulikwenda Arumeru pale bila shaka nimemwambia juzi, yapo mashamba ambayo tumeyafuta pale kwa niaba ya wananchi, tena moja lilikuwa la Chama cha Ushirika, walikuwa hawafanyi nalo kazi, wakataka wananchi wakalime kwenye mawe halafu huku wakodishe, tumelifuta. Hata hivyo, bado wana deni hawajaniambia utaratibu wa namna ya kulitumia. Kwa hiyo, Mheshimiwa Pallangyo tunamkaribisha sana, nampa fursa kama ana mengine pengine kwa sababu ya dakika tano nipo hapa tuzungumze ili tushirikiane mambo yaende haraka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nirudie hili la watendaji wa Serikali, ni kweli nimesema asubuhi kwamba watendaji wa Serikali ni wachache lakini pia tumegundua hawakupangwa vizuri, kwa hiyo tunarudia kuwapanga upya. Kwa uchache huo huo nataka kuahidi maeneo ambapo kulikuwa hakuna watendaji wa Serikali wa sekta ya ardhi watapatikana. Tunataka hawa watendaji watumike kama wasimamizi kwa sababu sasa kazi nyingi za sekta ya ardhi za upangaji na upimaji makampuni binafsi wanatusaidia lakini hawawezi kufanya kazi hizi ndani ya Wilaya kama hatuna mtu wa sekta ya ardhi pale wilayani. Kwa hiyo, tutawapanga vizuri na kuhakikisha kwamba wanaenea kila mahali.

Mheshimiwa Spika, masuala mengine ya RERA ambayo Msemaji wa Upinzani amezungumza Real Estate Regulatory Authority, najua kila mwaka huwa wanazungumza. Sheria hii sisi draft tumeshamaliza, tunakamilisha utaratibu wa Serikali, naamini ipo siku itaingia hapa. Sheria hii tunataka itusaidie kusimamia haki za wapangaji, haki za Serikali kwa kodi, lakini pia kusimamia sekta yenyewe ya ardhi kwa sababu tumegundua katika sekta ya ardhi inatumika sana na baadhi ya watu kwa ajili ya kutakasa fedha na kuingiza fedha haramu kwenye ardhi. Kwa hiyo, tunaifanyia kazi hii sheria na Mungu akipenda itafika hapa.

Mheshimiwa Spika, suala la ulipaji wa kodi nataka kusisitiza tena, kila mtu ambaye anadaiwa kodi, wakiangalia kwenye kile kitabu mbele ya jalada safari hii sikuweka sura yangu, nimeweka maneno fulani. Ukiangalia yale yamewakumbusha Waheshimiwa Wabunge ukitaka kujua deni lako, angalia pale, ukitaka kulipa kodi ya ardhi angalia juu ya kitabu nimefanya makusudi. Kwa hiyo, waangalie huo mfano kila mtu ajue, kama anadaiwa tafadhali asisubiri nimtangaze tarehe 30 Juni kwenye gazeti maana majina yote ya wanaodaiwa nitawaaibisha mwisho wa mwezi wa sita. Kwa hiyo, naomba waangalie hilo jedwali nimewatumia ili uangalie kama unadaiwa, mimi nisingefurahi sana Waheshimiwa Wabunge niwatangaze kwamba wanadaiwa kodi ya ardhi maana sheria zenyewe wametunga wenyewe.

Mheshimiwa Spika, nyuma ya jalada la kitabu nimeonesha aina mpya ya hati tunayotoa ya kielektroniki ya karatasi moja. Halafu ndani ya jalada la nyuma nimewaonesha leseni ya makazi ya elektroniki moja ambayo tunatoa na tunataka leseni za makazi zisambae baada ya bajeti hii, mpango huu uingie mikoa yote kwa sababu ni jambo rahisi. Watanzania vijana wataalam wa Wizara yangu wametengeneza teknolojia moja, wametengeneza app moja ambayo tutaambukiza katika Halmashauri zote halafu watu wachangie shilingi 5,000 wapate leseni. Ni kama hati lakini ya miaka mitano, itawasaidia.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo katika kitabu hicho kuna alama ambazo nimezitumia safari hii zitawasaidia Waheshimiwa Wabunge, hasa hiyo iliyopo ukurasa wa kwanza, ninaomba kila mtu ajaribu, utumbukize plot numbers zake zile halafu itamjulisha anadaiwa kiasi gani ili mlipe na Watanzania wote nawaomba walipe kodi ya ardhi.

Mheshimiwa Spika, mwisho wa mwezi wa sita nimeagiza mabaraza yote ya ardhi, hakuna kesi nyingine isipokuwa kuwaswaga mbele ya mabaraza yale watu ambao hawajalipa kodi ya ardhi; na Serikali, mimi Waziri asiniandikie mtu hata mmoja akiomba nimpunguzie penalty, hapana, sina madaraka hayo. Ukitaka sasa upunguziwe penalty, lipa kabda ya mwezi wa sita, ukiruka mwezi wa sita penalty yako iliyopo sasa inaruka kwa asilimia 300.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo naomba Watanzania wote kupitia tangazo hili angalieni mnadaiwa kiasi gani, kila mtu anayemiliki ardhi kwa hati ahakikishe kwamba analipa kodi ya ardhi ya kila mwaka. Wenye leseni ya makazi wanalipa, wenye hatimiliki wanalipa, isipokuwa wale wananchi maskini, Serikali ya Awamu ya Tano imewaonea huruma, wale wanaomiliki kwa hati za kimila, wale hawalipi kodi ya ardhi, wale wenye vishamba vya vijijini kule wenye hati za kimila Serikali imewasamehe, hawalipi kodi za ardhi. Lakini wale wanaomiliki hatimiliki, iwe ya shamba, iwe ni kiwanja mjini au shamba la mjini, lazima walipe kodi.

Mheshimiwa Spika, lakini wale wote wanaomiliki kishamba au nyumba ambayo ina kiwanja kilichopimwa mijini lazima aingie kwenye process ya urasimishaji apate hati ya muda mrefu, alipe kodi au aingie kwenye leseni za makazi alipe kodi. Hata kama una kishamba mjini, lazima upime uchukue leseni ya makazi tukutoze hela.

Mheshimiwa Spika, kuna watu wana maeneo makubwa mjini hawataki kuyapima kwa sababu wanajua mwisho wake watalipa kodi kila mwaka lakini wakivamiwa kidogo wako kwa Waziri. Tunataka mtu mwenye shamba mjini, mwenye kiwanja mjini, mwenye nyumba mjini, hana hati achukue hati kupitia urasimishaji au leseni ya makazi ambayo gharama yake ni shilingi 5,000, shilingi 4,000 zinakwenda Halmashauri kwa kazi ya kutayarisha leseni yenyewe, shilingi 300 anachukua Mwenyekiti atakayemsindikiza yule kijana anayekwenda na simu kupima zile nyumba na shilingi 700 ni yule kijana mwenye simu anayekwenda kupima. Kila nyumba yule kijana atapata shilingi 700.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo hii inatengeneza hata ajira kwa vijana wetu wa Wilayani kwenu; ni simu tu. Sisi tutamuwekea kifaa mule kwenye simu, akipita kwenye nyumba, uzoefu wetu unaonesha kijana anaweza kupima nyuma 20 kwa siku moja, Dar es Salaam wameweza, kwa hiyo nyumba 20 kwa siku moja na leseni zitatoka. Kwa hiyo nyumba 20 tunapata shilingi 5,000, shilingi 4,000 zinaingia kwenye Halmashauri, shilingi 300 anapewa Mwenyekiti wa Mtaa anayemtembeza huyu kijana anayepima, na 700 anapata yule kijana mwenyewe, kwa hiyo hii ni ajira. Mtakuta vijana wengi hata waliosomea masomo mbalimbali huko wenye simu za aina hii wanaweza kufanya hiyo kazi na kila siku akawa anaingiza mfukoni hata shilingi 10,000. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tuchangamkie fursa hii, nataka baada ya zoezi hili kufanikiwa Mkoa wa Dar es Salaam tutahakikisha sasa tunakwenda mikoa yote ili kila mtu awe na hatimiliki au leseni ya miaka mitano. Lakini tungependa kila Mtanzania awe na hatimiliki ya ardhi yake ili aweze kulipia kodi. Kwa hiyo ni suala la msingi na la lazima.

Mheshimiwa Spika, Naibu Waziri amesema hapa, watu wote ambao tayari tumeshawapimia halafu wamepewa invoice wanakaa nayo miaka mitatu, tunawatoza kodi kuanzia mwaka huu lazima walipe. Haiwezekani tumeshakupimia tumekupa na invoice hutaki kuchukua hati eti kwa sababu utalipa kodi, kwa hiyo lazima wote tulipe kodi.

Mheshimiwa Spika, narudia tena kukushukuru wewe, nawashukuru Wajumbe wote, Wabunge wa Bunge hili, kwa heshima mliyotupa, Mungu awabariki sana mliochangia, mlioweza kuchangia kwa kusema nawashukuru sana, mliochangia kwa maandishi nawashukuru sana, Mungu awabariki sana. Sisi majibu yetu yatakuja kwa maandishi lakini wengine nitawafuata, ambao kuna hoja ambazo zinahitaji ufafanuzi zaidi, nimeshachukua majina yenu, nitawafuata tutakaa hapa tutaelewana zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini msisite kama nilivyosema, kama kuna wengine hawakupata nafasi ya kuandika na kusema, tupo na Mheshimiwa Spika ametupa chumba namba 11 hapa. Ukileta watu wako wawili kutoka Kasulu walete hapa, tutakuhudumia hapa hapa; ukileta watu wako watatu kutoka wapi, tutakuhudumia hapa hapa, mpaka Bunge liishe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ndugu zangu, kwa hiyo sisi tunafikiri kwamba tuna wajibu mkubwa wa kuwatumikia ninyi, lakini kuwatumikia na wananchi wote wa Tanzania. Hii ndiyo kazi tuliyopewa na Dkt. John Pombe Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja. (Makofi)

WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, naafiki.