Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Hamidu Hassan Bobali

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Mchinga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. HAMIDU H. BOBALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, kwanza ningependa kuchangia kwenye suala la korsho ambalo mzungumzaji aliyepita amezungumza.

Mheshimiwa Naibu Spika, wakulima wa korosho walikuwa wanategemea pamoja na mambo mengine tungeona maelezo ya Serikali juu ya utaratibu upi utatumika kuziondosha korosho zilizo kwenye maghala kule Lindi, Mtwara na Ruvuma. Korosho zimejaa kwenye maghala, hata sasa hivi kuna ununuzi wa ufuta, ufuta ule hausafirishwi kupelekwa kwenye yale maghala makubwa kule mikoani kwa sababu hamna nafasi, msimu wa korosho umeanza. Tunaposema sasa hivi maeneo yale ya ukanda wa pwani kama Jimboni kwangu pale Mchinga, Kilwa na kwa Mheshimiwa Nape pale Mtama tayari zimeanza na mwezi wa saba tutaanza kuokota/ kuzikusanya, mwezi wa nane/tisa zinakuwa tayari.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali hebu tuelezeni mtatumia utaratibu gani kuziondosha zile korosho zilizopo maghalani ili matajiri watakaokuja kununua mwaka huu wawe assured kwamba hawatachanganyiwa korosho za mwaka jana na mwaka huu. Inafahamika kwamba ubora wa korosho za mwaka jana hauwezi kufanana na za mwaka huu. Kwa hiyo, kama kuna mpango wowote Serikali mnaweza mkaufanya either kuziuza hata kwa undergrade ili muweze kuziondoa ama vinginevyo basi zitaifisheni ili ziondoke ili sisi baadae hizi tunazozalisha mwaka huu, tuweze kupata bei tunayostahiki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, zipo taarifa tumezisikia na tunaendelea kuzifuatilia kwamba World Trade Organization (WTO) wameanza mchakato wa kufuatilia mfumo wa ununuzi wa korosho Tanzania kwamba isije wanunuzi mwaka huu wakaja kupata hasara, kuna uwezekano mkubwa wanunuzi wakubwa wasije kwa sababu ya kuhofia korosho za mwaka jana zikachanganywa na za mwaka huu. Fuatilieni watu wa Serikali kwa sababu mpo nadhani mtakuwa mnalijua vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, uchumi wowote wa nchi lazima uwe jumuishi, kusipatikane watu wakaachwa, wengine wakaendelea sana na wengine wakawa maskini sana, tutasababisha migogoro na migogoro mingi katika mataifa ya Afrika ni kwa sababu ya distribution of resources, watu wakihisi kwamba sisi tumeachwa, wengine wameondoka, kunaleta matatizo na wakati mwingine kunakuwa na fujo katika nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, uchumi wa Mikoa ya Lindi na Mtwara unategemea gesi, korosho na uvuvi, ni jambo muhimu sana. Nitatoa mfano, wakulima wa korosho ndiyo kama nilivyozungumza, waliobakia ni wavuvi; leo dagaa hawa wanaopatikana pale Kilwa wanatozwa ushuru wa dola 1.5 kwenye kila kilo, ni zaidi ya shilingi 3,000 na; lakini dagaa hawahawa ambao wanasafirishwa kupelekwa Congo wote wanaotoka kwenye maziwa kwa mfano Ziwa Victoria na Ziwa Tanganyika ushuru wake ni dola 0.16, this is quiet unfair. Hatuwezi kuwa na uchumi ambao bidhaa moja aina inayofanana huku inatozwa kodi kubwa, huku inatozwa kodi ndogo kwa lengo gani? Uchumi wa namna hii utapelekea…

MHE. PETER J. SERUKAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

MHE. HAMIDU H. BOBALI: ...kutuacha wengine wawe wameendelea sana, wengine tuendelee kuwa maskini.

MHE. PETER J. SERUKAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

MHE. HAMIDU H. BOBALI: Mheshimiwa Naibu Spika,…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Bobali kuna taarifa. Mheshimiwa Peter Serukamba.

T A A R I F A

MHE. PETER J. SERUKAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka kumpa taarifa msemaji, mimi natoka Kigoma, Kigoma pia dagaa wale wanaosafirishwa kilo moja wanatozwa dola
1.5 siyo 0.1.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Bobali unaipokea taarifa hiyo?

MHE. HAMIDU H. BOBALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Taarifa yake nimeipokea lakini maelezo ya Waziri wa Uvuvi wakati anazungumza na hili jambo tumelifuatilia sana, tulipewa maelezo humu ndani ya Bunge kwamba dagaa wa Pwani wanatozwa dola 1.5 na dagaa wanaotoka kwenye maziwa wanatozwa dola 0.16, maji baridi maana yake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa Mheshimiwa kama hilo na wenyewe wamekuwa introduced huko, ninachozungumza kwanza hii tozo yenyewe ni kubwa sana. Kilo moja ya dagaa unapotoza dola 1.5 zaidi ya shilingi 4,000 au 3,000 tuseme ili hawa dagaa wenyewe wauzwe kwa bei gani.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mimi napendekeza hii tozo iweze kushushwa badala ya kuwa dola 1.5 walau ishushwe iwe dola moja ama chini ya dola moja ili hawa wavuvi wa dagaa waweze kupata fedha stahiki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nazungumzia uchumi jumuishi. Kwenye Ilani ya CCM iliwekwa kitu kimoja kizuri sana na kama kingetekelezwa kingewafanya Watanzania waendelee kuwa na imani sana na Chama cha Mapinduzi, kupeleka shilingi milioni 50 kwenye kila kijiji/mtaa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namna pekee ya kusaidia watu maskini ambao hawawezi kufanya biashara, wameminywa kwenye kilimo ni kuwasaidia moja kwa moja kwa kupeleka fedha kwenye maeneo yao kuwe na mtiririko wa fedha watu waweze kutumia zile fedha kwenye biashara na mambo mengine. Mngekuja na maelezo, leo kwenye bajeti ya nne hii Serikali ya Awamu ya Tano mmeshindwa kabisa hii shilingi milioni 50 kwenye kila kijiji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kama wawakilishi tunapokwenda Majimboni tunaulizwa na hakuna tamko rasmi la Serikali mlilolitoa kwamba imeshindikana shilingi milioni 50 kila kijiji, shilingi milioni 50 kila mtaa. Semeni ndani ya Bunge ili na sisi tukienda tukaseme hili limeshindikana jipangeni na mambo mengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi nasema kwa sababu kuna wakati kule Jimboni kwangu kuna watu walikwenda wakawatapeli watu, wakawaambia leteni elfu kumikumi, zile shilingi milioni 50 zinakuja na bahati mbaya sana waliowatapeli wanachama wa Chama cha Mapinduzi kwamba utaletewa na hizi fedha zikija nyie ndiyo mtapewa kipaumbele. Kwa hiyo, yangetoka maelezo ya kina juu ya jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, uchumi wa gesi; uchumi wa gesi ni uchumi ambao mimi nadhani ungeweza kusaidia Mikoa ya Lindi na Mtwara lakini pia ungeweza kusaidia kama taifa. Upo mradi wa LNG ambao financiers watu wanaotaka kutoa fedha siyo Serikali, Serikali kazi yao ni kufanya regulation na kuangalia manufaa ambayo sisi tutakuja kuyapata. Wawekezaji wapo tayari na mwezi uliopita tulikutana nao pale Lindi, tulikwenda Wabunge wote wa Mkoa wa Lindi, wanaonesha commitment kwamba wapo tayari, hatuoni progress yoyote ya Mradi wa LNG.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilizungumza wakati nachangia Wizara ya Nishati hapa, LNG kwa Tanzania siyo mradi wa kwanza Afrika. Kama kuna mambo mnahitaji ku- study kwa nini msiende kwenye nchi ambazo tayari hii miradi inatekelezwa? Kwa nini msiwende Angola, Msumbiji, Algeria na maeneo mengine mkaenda mka-study wenzetu walifanyaje, mnanufaikaje. Huu ni mradi ambao ungeweza kusaidia sana pato la Taifa kwa ku-create ajira lakini pia mngeweza kuinua uchumi wa Watanzania hususan wa Mikoa ya Lindi na Mtwara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kama Serikali upande wa Mkoa wa Lindi eneo limetengwa, wananchi wapo tayari kuhama na wameshafanyiwa tathmini ya malipo, leo huu mwaka wa nne watu wamezuiwa wasiendeleze maeneo yao, mpaka sasa hakuna kinachoendelea. Kwa hiyo, na lenyewe hili kwa sababu ni mradi wa kimkakati, mradi ambao ulikuwa unakuja kuwekezwa zaidi ya shilingi trilioni 59, ni mradi mkubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali iseme mradi huu umeishia wapi, kama hautakuwepo tena basi kila mtu aweze kujua ili wale wananchi tuweze kuwaambia kwamba haya maeneo yenu limeni ufuta na karanga, hii habari ya LNG imeishia hapa.

Mheshimiwa Naibu Spika, muda mchache uliopita nilikuwa na kikao hapo na Profesa Lipumba, Mwenyekiti wetu wa Chama ambaye pia yeye ameniambia kwamba yeye ni mwalimu wa Dkt. Mpango, amemfundisha uchumi Chuo Kikuu.

Sasa ukiangalia kwenye takwimu za Umoja wa Mataifa, takwimu ya mwisho iliyotolewa mwezi wa tatu ya hali ya furaha ya wananchi katika ulimwengu, Tanzania tupo nchi ya 153 kati ya mataifa yote ya ulimwengu. Maana yake inaonesha kwamba wananchi wa Tanzania wengi hawana furaha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa Mheshimiwa Mpango unaweza kujiuliza kwa nini watu hawana furaha na hata ndani ya Bunge inaonekana, wakati unasoma bajeti yako mwaka jana hapa, palikuwa na vigelegele na makofi, humu ndani tuliambiwa hii ni bajeti ya kihistoria haijawahi kutokea, uliposoma mwaka huu umeyaona yale? Kwa sababu huko nje watu hawana furaha na takwimu za mwezi wa tatu mwaka huu, Tanzania tunatajwa tupo wa 153 kwa kiwango cha furaha. Sisi katika Afrika Mashariki tunawazidi Burundi na jirani zetu hapa kidogo wa Somalia, kwisha habari. hata wenzetu Kenya na Rwanda wametuzidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hali/mazingira ya biashara, Tanzania tupo 144 Rwanda wapo nchi ya 29, Kenya wapo nchi ya 40, mazingira ya biashara mnakuja kutuambia uchumi unakua, kweli Mheshimiwa Mpango? Na swali moja mimi nilimuuliza Mheshimiwa Profesa Lipumba, huyu si ndiyo mwanafunzi wako, inawezekanaje haya mbona humuelezi haya maana yake anakuja kutueleza hapa. Akasema sasa wakati mwingine unapotoa ushauri usipofanyiwa kazi unaachana nao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini Mheshimiwa Mpango kiukweli kabisa vyuma vimekaza, hali ni mbaya. Hata takwimu zako wewe mwenyewe, ukisoma kitabu hiki cha hali ya uchumi. Nasikitika hiki kitabu tungekuwa tunakipata wakati ule wa kusoma randama zile kwenye bajeti za kisekta kwa sababu ingeweza kutusaidia pia kuchangia kwenye sekta.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho; ukiangalia kitabu cha hali ya uchumi, inaonesha kilimo kinachangia asilimia 28 ya Pato la Taifa, lakini kwenye bajeti yako Mheshimiwa Mpango mmepeleka asilimia 1.2. Sasa huyu ni ng’ombe gani wa maziwa ambaye unataka akupe lita 20 kwa siku halafu haumlishi yaani yeye ambaye anakupa asilimia kubwa ya pato la Taifa unamtengea asilimia 1.2. Mheshimiwa Waziri hatuwezi kwenda na kwenye uchumi wa viwanda kama kilimo hakiko vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. (Makofi)