Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Jumanne Kibera Kishimba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kahama Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. JUMANNE K. KISHIMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwanza na mimi naungana na Wabunge wenzangu kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Fedha na timu yake nzima kwa bajeti hii aliyotuletea. (Makofi)

Mimi nina suala moja tu la afya; ugonjwa siyo kitu ambacho unaweza kuchagua wala kupanga muda wa kuugua wala uwe na pesa kiasi gani au uwe maskini. Ni kweli kabisa napongeza Serikali hasa vijijini dawa ni nyingi sana sana kwa mara ya kwanza toka mwaka 1980 kumeonekana dawa nyingi sana sana hospitalini hata mimi mwenyewe nashangaa na tunashukuru sana kwa Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa sana aliyofanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye afya bado kuna matatizo mawili au matatu; tatizo la kwanza sisi tunaotoka mikoa ya Kanda ya Ziwa ambako wenyeji wa maeneo yale aidha, hawataki kukata bima kwa ajili ya tradition yao kwamba watakuwa wanajitabiria kifo au kujitabiria ugonjwa, tunaomba Wizara ya Afya au TAMISEMI wawaruhusu wanakijiji wetu anapokuwa ameugua kama ana mbuzi au kuku hospitali au zahanati zetu zipokee atibiwe ili asubuhi au mchana ziuzwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini nasema hivi mtu ameugua mchana au usiku yeye hana pesa lakini anatakiwa aende hospitali na bima hana na leo kuuza mfugo ni kazi lakini kama atapokelewa mfugo au mahindi, atapata matibabu na kesho yake vitu hivyo vitauzwa, hakuna daktari ambaye hajui kuku wala nini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wetu ni maskini, sasa hivi kumezuka kwenye hospitali za Serikali na za Misheni kitu cha kusikitisha sana. Mtu anapokufa kwanza unapewa bill ya marehemu ukiwa huna pesa wanakatalia maiti na maiti ile wanaenda kuizika kama wanatupa mbwa, ni kitu kibaya sana na humu ndani nashangaa Mheshimiwa Waziri Mpango sisi wote ni maiti watarajiwa, Bunge zima.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kishimba naomba ukae kidogo, Waheshimiwa Wabunge kwa mujibu wa Kanuni ya 28(5) naongeza muda wa nusu saa ili Mheshimiwa Kishimba aweze kumaliza mchango wake. (Makofi)

MHE.JUMANNE K. KISHIMBA:Ahsante sana Mheshimiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, narudia tena kwamba humu ndani wote Waheshimiwa Wabunge sisi ni maiti watarajiwa kasoro itakuwa muda, tarehe na wakati. Ni kweli ukiangalia kwenye bajeti yetu tumesamehe unga wa keki, lakini tunatoza tozo la maiti kwenye mortuary nakuomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha au Naibu Waziri wa Fedha hebu rudisha hiyo kodi ya unga wa keki ili tufute tozo la maiti kwenye mortuary. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, asilimia 95 ya vifo vinatokana na kuumwa na kuumwa kwenye mara nyingi ni kwa muda mrefu, kunapokuwa kwa muda mrefu huyu mtu anakuwa amedhoofika kiuchumi, amedhoofika kiafya sasa leo anafariki ni kweli hospitali inampa bili ya shilingi 500,000 anazipata wapi ameshakufa na huyu mtu wachangiaji wengi humu wamesema Watanzania woote wanalipa kodi wanavuta sigara, wanakunywa bia, wanafanya shughuli zote, sasa kwa nini Serikali isimsamehe mtu aliyefariki imsamehe bili halafu hizo pesa tuzipeleke kwenye keki ni hatari sana watengeneza bajeti najua ni vijana wetu wa Oysterbay ambao nafikiri walijua keki ni kitu cha muhimu sana ndiyo maana wakashindwa kuelewa kwamba kuna shida nyingi sana kule kwetu vijijini. (KIcheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, ulikuwa Kahama juzi nashukuru sana umepita mle njiani zile nyumba unaziona mle za nyasi ni waganga wa kienyeji. Waganga wa kienyeji ukipeleka mgonjwa bahati mbaya akafariki hawaombi pesa badala yake wanakusaidia na sanda, inawezekanaje sisi Serikali tumdai mtu aliyefariki halafu tukatalie maiti, halafu maiti tukaizike kwa kutupa kwa gharama na bahati nzuri Mheshimiwa Msigwa ni Mchungaji na Mama Lwakatare wangetusaidia sana maana yake turuhusiwe basi watu wakafanye maombi kule kwenye makaburi ya Serikali wajue na kaburi ya ndugu yao ili baadaye baada ya miaka 10 watoto wakipata hela wakachukue mifupa ya baba yao au mzazi wao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kitu ambacho kweli ni vizuri tukiangalie sana kama watakubali ni vizuri sana warudishe kodi ya keki maana yake hapo wamefuta kodi ya unga wa keki wanasema unga wa ngano ambao unatengeneza vyakula, vyakula gani ni keki na biskuti. (Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna tatizo la pili hapa sasa hivi kumezuka mtindo huu wa x-ray na dialysis ya figo. Daladala inauzwa shilingi milioni 50 mpaka shilingi milioni 100 kwa siku inaleta shilingi 50,000 mashine ya x-ray inauzwa shilingi milioni 40 mpaka shilingi milioni 100 na yenyewe mashine zote hizi, kwa nini hii inafanya shilingi 200,000 au shilingi 40,000 kwa mtu mmoja kwa nini Serikali isiruhusu watu wanunue x-ray wazipeleke hospitali ili bei ya hizi x-ray ipungue? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, najua wataalamu wataleta maneno mengi sana ambayo yanahusu afya, yanahusu nini lakini ni uongo, ni uongo kwa sababu waganga wa kienyeji wanapewa kibali na Wizara ya Afya kuendesha shughuli zao na waganga wa kienyeji hawana elimu yoyote ya hospitali, kule kwetu Kanda ya Ziwa mgonjwa mahututi ndiyo anapelekwa kwa mganga wa kienyeji ambako hakuna choo, hakuna kitu chochote, ni vipi Serikali ikatae leo kuwa watu wanunue wapeleke hizo x-ray kwenye hospitali ili bei hii ipungue? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa watu wetu ambao ni wa mjini ambao hawana pesa, nchi nyingi sasa hivi duniani bili yako ya maji na bili ya umeme inakudhamini hospitali. Anapofika mtu akatibiwa ikija bill ni shilingi 24,000 mnakaa na hospitali mna-bargain kwamba utalipa shilingi 4,000, 4,000 wanakwambia lete bill yako ya maji au bill ya umeme wanaingiza shilingi 4,000, 4,000 mle kwa kuwa TANESCO na Idara ya Maji ni taasisi za Serikali, wakichukua ile shilingi 4,000 wataipelekea hospitali, lakini mtu wetu anakuwa amepona kuliko sasa hivi kama huna pesa ni tatizo sana sana, namuomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha aliangalie sana suala hili ili kusudi itusaidie sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitaongelea suala zima la biashara; juzi kwenye mkutano wa Mheshimiwa Rais suala walilokuwa wanalalamika karibu wafanyabiashara wote lilikuwa ni suala la investigation baada ya kuwa mtu umemaliza kulipa kodi. Suala la kutafuta watu watakatifu mimi siliamini maana yake dini ina zaidi ya miaka 2000 toka Bwana Yesu aje, lakini mpaka leo watu hawajashika dini, dawa ya kumaliza mgogoro ni kuondoa zile sheria ambazo zinatusababishia mgogoro.

Mheshimiwa Naibu Spika, TRA wanayo sheria inayoruhusu mtu ambaye hakufanya hesabu wam-charge kwa percent ya mauzo, lakini sheria ile inawaruhusu wao kumu-investigate yeye, lakini sheria ile iliachwa na mkoloni na ilikuwa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kwamba kama mtu hana vitabu atalipa 2% ya mauzo yake, lakini na yeye asilete gharama zake, kwa hiyo kama mtu ameuza shilingi bilioni moja, analipa shilingi 20,000,000 na yeye hawezi kuleta hesabu zake.

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivi kwa sababu asilimia 90 ya wafanyabiashara wa Tanzania elimu yetu ni darasa la saba, wengine hawakusoma kabisa. Sasa inakupa kazi ngumu sana utunze store ya mali, utunze na stoo ya karatasi na bado karatasi hizo ukizipeleka unaambiwa hazifai lazima utatoa hela. Lakini kama wao TRA walishamfanyia investigation mtu zaidi ya miaka mitano, wakajua huyu mtu sells zake huwa ni hizi na tulikusanya hela hizi kwa nini wasichukue formula ile ile wakaigawa ikaenda kwenye sells ya mauzo ambayo itamaliza kabisa ule ugomvi wote uliokuwepo siku ile. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili ni suala la Kariakoo; ni kweli Kariakoo imekufa, lakini Kariakoo imeuwawa na vitu viwili. Wataalamu wetu nafikiri hawajui kitu gani kinauzwa Kariakoo. Kariakoo haiuzi soda, haiuzi diesel, haiuzi vitu hivi ambavyo kwenye tarrif za TRA zinahesabiwa kwa tani na lita. Vitu vinavyouzwa Kariakoo ni vitu hivi vidogo vidogo. Nitatoa mfano uki-import glass Sheria ya TRA ina kitu kinaitwa tariff, tariff ya glass inaitwa glassware, lakini kuna glass ya shilingi 800 na kuna glass ya shilingi 10,000; TRA kwa kuwa anataka pesa atachukua glass ya shilingi 1,000 kwenda kui-charge 5,000 akikuwekea kwenye shilingi 5,000 hautauza na watu wote Watanzania, wa Malawi na wa Kongo wanafata hii glass ya shilingi 1,000 hawa watu wa Samora ndiyo wanafanya glasi ya shilingi 10,000. (Makofi)

Kwahiyo nafikiri TRA waangalie tariff ni kitu ambacho tuliki-download sisi kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki iliyovunjika, ni vizuri TRA wachukue vitu waviainishe ili mtu alipie kwa kitu alicholeta, watu wote watarudi kama wenyewe watakubali watu walipie kwa kile kitu alicholeta.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi ukileta kontena moja la glass hutalilipia hapa, lazima ulipeleke Mutukula ukalipie Mutukula ili watu wachukue polepole na baskeli kuleta au ulipeleke mpaka Tunduma ili watu waanze kulileta kwa sababu watu wale kule Wazambia wanakubali ulipie kwa item uliyoleta, huku unatakiwa ulipie kwa tariff. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukileta nguo zinazouzwa Kariakoo ambazo ni t-shirt, t-shirt ziko za shilingi 3,000, iko t- shirt ya shilingi 20,000. Kwenye hesabu ya tariff unalipa excise duty, unalipa VAT halafu unaenda kwenye weight (kwenye uzito) na nguo nzito ni ile ya bei rahisi nguo nyepesi ndiyo ya bei ghali. Sasa haitawezekana ile nguo kuiuza ndiyo maana inakwenda nje halafu inarudi huku, nafikiri wataalamu wetu wa TRA... (Makofi)

MHE.SALIM HASSAN ABDULLAH TURKY: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Turky anayezungumza hapo ni Profesa sasa...

MHE. SALIM HASSAN ABDULLAH TURKY: Taarifa ninayompa maneno anayozungumza ni sahihi kabisa na ukienda kuangalia chupi ile ya kamba ndiyo ghali zaidi kuliko chupi nzima, ahsante sana. (Kicheko)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kishimba unaipokea taarifa hiyo?

MHE.JUMANNE K. KISHIMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, naipokea taarifa yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, nafikiri wataalamu wetu wa TRA ni vizuri kabisa wakubaliane na wafanyabiashara, ni vizuri Mheshimiwa Waziri wa Fedha awaite wafanyabiashara wakiwa wametulia ili apate kabisa data ili turudishe soko letu la Kariakoo. Ni kweli kabisa wachangiaji wote wanaliongea hili na kwenye Kamati ya Bajeti tumejaribu sana kuliongea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho kabisa Benki Kuu ya Tanzania nafikiri wakati wowote itatangaza utaratibu mpya wa namna ya ku-import mali. Utaratibu uliopo unaotarajiwa ni kwamba mtu lazima atume pesa kwa TT kwenda kwenye source ya kununua.

Mheshimiwa Naibu Spika, tungeomba wataalamu wote kabla hawajafanya kitu labda na wao watoe watu wao waende kule Dubai na China waone mali inanunuliwa namna gani. Kule China na Dubai hakuna mahala unaweza kumtumia mtu hela ukazikuta hizo hela, watu wananunua kule wakiwa na hela cash kwa sababu hata mali aliyokuuzia anaweza akakuletea fake na ukirudi kwenye lile duka limekuwa saloon. (Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kama utatuma hela toka hapa, utamtumia nani kule China au Dubai, haiwezekani, ndiyo maana tunaomba wataalam wetu basi labda wachanganye changanye na watu wa biashara kidogo ili wanachotengeneza kionekane cha Tanzania maana yake inaonekana kinachotengenezwa hata wananchi wanatucheka kwamba hivi hata ninyi Wabunge mnafanya nini huko maana yake kinachotoka ni kama kimetoka London. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hayo yote nashukuru naunga mkono hoja ahsante sana. (Makofi)