Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Vedastus Mathayo Manyinyi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Musoma Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. VEDASTUS M. MANYINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante; nikushukuru kwa kuweza kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia katika hii hotuba ya bajeti ya Waziri Mpango.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais pamoja na timu yake kwa ujumla; kusema kweli wanafanyakazi nzuri na ni kazi yenye kutukuka. Mimi nikuombe tu Waziri Mpango kwamba mnapoona kule upande wa pili wanajaribu kubeza haya mafanikio wanabeza tu kwa sababu ni utaratibu kwamba lazima wazungumze. Kusema kweli kazi ambayo mnaifanya ni kazi nzuri ni kazi ambayo inawapa matumaini makubwa Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, labda mimi ninachoweza kusema katika mchango wangu; ni kweli kwamba pamoja na maendeleo yote ambayo yanafanyika lakini Watanzania wangependa kuona huko kukua kwa uchumi kukiwa kunaonekana katika maisha ya kawaida ya watu. Kama hivyo ndivyo labda mimi nichangie tu katika maeneo machache ambayo tunaweza kuyafanya katika mpango wa muda mfupi, mengine tukaweka kwenye mpango wa muda wa kati, na mengine tukayaweka kwenye mpango wa muda mrefu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikianza na mpango wa elimu, nakumbuka mwezi uliopita Mheshimiwa Rais alienda Malawi, akaenda Afrika Kusini, akaenda pamoja na Namibia. Pamoja na mambo mengine aliyokuwa anayazungumzia lakini alikuwa anasisitiza zaidi kuona namna ya kuboresha au Kiswahili kuwa lugha ya Afrika.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo Mheshimiwa Waziri unaweza ukatenga kiasi kidogo cha fedha na kiasi hicho ukakipeleka kwenye ofisi zetu za Ubalozi zile ofisi za Ubalozi zile tukatengeneza tu crash program kwa ajili ya walimu wanaofundisha Kiswahili wakawa na vyumba pale kwenye Ubalozi wetu. Kiswahili ambacho nchi zetu za Afrika wanahitaji kufundishwa ni kile cha kujua kusoma na kuandika. Sasa hii crash program inaweza ikawa inaanza asubuhi mpaka jioni. Kwa hiyo utajikuta kwamba yale mataifa mengine wanaotaka kujifunza Kiswahili wanajiandikisha pale ubalozini, na walimu wetu wako pale na wanawafundisha. Kwa hiyo tutajikuta kwamba mambo mawili tutayafanikisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza, tutakuwa tumepata ajira kwa ajili ya walimu wetu kwa ajili ya mpango wa muda mfupi, lakini la pili tutakuwa tumepata mapato. Hilo nalisema; leo ukienda pale British Council pale Posta pale, unakuta unakuta pale Serikali ya Uingereza imeanzisha mfumo huo na kila siku zaidi ya wanafunzi 200 wanapata pale elimu na kwamba wale wanaotaka kujifunza Kiingereza wanajifunza, lakini vile vile Serikali yao inapata kipato.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tunadhani kwamba pamoja na mpango wa muda mrefu, lakini naamini kwamba huo ni mpango wa muda mfupi ambao Mheshimiwa Mpango ukiuamua leo tayari ndani ya miezi miwili ni zoezi linaloweza kufanyika na tayari watu wetu wakapata maisha, na mambo yakaendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo nilipenda nichangie, katika kukuza ajira; maana mojawapo ya kazi yoyote ile ya Serikali, pamoja na mambo mengine lakini ni pamoja na ku-create ajira kwa wananchi wake. Leo ukiangalia tunao vijana wengi wa Kitanzania hawana ajira. Sasa kwenye upande wa kilimo kinaweza kikachukua watu wengi zaidi katika kuwasaidia wakajipatia ajira.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo mojawapo Serikali imeanzisha mpango mzuri wa kuchukua vijana wanaojiunga na Jeshi la Kujenga Taifa kwa kipindi cha miaka miwili. Hivi sasa kuna in-take ambayo sasa nadhani kama sikosei huu inaelekea mwaka wa tatu. Mimi ushauri wangu ni kwamba, wale vijana pamoja na kazi zingine wajikite zaidi kwenye uzalishaji wa kilimo.

Mheshimiwa Naibu Spika, na hili suala la JKT kwanza ni vizuri likawepo katika kila mkoa, na kulekule wakachagua mazao. Pia tusikalie tu yale mazao ambayo tunasubiri soko la dunia liseme, yako mazao ambayo tunaweza kuyauzia katika nchi zetu hizi za Afrika. Kwa mfano leo tukilima zao kama la mpunga tunaweza kuuza Kenya, Uganda Rwanda na Zambia. Kwa hiyo basi kama hivyo ndivyo hawa vijana hawa, badala ya kuwaingiza JKT miaka miwili halafu tukawaondoa ni vizuri wakatumia muda mwingi wakazalisha na wakapata mtaji na kwa hiyo tunapowaondoa wawe wamejifunza maisha ya kijeshi lakini vile vile sasa tuwape mitaji ili wakaendelee na maisha yao. Kwa hiyo nadhani hii ni nafasi nzuri ya kuwatumia wale vijana ili waweze kujipatia ajira lakini vile vile waweze kujipatia kipato.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama hiyo haitoshi hata leo ukija kwenye mifugo; katika nchi hii tunayo mapori mengi tena ni ranch za Serikali. Kwenye zile ranch leo ukienda ni miti tu inakua kiasi kwamba hata mifugo haiwezi kuchungwa. Kwa hiyo zile ranch zile tukizitumia vizuri; na tunaweza kuzitumia vizuri kwa maana ya kuzikodisha; na katika kuzikodisha leo Watanzania wengi wanayo mifugo, wengi wanafuga lakini hawana mahala pa kufugia. Kwa hiyo zile ranch zile tukizikatakata vipande na Serikali ikawakodishia wananchi, watanenepesha mifugo yao humo na baada ya kunenepesha ile mifugo, tunayo masoko makubwa; kule Comoro kuna soko kubwa sana la mifugo, kule Uarabuni nako soko ni kubwa. Shida moja tu ni kwamba Watanzania wengi hawana mahala pa kufugia mifugo yao, kwa maana ya kunenepesha ili waweze kuuza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ndiyo maana wakati mwingine tunalalamika au watu wetu wanalalamika wanasema uchumi mgumu kwa sababu tu kwamba kuna maeneo ambayo yangeweza kuwachukua ku- accommodate watu wengi lakini hizo fursa wanashindwa kuzipata. Kwa hiyo,naamini kwamba tukitumia na hiyo nayo itawasaidia sana Watanzania wengi kuweza kujipatia uchumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ni eneo la uvuvi, ambalo nalo; leo ukiangalia samaki kama sato wanatakiwa kila mahali lakini uwezo wetu wa ku-supply ni mdogo. Kwa hiyo nadhani kwamba haya ni baadhi ya maeneo ambayo leo tukiyasimamia vizuri, yataleta matokeo ya haraka. Baada ya kusema hayo, nakushukuru sana naunga mkono hoja. (Makofi)