Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Rashid Mohamed Chuachua

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Masasi Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. DKT. RASHID M. CHUACHUA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi name niweze kuchangia mapendekezo ya bajeti kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2019/2020. Nami nianze kwa kuunga mkono hoja hii iliyopo mbele yetu na kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuisimamia Serikali yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nampongeza sana Mheshimiwa Waziri Dkt. Mpango pamoja na Naibu Waziri na Watendaji wote wa Wizara ya Fedha kwa kazi kubwa waliyoifanya ya kutengeneza mapendekezo haya ambayo kwa kiasi kikubwa yanakwenda kuipeleka Tanzania mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Serikali kwa usikivu, kwa kusikiliza maoni ya baadhi ya Waheshimiwa Wabunge na maelekezo yao pamoja na maoni yaliyokuwa yanayotolewa kwenye Kamati za kisekta, maoni ambayo yalikuwa yanakusudia kuijenga Tanzania kwenye mwelekeo wa kiuchumi unaofaa. Bajeti hii imeonyesha kupokea kwa kiwango kikubwa maoni hayo na kuyafanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme kwamba Serikali ilikuwa haijachelewa kupokea maoni haya kwa sababu tungeshangaa sana kama Serikali isingejipa muda wa kuyatafakari na kutathmini kabla ya kuyapokea. Kwa hiyo, tunaipongeza sana Serikali yetu kwa kazi kubwa waliyoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti hii iko karibu sana na wafanyabishara wakubwa, lakini ipo karibu sana na wafanyabiashara wa kati, pamoja na wafanyabiashara wadogo na hata wajasilimali. Hii ni bajeti ambayo inakwenda kusukuma mbele mapinduzi ya viwanda na kujenga msingi wa kwenda vizuri kwenye Serikali ya Chama cha Mapinduzi ya Awamu wa Sita. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wapo wanaosema Sera yetu ya Viwanda haitekelezeki kwa sababu pengine eti hatuna malighafi za kutosha. Hili siyo suala la kweli hata kidogo. Ukiangalia malighafi ambazo zipo katika Sekta ya Kilimo tu, ni nyingi na toshelevu kuliko uwezo wa viwanda vyetu vya ndani wa kuzichakata malighafi hizo. Ukiacha katika maeneo mengine, lakini tuna tumbaku ya kutosha. Je, tunao uwezo wa kusindika tumbaku yetu yote? Tunalima korosho, tunavuna korosho zaidi ya tani 250,000, hatuna uwezo hata wa kuchakata robo ya korosho tunayovuna.

Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania ni nchi ya sita Afrika katika kilimo cha muhogo. Inakadiriwa kwamba tunavuna muhogo zaidi ya metric tani tano kwa mwaka. Ni kiasi gani cha muhogo tunakichakata katika viwanda vyetu?

Mheshimiwa Naibu Spika, nayasema haya huku nikiwa na uhakika kwamba Tanzania tunalima sana nazi, lakini ni kwa kiwango gani mazao yanayotokana na nazi tumeweza kuyachakata kwenye viwanda vyetu? Hii ina maana kwamba, tuko vizuri katika malighafi, lakini pia tuna fursa pana bado ya kuendeleza Sekta ya Viwanda. Hata hivyo, hakuna nchi ambayo inajitosheleza katika malighafi zake zote, ndiyo maana tuna-export na tuna-import malighafi na kuzipeleka pia nje kwa ajili ya kupata fedha za kigeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninayo maoni ambayo pengine yakichanganywa na maoni mengine ya Bunge yaliyotolewa katika kuimarisha Sekta ya Viwanda basi tunaweza tukapiga hatua. Maoni haya yanaweza yakaongeza pato la Taifa, lakini pia yanaweza kuongoze ajira katika nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza ambalo nadhani ni jambo muhimu, ni kuendelea kukaa chini na kuondoa changamoto zote za kikodi na kitozo ambazo zinaonekana kuwakwaza wawekezaji. Hili ni jambo la msingi sana. Tunaona Serikali imepiga hatua, kwanza kwa kutuletea mapendekezo yaliyopo kwenye mapendekezo ya bajeti, lakini pia mpango wake wa kutengeneza mazingira wezeshi ambao unapangwa sasa kupitia blue print, nina imani tunakwenda vizuri katika kuhakikisha kwamba tunasonga mbele kwenye uchumi wa viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo ni muhimu, ni lazima kuwe na mkakati unaotekelezeka wa kufanya uwekezaji katika maeneo ambayo tayari kama nchi na mikoa mingine yote imeitikia wito kwa kutenga maeneo kwa ajili ya uwekezaji. Tunazo kanda za kiuchumi, lakini pia tunayo maeneo ya EPZA ambayo kimsingi bado uwekezaji haujafanyika kwa kiwango kinachoridhisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda katika Mikoa ya Kusini, kwa mfano, katika Mkoa wetu wa Mtwara, utaona kuna eneo kubwa limetengwa kwa ajili ya uwekezaji na wananchi wameshalipwa fidia zao, lakini uwekezaji bado haujafanyika. Hivyo, kuna jitihada za makusudi zinazohitajika kufanywa na Serikali ili uwekezaji katika eneo la viwanda uendelee kufanyika katika maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, naona kuna ushauri mwingine, hebu tuangalie ni kwa kiwango gani Sera yetu ya Viwanda kama nchi inafungamana na kuchangamana na sera za viwanda za nchi nyingine ambazo ni jumuiya za kiuchuni. Ni namna gani sera yetu ya viwanda inachangamana na kufungamana na sera ya viwanda katika nchi za Afrika ya Mashariki; katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara; nchi za SADC; katika Kanda za Kimataifa na hata nje ya Bara la Afrika? Ni namna gani sera yetu ya viwanda inafungamana na sera za nchi hizo? Hili ni jambo la msingi sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, lipo jambo lingine, hebu tuone ni namna gani Serikali inasimamia kikamilifu namna ambavyo soko la ndani na soko la nje la bidhaa zetu zitakuwa ni za kiushindani ili tuweze kuuza bidhaa zetu nje na katika jumuiya hizo nilizozitaja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lipo jambo lingine, nalo ni jambo muhimu sana katika kuliangalia. Ni vema Serikali ikaendelea kusimamia matumizi ya teknolojia ya kisasa katika viwanda vyetu. Hili nalo linaweza likawa ni changamoto kubwa. Ili tuendelee kuimarisha Sekta ya Viwanda na kuongeza pato la Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mambo mengine haya yakifanyika, ninayo imani kwamba tutasonga mbele katika suala letu la kusukuma maendeleo ya uchumi wa viwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema, ni muhimu kuangalia pia namna nyingine tunavyoweza kuwekeza katika maeneo mbalimbali. Katika upwa wa Pwani ya Bahari ya Hindi, hususan katika Mkoa wa Mtwara na hata katika Mkoa wa Lindi, hatuna hata kiwanda kimoja ambacho kinachakata mazao ya bahari, tungependa uwekezaji uliangalie eneo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia katika Mkoa wa Mtwara tuna gesi na miongoni mwa mazao ya gesi ni mbolea inayoweza kutengenezwa. Tungependa Serikali ione ni namna gani sasa tunaweza kujenga kiwanda cha mbolea katika Mkoa wa Mtwara ili kusukuma mbele maendeleo na mapinduzi ya kilimo kwa kuongeza uzalishaji wa mbolea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mapendekezo ya bajeti yameeleza pia namna mabavyo Serikali imefanya kazi ya kuhakikisha inalipa madeni na malimbikizo au madai na malimbikizo katika mapendekezo yaliyopendekezwa na Serikali. Katika bajeti iliyopita, Waziri ameonyesha ni namna gani madai hayo pamoja na malimbikizo yamekuwa yakilipwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2015/2016 kuna wafanyabiashara walisambaza pembejeo. Kama ikiwa pembejeo walizosambaza zimeshahakikiwa, basi tunamwomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango achukue hatua ya kuwalipa wafanyabiashara hawa. Ni miaka minne sasa, uhakiki unaendelea. Kwa kweli inasikitisha sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2017/2018 wajasiriamali wadogo wadogo walipewa majukumu ya kuzalisha miche kwa ajili ya kusambaza kwa wakulima wa korosho. Wajasiriamali hawa wengi walikopa benki na wengine walikopa hata kwenye Halmashauri yangu ili kuhakikisha kwamba wanapata fedha na kutengeneza vitalu vya kusambaza miche. Mpaka leo tunavyozungmza, watu hawa bado hawajalipwa. Ni nini kinachosababisha wasilipwe? Watahakikiwa mpaka lini?

Mheshimiwa Naibu Spika, ni vema kama mtu hata kama alizalisha mche mmoja, alipwe kwa haki yake, lakini alipwe kitu ambacho kwa kweli anastahili kulipwa. Wananchi hawa wana malalamiko makuwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunakwenda kwenye uchumi wa viwanda. Uchumi wa viwanda tunaokwenda nao ni lazima kusukuma mbele uzalishaji wa umeme. Tunaipongeza Serikali, kwa mradi mkubwa wa kielelezo wa Stiegler’s Gorge, lakini kama walivyosema Waheshimiwa Wabunge wengine, sisi pia tuna mategemeo makubwa katika maeneo yetu kuhusu usambazaji wa umeme wa REA. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lipo tatizo kubwa la kasi ya usambazaji wa umeme huu. Nilichangia katika Wizara ya Nishati na leo narudia, nazungumza kwamba, katika mikoa ambayo ina vijiji vingi havijafikiwa na umeme, ni Mkoa wa Mtwara na Mkoa wa Lindi. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. DKT. RASHID M. CHUACHUA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)