Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Kiteto Zawadi Koshuma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. KITETO Z. KOSHUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii, pia naomba nimshukuru sana Mungu kwa kuendelea kunipa afya njema ili niendele kutoa michango yangu katika Bunge hili Tukufu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa naomba nitoe salamu za pongezi kwa Serikali. Naomba kuanza kwa kuipongeza Serikali kwa namna ambavyo wameweza kuleta upanuzi wa uwanja wa ndege wa Mwanza, tumeuona watu wote tumekuwa tukisafiri na tunaona uwanja wa ndege wa Mwanza kwa hali ambayo ulikuwa nayo lakini Serikali imewekeza pesa pale na kuweza kufanya upanuzi wa uwanja ule wa ndege wa Mwanza.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia naipongeza Seriakli kwa sababu imeweza kuwalipa fidia wananchi ambao walikuwa wana migogoro na Jeshi katika maeneo ya Lukobe na maeneo mengine ambayo walikuwa na migogoro katika Mkoa wa Mwanza. Tunaipongeza sana Serikali kwa sababu tumekuwa tukiiomba sana kuwalipa fidia wananchi hawa ambao wamekuwa wakiingia kwenye migogoro na Jeshi. Pia naomba kuiomba Serikali waendelee kutusaidia kuwalipa fidia wananchi ambao wapo katika uwanja wa ndege ambao unapanuliwa. Wawalipe fidia wananchi hawa ili kuweza kuepusha migogoro inayoendelea katika upanuzi ule wa uwanja wa ndege na kutufanya, kama wananchi wa Mkoa wa Mwanza au Wabunge wa Mkoa wa Mwanza kupunguza kura zetu. Ninaamini kwamba Serikali ni sikivu na itaweza kulisikia hilo na kulifanyiakazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kutoa salamu hizo za pongezi, naomba sasa kuendelea kuipongeza Serikali kuhusiana na suala la hoja iliyoko mbele yetu ya Bajeti Kuu ya Serikali. Bajeti hii kama hatutatoa pongezi kwa Serikali kwa namna ambavyo imejitahdii kuhakikisha kwamba inazifanyia kazi changamoto mbalimbali ambazo zimekuwa zikitolewa mara kadhaa katika Bunge hili na Wabunge wa Bunge hili tutakuwa hatujaitendea haki Serikali. Wanasema ‘mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni’ name sina budi kuipongeza Serikali kwa sababu bajeti hii ambayo iko mbele yetu tunaijadili siku hii ya leo imezitatua changamoto mbalimbali za kodi lakini pamoja na tozo mbalimbali ambazo zimekuwa ni kero pamoja na yote wameendelea kuhakikisha kwamba wanaweka mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara wote walio wakubwa, wa kati pamoja na wafanyabiashara wadogo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, siipongezi tu hivi mtu anaweza akadhani ninapongeza pasipokuwa na evidence. Ukiangalia Serikali imeweza kufanya marekebisho ya ulipaji wa kodi mbalimbali. Wamepunguza ulipaji wa kodi kutoka kiwango cha shilingi 150,000 hadi shilingi 100,000 lakini pia wamepunguza malipo ya kodi kutoa 318,000 hadi 135,000. Waheshimiwa Wabunge mkiangalia ukurasa wa 41 hadi ukurasa wa 42 mtaona ni namna gani Serikali imeweza kuingatia ushauri ambao umekuwa ukitolewa na Waheshimiwa Wabunge.

Mheshimiwa Naibu Spika, siishii hapo; katika miaka mitatu mfululizo ndani ya Bunge hili nimekuwa nikiishauri Serikali mara kwa mara kuhakikisha kwamba wale wafanyabiashara ambao wanaanza biashara zao wasitozwe kodi kabla hawajaanza biashara. Kwa nini nisiipongeze Serikali kama imeweza kuyachukua maoni yale na kuweza kuyafanyiakazi kwa kufanya marekebisho ya Sheria na kuhakikisha wkamba inatoa tax holiday kwa wale wafanyabiashara ndani ya miezi sita kama unaanza biashara yako unapewa unafuu wa kutokulipa kodi hadi baada ya miezi sita ina maana kwamba baada ya miezi sita ukiwa kama mfanya biashara unaweza kuwa umekwishakufahamu kuwa biashara yako ina mtiririko gani, unapata faida ama unapata hasara, pamoja na hapo utaweza kukadiriwa kodi vizuri na hiyo itasababisha wafanyabiashara wengi kulipa kodi kwa hiari bila kukwepa kulipa kodi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kuipongeza bajeti hii ya Serikali, tumekuwa na changamoto mbalimbali pia ambazo zinatokea. Bajeti hii ina changamoto kubwa moja ambayo inawagusa Wanawake wa Tanzania. Nikiwa kama Mbunge ambae nawakilisha Wanawake wa Tanzania nitakuwa sijawatendea haki wale ambao ninawawakilisha hawana uwezo wa kuja kuyasema haya ndani ya Bunge hili bali wametuma wawakilishi wao, kama sitawasema nitakuwa sijawatendea haki.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti hii imeonesha kutokuwa na gender responsive, kwa sababu gani nasema hivyo? Kuna suala la Serikali ukiangalia pale katika ukurasa wa 34 wamefuta msamaha wa kodi la ongezeko la thamani katika taulo za kike. Suala la kufuta msamaha huu kwa kweli kama Wanawake wawakilishi ndani ya Bunge hili hatujalielewa suala hili, ni kwa nini Serikali imekuja na wazo hili, walikaa wakafikiria nini. Ukiangalia suala la taulo hizi za kike hazitumiwi tu na watoto au wanafunzi ambao wako mashuleni bali zinatumiwa na asilimia kubwa sana ya Watanzania ambao ni wanawake. Wanatumia watoto wa kike, wanatumia akinamama ambao wametoka kujifungua.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kujifungua mwanamama anahitaji kutumia taulo za kike ndani ya siku 14 au zaidi kwa hiyo Serikali ilipokuwa imetoa msamaha wa kodi ya ongezeko la thamani katika taulo hizi za kike walitarajia na walikuwa wana nia njema na tuliwapongeza kwamba walikuwa wana nia njema ya kuhakikisha kwamba kunakuwa kuna unafuu wa gharama katika kununua taulo hizi za kile lakini kwa bahari mbaya sana suala ambalo Serikali na wananchi tulilitarajia halikutokea lakini Serikali imekuja na kusema kwamba wanaondoa tena ule msamaha wa kodi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi kama Mbunge nimekuwa nikijiuliza, Serikali ina mkono mrefu. Wajibu mmojawapo wa Serikali ni kuhakikisha kwamba wana- regulate bei ya bidhaa zinapokuwa zipo sokoni. Kama Serikali inaweza leo hii sukari ikapanda bei Serikali ikatia mkono wake, ikatoa kauli yake, kutoa bei elekezi ya sukari ili kila mwananchi aweze ku-afford kununua sukari, vipi kuhusiana na taulo za kike suala ambalo linawagusa wananchi karibu asilimia 50 ambao ni wanawake?

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali baada ya kuwa wametoa ule msamaha, wameshindwa vipi kuhakikisha kwamba wana-monitor suala la ongezeko au punguzo la bei? Serikali imeshindwa vipi kukaa na wafanyabiashara hawa kuwaambia kwamba tumetoa msamaha wa kodi tunaomba mpunguze bei na kuwapa bei elekezi kuwa kiasi kadhaa?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa hivi taulo hizi za kike zinanunuliwa kwa gharama ya Sh.2000 hadi Sh.3500, hiyo ni gharama kubwa sana. Kwa Mtanzania tu wa hali ya kawaida hawezi kununua taulo hizi za kike. Ndiyo maana tukaitaka Serikali kutusaidia na ndiyo maana na wenyewe wakatoa msamaha huo wa kodi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali irudi tena mezani iangalie suala hili linawezekana kwa sababu limekuwa likiwezekana kwenye bidhaa zingine kama vile petroli, sukari, Serikali imekuwa ikiweka mkono wake, kwa nini Serikali isitusaidie sisi wanawake? Mnataka mpaka wanawake wote wa Bunge hili tugome pamoja na wanaume naamini watanisaidia kwa sababu wao ndiyo wanunuzi wa taulo hizi za kike. Hatuzinunui sisi wenyewe, akina baba hawa ndiyo wanaozinunua hizo taulo za kike. Ina maana mwanaume kama yupo ndani ya nyumba ana mke wake ambaye ndio mama, watoto wa kike watano, ndugu, jamaa na marafiki anaishi nao mule ndani ya nyumba ambao ni wanawake, mwanaume si ndiye anayenunua? Kwa hiyo, leo nikisema wanawake tuanzishe mgomo kwa ajili ya suala hili, naamini wanaume watatuunga mkono na tutaweza kufanikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hatutaki kufika huko kwa sababu tunaamini kwamba Serikali hii ni sikivu. Kama imekuwa ikiyasikia maoni mbalimbali ya Waheshimiwa Wabunge na kuyatafakari na kuyafanyia kazi, naamini hata hili haliwashindi wanaweza wakalitafakari na wakalifanyia kazi. Huo ndiyo ushauri wangu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kutoa ushauri huo, pia naomba niishauri Serikali kwamba vipo viwanda vyetu, kwa mfano kuna Kiwanda cha cha MSD, Mkoa wa Pwani, pia kuna kiwanda kingine cha madawa Mkoani Simiyu, naishauri Serikali ivielekeze viwanda hivi kuanzisha production line ya hizi taulo za kike. Hiyo itasaidia taulo hizi kupatikana ndani ya nchi na hivyo kuleta unafuu wa bei na wananchi wanaweza wakazifikia kwa urahisi zaidi. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)