Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Ritta Enespher Kabati

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na kuunga mkono hoja kwa asilimia mia moja na nimpongeze Waziri wa Fedha, Dkt. Mpango, Naibu Waziri Dkt Kijaji, Katibu Mkuu na watendaji wote wa Wizara kwa kazi nzuri na kuwasilisha bajeti na taarifa ya hali ya uchumi wa Taifa hapa Bungeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitakuwa sijatenda haki kama nitakuwa sijampongeza Mheshimiwa Rais wetu Dkt John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri sana. Kwa kipindi kifupi ameweza kusimamia ukamilishwaji wa miradi mikubwa sana ya maendeleo. Pia kwa kikao kizuri sana alichokifanya tarehe 7/6/2019 Ikulu na wawekezaji na wafanyakazi nchini. Mheshimiwa Rais ameonyesha jinsi anavyoweka kipaumbele katika kuchochea uwekezaji nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, nipongeze Serikali pia kwa kuona umuhimu wa kusikiliza kero na kuondoa tozo 54 za kodi mbalimbali, lakini pia Serikali iangalie mwingiliano wa majukumu ya taasisi au mamlaka za udhibiti kama TBS, TFDA na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali iangalie kuhusu madai ya watoa huduma kwa Serikali yanachukua muda mrefu kulipwa wakati wazabuni hao pia wanatakiwa kulipa kodi zao Serikalini kwa wakati.

(i) Kwa nini kusiwepo na utaratibu wa kubadilishana madeni, yaani Serikali ichukue kodi yake inayodai wazabuni kutoka kwenye deni inayodaiwa na mzabuni, hivyo kupunguza mzigo wa kulipa pesa ambayo mzabuni bado hajalipwa.

(ii) Mtoa huduma anapotoa huduma kwa taasisi zikiwemo zile za Serikali anatakiwa aambatanishe invoice yake ya madai na receipt ya EFD hii ikiwa na kuwa analipa kodi ya VAT hata kabla ya kupata malipo husika. Kwa nini EFD isitolewe pale tu malipo ya huduma yanapofanyika na si wakati wa madai yanapowasilishwa ikiwa na maana ni kwa malipo ya huduma kwa yanayochelewa kulipwa? Hivyo huathiri mitaji ya mfanyabiashara na kuanguka kwa biashara hizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ipo miradi ambayo ni ya kimkakati lakini Serikali inachelewesha kupeleka pesa na kusababisha gharama za miradi kuongezeka kwa kiasi kikubwa sana mfano, katika Mkoa wa Iringa upo mradi wa machinjio ya kisasa, mradi huo una zaidi ya miaka 10 toka uanzishwe na mradi huu kama ungekamilika kwa wakati ungeweza kuwa ni chanzo kizuri sana cha mapato katika Halmashauri yetu na ni mradi ambao ungetengeneza ajira zaidi ya 200 kwa wananchi wa Iringa. Ni kwa nini Serikali isifanye upembuzi yakinifu wa miradi kama hii nchi nzima na kuipatia fedha ili halmashauri zetu ziweze kujiendesha?

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaelekea katika uchumi wa viwanda nchini lakini barabara nyingi bado wakati wa kipindi cha masika hazipitiki kabisa. Ni kwa nini Serikali isifanye upembuzi yakinifu wa barabara zote za kiuchumi ili itoe kipaumbele kutokana na bajeti finyu ya TARURA zihudumiwe na TANROAD. Kwa mfano, Mkoa wetu wa Iringa karibu barabara zote wakati wa masika hazipitiki kabisa na kusababisha magari makubwa yanayobeba mazao ya misitu kukwama karibu siku tano mpaka saba au zaidi na kuleta athari kubwa sana za kiuchumi. Pia mkoa wetu unategemewa hata kuwa na malighafi za viwanda na wakulima wanashindwa kufikisha sokoni mazao kama njegere, mahindi, vitunguu, nyanya, viazi na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.