Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Juma Othman Hija

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tumbatu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. JUMA OTHMAN HIJA: Mheshimiwa Naibu Spika, nachukua nafasi hii kukushuKuru wewe kwa kunipatia nafasi hii ya kutoa mchango wangu katika Hotuba ya Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka 2019/2020. Pia niwapongeze Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri pamoja na watendaji wake wote kwa kuandika na hatimaye kuwasilisha kwa ufasaha mkubwa katika Bunge letu Tukufu.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuunga mkono hoja hii kwa sababu zifuatazo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Bajeti hii ni bajeti ya matumaini sana kwa wananchi wote wa Tanzania. Bajeti hii inatoa ufafanuzi mzuri juu ya kupunguza umaskini katika nchi yetu. Hii inatokana na kuangalia mahitaji ya raia maskini yamezingatiwa kwa rasilimali za Serikali. Kodi zote zinazoidhinishwa kwenye mpango huu zinawajenga zaidi maskini badala ya kuwalemaza. Wananchi wana matumaini makubwa na bajeti hii kwa kuwa Serikali imeangalia katika maeneo ya biashara na uwekezaji katika kuimarisha nafasi zote zitakazojitokeza. Bajeti hii imeakisi maisha ya kila Mtanzania mwenye ndoto ya kufikia kilele cha mafanikio. Hizo ndio miongoni mwa sababu zinazonisukuma niunge mkono hoja hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushirikishwaji wa wadau katika kuandaa bajeti hii; katika hitimisho lake Mheshimiwa Waziri ametaja wadau ambao amewashirikisha katika kuandaa bajeti hii. Hili ni jambo jema sana. Ushauri wangu katika suala hili ni kuiomba Serikali kwa bajeti zinazofuatana kuwashirikisha Mabalozi wetu wanaotuwakilisha katika nchi za nje. Hili ni kundi muhimu sana katika nchi yetu ambalo lina uelewa mzuri (exposure) katika nchi inazotuwakilisha. Wanaweza kutumia uzoefu wa bajeti za nchi wanazotuwakilisha na kuuleta kwa matumizi ya bajeti ya nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, vyanzo vya mapato; Mheshimiwa Waziri ameeleza vyanzo vingi vya mapato ambavyo miongoni mwao ni tegemezi, lakini tuna vyanzo ndani ya nchi yetu ambavyo kama tukiviboresha vitaweza kutoa mchango mkubwa sana, mfano ni Bandari bubu.

Mheshimiwa Naibu Spika, bandari hizi zinaitwa bubu kwa kukosa huduma muhimu za wafanyakazi. Ikiwa Serikali itaweza kupeleka Maafisa wa Mamlaka ya Bandari na maofisa wa TRA, bandari hizi zitabadilika kuwa bubu na kuwa bandari official na zitaweza kutoa mchango mkubwa katika nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.