Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Masoud Abdalla Salim

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Mtambile

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu Subhana Wataala aliyetulia uzima na afya nje ilikuwa bado siku 25 kufika mwezi mtukufu wa Ramadhan tumwombe Mwenyezi Mungu atufikishe salama wasalumini, tumwombe Mwenyezi Mungu atuepushe na janga la Corona ambalo linatukabili na sisi ni rai kwa watu wote duniani na watanzania rai yangu tuachaneni na dhambi ambazo zinamchukiza Mwenyezi Mungu tupunguzeni madhambi. Rai yangu kwa watanzania wote kwa imani na dini zote tuacheni dhambi dunia imebadilika, dunia imesimama.

Mheshimiwa Spika, baada ya hayo, machache sasa nianze kuchangia. Niendelee na mwenzangu alipomalizia kuhusu Corona. Ni vyema mkakati ukaongezwa zaidi kupambana na Corona na inaonekana vitakasa mikono (sanitizers), bei zake sasa zimekuwa zikiongezeka siku hadi siku. Ile ambayo ilikuwa inauzwa 1,500 kabla ya Corona sasa inauzwa 3,000 hadi 2,500 na ile ya 2,500 sasa ni 4,500 hadi 5,000. Ni ushauri wangu kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu kwamba jambo hili ni jambo kubwa, Serikali haziko vijijini, elimu hakuna vijijini, viziba midomo navyo bei zimepanda. Niombe Serikali iingilie kati suala hili tuone kwamba tunafanyaje.

Mheshimiwa Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri Mkuu, bajeti yake mimi sina pingamizi nayo sana. Katika bilioni zake ambazo zimetajwa tumpitishie ila kwa sababu yeye ana Mafungu tisa, sina pingamizi na Fungu 15 lakini pingamizi yangu iko na Fungu 27; Registrar of Political Parties (Msajili wa Vyama vya Siasa). Shida yangu iko kwenye Fungu 61 - Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Fungu 41, Fungu 42 sina wasiwasi nalo, Mafungu 91, 92, 65, Mafungu yote tisa ambayo Waziri Mkuu anasimamia sina mapingamizi nayo, lakini Fungu 27 - Registrar of Political Parties; na Fungu 61 - Tume ya Taifa ya Uchaguzi, ni shida. Nasema hayo kwa sababu zifuatazo:-

Mheshimiwa Spika, Msajili wa Vyama vya Siasa yeye ni mlezi. Ningependa kuona kwamba Msajili huyu anakwenda vizuri na kuona kwamba vyama vyote ni sawasawa na sote ni Watanzania, lakini akitokea kiongozi yeyote akianza kutoa matamshi ya uchochezi akisema kwamba tutashika dola mwaka huu kwa kutumia dola, tafsiri si nzuri. Hata vyovyote ambavyo yeye amekusudia lakini haijengi taswira nzuri ya ulinzi na usalama, si jambo jema sana.

Mheshimiwa Spika, si muda mrefu umesema hapana, mambo haya si mazuri, hotuba hii si nzuri, hii si nzuri, lakini mtu anasema tutashika dola kwa kutumia dola na nchi ambayo haikutumia dola kama vile KANU ikaondoka, hatufanyi kosa hilo; why? Mambo gani hayo? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kiongozi mkuu yeye haipaswi, mimi ningetarajia Msajili amuite amtake atoe maelezo kwa sababu vyama vingine vya Upinzani viongozi wakisema maneno mengine wanaitwa wanahojiwa wamekusudia nini, lakini sisi wapinzani tunaonekana kama vile sijui watu gani tumetoka nchi gani. Ushauri wangu kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu, ushauri wangu viongozi kama hawa muanze kuwafanyia utafiti; ni kweli? Stori ni za kweli? Maana yake wana uchungu kweli na nchi hii? Ni shida.

Mheshimiwa Spika, Tume ya Taifa ya Uchaguzi; Mheshimiwa Waziri Mkuu wakati anatoa hotuba yake ambayo ni nzuri sana na alisema kwamba tunakwenda kwenye Uchaguzi Mkuu na utakuwa huru na haki, lakini jambo la kwanza kabisa uchaguzi huru na wa haki ni Tume huru ya Uchaguzi. Tume huru ya Uchaguzi ni muhimu sana, kuanzia uandikishaji, tunakwenda kwenye kampeni, kwenye kupiga kura, kwenye kutangaza matokeo, lazima Tume ya Taifa ya Uchaguzi ifanye kazi yake kwa uadilifu mkubwa sana, vinginevyo kama hatutakuwa na Tume huru ya Uchaguzi uchaguzi hauwezi kuwa huru na wa haki tunaweza tukapelekana tena mahali ambapo sio pazuri sana.

Mheshimiwa Spika, nimwombe Mheshimiwa Waziri Mkuu awe makini sana na uchaguzi wa mwaka 2020. Kenya wana kitu kinaitwa IEBC (Independent Electoral and Boundaries Commission), uchaguzi wa Kenya huo. Kuna hofu gani kuwekwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi? Tuige nchi jirani tu Kenya mipaka hii hapa.

Mheshimiwa Spika, nasema hivyo kwa uzoefu. Mimi nilikuwa mmoja wa Wasimamizi wa Uchaguzi wa Kenya, mimi nilikuwa Busia na Bungoma katika kaunti hizo, majimbo 16. Sasa kuna jambo gani? Nasema kwamba tubadilike tuone kwamba tunakwenda vizuri tuone kwamba kwa vyovyote iwavyo tunapata utambuzi zaidi.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu, lakini kwenye suala la Corona kuna jambo moja; mgonjwa kuthibitika kama ana Corona uthibitisho wake uko eneo moja tu la Hospitali ya Muhimbili peke yake. Mikoa yote hakuna kipimo hicho mpaka sampuli ipelekwe Muhimbili iende ikachunguzwe baada ya hapo ndipo inakuwa imethibitika kama mgonjwa huyo tayari ana maradhi ya Corona. Ushauri wangu; tuandae mazingira sasa angalau kila mkoa; tuna mikoa 32, sampuli ichukuliwe Kagera ipelekwe Dar es Salaam, kwa Wapemba wenzangu huko Dar es Salaam. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, hili liangaliwe. Ni jambo kubwa kwelikweli, kujua afya zetu wakati huu ni muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niendelee, jambo lingine ambalo napenda niendelee ni suala zima la msongamano wa wafungwa. Amesema Mheshimiwa Mbunge mmoja hapa; suala la msongamano wa wafungwa linachangiwa na mambo mengi lakini mpaka sasa Bunge letu limeshindwa kuweka ukomo wa upelezi. Msongamano wa wafungwa na mahabusu, mahabusu hadi sasa wanafika 17,000, wafungwa 15,000 jumla 32,000. Mahitaji ya magereza ni nusu tu lakini mpaka sasa sheria bado haijaweka wazi ukomo wa upelelezi. Kuna watu wako magerezani miaka mitatu, wako miaka mine, wako miaka mitano, wako miaka sita, wako miaka saba. Ukomo wa upelelezi uko wapi? Na huyo akithibitishwa kwamba hana kosa tayari alikuwa ameshafungwa.

Mheshimiwa Spika, Bunge hili sasa, naishauri Serikali, Mheshimiwa Waziri Mkuu sina pingamizi naye sana mimi maeneo yangu ni mawili makubwa, lakini lazima Bunge hili tutoke na jambo moja kubwa; kuwepo na ukomo wa upelelezi, watu magerezani wanateseka na ni kesi za kubambikiza, kesi zingine ni za kubambikiza, watu wanateseka, watu wanaumia, watu wamepoteza imani na Serikali kwa sababu gani, muda umekuwa ni mkubwa kesi zinaendelea unaambiwa upelelezi bado haujakamilika; kwa nini?

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais mwenyewe alipita magerezani huko akasema hawa fyekelea mbali. Sisi Bunge tunashindwaje kuandaa mazingira ya kuweka ukomo wa upelelezi? Tutaendelea kuweka msongamano mkubwa, wanaendelea kula, wakati huu wa Corona sisi tuna sanitizers, wao ambao wanalala kama pipi hivi? Sisi huku tunaambiwa tukae mbalimbali Wabunge, wewe kaa kule, wewe kaa kule, wewe kaa kule; wale kule magerezani mmekwenda mkaona? Corona hii, mmekwenda mkaona? Niishauri Serikali, lazima kuwepo na ukomo wa upelelezi kwenye shughuli hizi.

Mheshimiwa Spika, baada ya maneno hayo, nashukuru sana.