Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Joseph Kizito Mhagama

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Madaba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia hotuba ya Waziri Mkuu. Kwanza nitumie nafasi hii kuipongeza sana Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Jemedari Dkt. John Pombe Magufuli na wasaidizi wake akiwemo Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kufanya kazi iliyotukuka kwa Watanzania kwa miaka hii mitano. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu jambo kubwa ambalo limejitokeza ni dhana ya uchumi jumuishi (inclusive economy). Mfumo huu wa uchumi jumuishi ni uchumi ambao unatoa fursa kwa Watanzania wote, kwa wananchi wote kuweza kunufaika nao. Dhana hii inatofautiana na dhana ya uchumi ambao sio jumuishi (extractive economy) ambayo inawanyima fursa watu walio wengi kuweza kushiriki kwenye uchumi au kunufaika na uchumi. Unawakumbatia mabeberu wachache na mabepari, hautoi fursa kwa watu wengi na watu wa kawaida.

Mheshimiwa Spika, Serikali yetu kwa miaka hii mitano imekuwa inatekeleza dhana ya uchumi jumuishi na imekuwa inafanya hivyo kwanza kwa kujenga mazingira na miundombinu wezeshi inayomfanya kila Mtanzania aweze kushiriki na kunufaika na uchumi wa Taifa lake. Imefanya hivyo kwa kujenga miundombinu ya reli, sasa programu kubwa ya ujenzi wa reli za kisasa imeanza na hii ya SGR inayoendelea sasa ni hatua ya kwanza na naamini tutaendelea kujenga reli. Pia programu kubwa ya umeme. leo Serikali imefikia vijiji 9,001 kutoka vijiji 2,118; ni achievement kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika kutafsiri hii dhana ya uchumi shirikishi, Serikali imewekeza kwenye usafiri wa anga ili Watanzania waweze kujenga uchumi wao kwa kusafiri kwa haraka na kufanya mambo mengine ikiwemo uchumi wa utalii, lakini pia dhana hii tunaitafsiri kwenye namna ambavyo Watanzania wananufaika na ukuaji wa uchumi. Tunaona uchumi wetu unakua kwa asilimia 6.9. Kwenye maisha ya Mtanzania ananufaika nao vipi? Serikali imefanya kazi za kutukuka kwenye eneo hili. Leo tuna huduma za afya kwa kupitia vituo vya zahanati zaidi ya 1,198, Watanzania kwa maelfu wanapata huduma huko. Lakini tuna vituo vya afya, hospitali 69 mpya na hospitali za rufaa kumi, hiyo ni sehemu tu ya tafsiri ya ukuaji wa uchumi ambao umejengwa na Awamu hii ya Tano.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo nina ushauri wa mambo ya nyongeza kwa Serikali; kazi iliyofanyika ni kubwa sana, tumeona uchumi unakuwa na miundombinu inakuwa na mazingira wezeshi ya kiuchumi yanajengwa na Watanzania wananufaika na uchumi wao. Hata hivyo kuna mambo ambayo Serikali inapaswa kwenda kuyatafakari.

Mheshimiwa Spika, ukiangalia takwimu za ukuaji wa uchumi ambao tumesema unakuwa kwa asilimia 9.9, sekta zilizochangia ukuaji huo zinatofautiana kwa umuhimu lakini Sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ambayo inaajiri asilimia 64 ya Watanzania ukuaji wake ni asilimia 3.6 wakati sekta zingine ambazo zimechangia kwenye ukuaji wa uchumi wa Taifa letu kama ujenzi unakua kwa asilimia 14.8, mchango wake kwenye ajira ni asilimia 2.42.

Mheshimiwa Spika, ukiangalia uchukuzi, unakua kwa asilimia 8.8 lakini mchango wake kwenye ajira za Watanzania ni asilimia 2.94; ukiangalia huduma za usambazaji maji vijijini mchango wake kwenye ajira ni 0.05. Tafsiri yake ni nini; tafsiri yake eneo ambalo linawagusa Watanzania wengi ambao ni asilimia 64 mchango wake wa ukuaji ni mdogo sana ambao ni asilimia 3.6. Niiombe sana Serikali; dhana ya uchumi shirikishi ni kuwafikia hawa Watanzania walio wengi ambao sehemu kubwa ya maisha yao wanategemea kilimo. Nikiri, Serikali imefanya kazi kubwa kwenye kilimo, lakini kazi bado haijakwisha. Niiombe Serikali tunavyoendelea na mchakato huu wa bajeti ifikirie sasa kwenda kuwekeza zaidi kwenye kilimo.

Mheshimiwa Spika, pili, Watanzania wengi, asilimia 60 mpaka 70 wanaishi vijijini. Dhana ya uchumi shirikishi au uchumi jumuishi ni kuwawezesha Watanzania hawa kuweza kushiriki kwenye uchumi. Watashiriki vipi kama barabara zao hazipitiki? Leo maeneo mengi ya vijijini bado yana changamoto na mafuriko ya mwaka huu yatufumbue macho tuone kwamba yapo maeneo ambayo tunahitaji kwenda kuwekeza nguvu zaidi.

Mheshimiwa Spika, Watanzania wengi wapo maeneo ya vijijini. Kule Madaba kuna Vijiji vya Ifinga, kilometa 48 hazipitiki msimu mzima wa mvua, lakini huko ndiko kwenye Mbuga ya Selous na huko ndiko kwenye Watanzania ambao wanahitaji kushiriki kwenye uchumi. Niiombe Serikali yangu Tukufu inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kuwekeza pia kwenye miundombinu ya barabara, miundombinu ya uchumi vijijini ili Watanzania walio wengi wanaoishi katika maeneo hayo waweze kunufaika zaidi na uchumi.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)