Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Khadija Nassir Ali

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. KHADIJA NASSIR ALI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa nafasi kwanza kabisa nipende kuungana na viongozi wote ambao wameweza kutoa pole kwa Taifa letu na kwa dunia nzima kwa ajili ya hili janga la corona. Lakini pia nitoe pongezi kwa Serikali kwa namna ambavyo imekuwa ikikabiliana na hili janga.

Mheshimiwa Spika, pongezi pia kwa Serikali ya Awamu ya Tano kwa jinsi ambavyo imeweza kujipambanua kufanya mageuzi makubwa sana ya kimaendeleo katika sekta mbalimbali.

Hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu imeeleza mambo tofauti tofauti ambayo kama nchi na Serikali tumeweza kuyafikia. Hotuba hii imeeleza ukuzaji wa fursa za ajira kwa vijana, lakini pia imeeleza vizuri uboreshaji wa miundombinu kwa reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa. Hotuba hii pia imeeleza ufufuaji wa shirika ndege, ufufuaji wa mali za ushirika, ulinzi wa rasilimali zetu za nchi, ukarabati wa miundombinu ya elimu, uboreshaji wa huduma za afya na maji, upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa mijini na vijiji.

Mheshimiwa Spika, mafanikio haya niliyotaja na mengi ambayo sijayataja yanakwenda sasa kutekeleza moja kwa moja azma ya kuchochea uchumi wetu kwenda sasa kuwa uchumi wa viwanda. Baada ya pongezi hizo sasa niweze kwenda moja kwa moja kwenye mchango wangu na nitaanza kuelezea ukuzaji wa fursa za ajira kwa vijana.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeeleza hapa namna ambavyo imeweza kubuni uzalishaji wa ajira ambazo ni rasmi na zile ambazo sio rasmi, lakini takwimu ambayo Mheshimiwa Waziri Mkuu ameitoa kwenye hotuba yake inaonesha kwamba ajira ambazo sio rasmi ni nyingi sana nchi kuliko zile ambazo ni rasmi. Vile vile tunafahamu ajira ambazo sio rasmi zinahitaji mambo mawili makuu; la kwanza mafunzo wezeshi, lakini pia vitendea kazi baada ya vijana kupatiwa mafunzo ambayo Serikali imeanza kuyatoa.

Mheshimiwa Spika, nafahamu Serikali ina Mfuko wa Maendeleo kwa Vijana na umekuwa ukifanya vizuri sana, lakini kutokana na uhitaji kuwa mkubwa Mfuko huu umeanza kuelemewa kwa mahitaji ambayo kama nchi tupo nayo. Sasa kwa kuzingatia hayo nina ushauri ambao nitatoa kwa Serikali.

Mheshimiwa Spika, jambo la kwanza, Serikali iweze kupunguza masharti kwa taasisi za fedha ili vijana ambao wataweza kupatiwa yale mafunzo waweze kupata mikopo ya kuweza ku-practice yale masomo ambayo watayapata na kuweza kujiajiri. Tunafahamu tulifanya marekebisho ya Sheria za Taasisi za Fedha ambayo yamekwenda sasa kufuta huduma ya VICOBA na zile taasisi ndogo ndogo ambazo mitaani zilikuwa zinawasaidia vijana na akinamama. Sasa tunaomba vijana watakapotoka kwenye zile incubation programmes waweze kupata angalau hata kama sio benki za biashara, benki ya maendeleo ambayo itaweza kuwapatia mikopo kwa masharti naafuu.

Mheshimiwa Spika, ushauri wa pili, kumekuwa na msongamano na uhaba wa vyuo vya stadi za kazi, sisi kama vijana tumelia sana hapa Bungeni angalau kila wilaya iweze kuanzisha Chuo cha VETA na kama wilaya hazitaweza basi angalau hata mkoa. Vyuo hivi ndio ambavyo vinakwenda sasa kutoa zile stadi za kazi ambazo tunazihitaji katika kukuza au kufikia ule uchumi ambao tunaita wa viwanda. Sasa hapa tumeona vyuo ambavyo vinatoa stadi hizo za kazi ni vichache nchini, lakini pia msongamano umekuwa mkubwa. Naomba Serikali iweze kulichukua hilo na kuweza kulifanyia kazi.

Mheshimiwa Spika, la tatu, Serikali iweze kuwa na takwimu ya vijana ambao wana vipaji maalum kwa hizi stadi za kazi. Pia serikali iweze kuwa na takwimu ya vijana ambao tayari wameshapewa mafunzo ya kujiajiri. Kwa kufanya hivyo tutaweza kuona sasa ile elimu inashuka kwa jamii ambazo vijana inawazunguka, lakini pia tutarahisha kwa Serikali katika kuhakikisha kwamba vijana ambao hawana ajira wanaweza kupata hizo taaluma ambazo zinahitajika.

Mheshimiwa Spika, la mwisho kwenye hili, napenda kutoa ushauri kwa Serikali angalau iweze kufikiria namna ya kutoa intensive internship programs kwa wale wanavyuo ambao wamemaliza. Tumekuwa na changamoto ya vijana kukataliwa katika ajira kwa kigezo cha uzoefu. Kwa kufanya hivi tutawawezesha sasa waajiri waweze kuwa comfortable kutuajiri sisi vijana ambao tunatoka chuoni moja kwa moja kwa sababu tayari wanakuwa na uhakika tumepata mafunzo ya kutuwezesha kuingia kazini vizuri.

Mheshimiwa Spika, baada ya hilo nitakwenda moja kwa moja kuongelea hali ya uchumi.

Mheshimiwa Spika, tumeona hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu imeongelea ongezeko la ukuaji uchumi, nawapongeza sana Serikali kwa hilo na niwapongeze Serikali kwa usimamizi mzuri wa ukusanyaji wa mapato. Pia niwapongeze Serikali kwa kuandaa mfumo mzuri wa ukusanyaji mapato. Kwa hayo mawili ndiyo results ambazo tunaziona sasa hivi. Vile vile kwenye hili ningependa kushauri mambo yafuatayo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza, Serikali ifanye jitiahada ya kuangalia walipakodi wapya; tumekuwa tukiwakamua walipa kodi wale wale wa zamani bila ya kuangalia kwamba kila mwaka Serikali ina uwezo wa kukusanya walipakodi wapya na wakaweza kuingia katika kuchangia pato la Taifa.

Mheshimiwa Spika, pili, ningependa Serikali ione namna kuweza kuwatambua wajasiliamali ambao hawana ajira rasmi na kwa nchi hii ndio wengi. Tukiweza kuwatambua tukawapa elimu, tukaweza pia kuwashirikisha katika ukuzaji huu wa uchumi, nadhani watakuwa tayari na wao kuweza kuunga mkono jitihada za Serikali na wao wakaweza pia kuingia katika kukuza pato la nchi.

Mheshimiwa Spika, tatu, kuna wafanyabishara wengini na wajasiliamali ambao sasa hivi wamekuwa wakitumia ukuaji wa teknolojia katika kufanya biashara zao yaani online business na wana make money kuliko hata hawa ambao wameweza ku-estabilish biashara zao kwenye hii proper arrangement.

Mheshimiwa Spika, nchi zote duniani wafanyabiashara wakubwa ambao wamechipukia ni wale ambao wameweza kuona fursa katika ukuaji wa teknolojia. Nasema hivi sio kuwabana au kuwaminya, lakini naamini wao na mimi na sisi wengine Watanzania tupo tayari katika kushirikiana na Serikali kukuza pato la Taifa. Sasa tutakapowawekea protection, tutakapowaona na kwamba na wao ni part ya watu ambao wapo tayari katika kushirikiana na Serikali wataweza kuwa wa msaada mkubwa sana katika kukuza uchumi wa nchi, pia tutaweza kuwaona miongoni mwetu na wao pia wataweza kufaidika katika hili.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. KHADIJA NASSIR ALI: Mheshimiwa Spika, ya mwisho?

SPIKA: Ndiyo.

MHE. KHADIJA NASSIR ALI: Naunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)