Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Hassanali Mohamedali Ibrahim

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kiembesamaki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. IBRAHIM HASSANALI MOHAMMEDALI: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi ili nichangie hotuba ya bajeti ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa mwaka 2020/2021.

Mheshimiwa Spika,nichukue nafasi hii adhimu nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa jinsi jana alivyotueleza namna ofisi yake ilivyokuja na mkakati wa bajeti hii ya mwaka 2020/2021. Mimi nipongeze Wizara zote zilizopo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kazi kubwa wanayofanya kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi na kwa kweli kwa miaka minne hii, tunakwenda mwaka wa tano (5) Wizara zote zilizo chini ya Mheshimiwa Waziri Mkuu zimefanya kazi kubwa sana akiwemo yeye mwenyewe Mheshimiwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amekuwa na kiungo mzuri sana katika kumshauri na kumsaidia Rais wetu Mheshimiwa John Pombe Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitakuwa mwizi wa fadhila kama sijakushukuru wewe, Kiti chako pamoja na Naibu wako kwa kuweza kutuongoza sisi Wabunge kwa kipindi cha miaka mitano. Kwa kweli kazi mliyoifanya ni kubwa, sisi Wabunge tunakushukuru sana tunakuombea maisha marefu wewe na Naibu wako, Mungu akupeni afya na umri na Inshallah Mungu awarejeshe tena katika jengo hili mwaka huu wa 2020. Amen. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nipongeze Wizara zote ambazo zimetekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi, lakini nizipongeze sana Wizara ya Madini na Wizara ya Nishati. Kwa kweli katika kipindi hiki kidogo Wizara ya Madini imefanya kazi kubwa sana katika kubadilisha sheria zetu za ukusanyaji wa mapato. Kwa muda mfupi sana Wizara hii ya Madini imeweza kutuingizia mabilioni ya fedha katika uuzaji wa dhahabu, tanzanite na almasi. Nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri wake kwa kusimamia hilo na vilevile nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri ambaye anasimamia Nishati, kwa kweli leo Watanzania kwa asilimia kubwa sana wanapata umeme mpaka vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile niipongeze Wizara ya Mambo ya Ndani kwa habari njema waliyotulea kwamba wamenunua mashine ya kuweza kutengeneza kadi za NIDA ambayo ime-cost8.5 billion na itaweza kutengeneza kadi za NIDA 9,000 kwa muda wa saa moja. Kwa kweli niipongeze sana Serikali ya CCM ikiongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nije sasa katika suala hili la Corona. Corona ni janga la kimataifa na kila ukisikiliza taarifa za habari ni Corona tu sasa hivi. Nipongeze Serikali zote mbili, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa jinsi walivyochukua jitihada ya kuweza kusimamia masuala haya ya Corona na kuwaelimisha wananchi kwa ujumla na wale ambao wanaingia nchini.

Mheshimiwa Spika, nataka kumshauri Mheshimiwa Waziri Mkuu ambaye ndiye anatuongoza na ndiye mshauri wa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. Kipindi hiki Watanzania wengi wanatumia maji, kila nyumba, mtaa na kila unapokwenda wanatumia maji. Maji yale pengine hata huyo mtu ambaye hana lakini anasaidiwa na mtu mwingine anaambiwa chukua ndoo ya maji hii nawia mikono.

Mheshimiwa Spika,mimi natoa ushauri lakini Serikali ndiye mwenye maamuzi ya mwisho. Ushauri wangu ni kwamba Serikali isamehe kodi ya miezi mitatu katika sekta ya maji kwa sababu sasa hivi kila mahali maji yanatumika. Kwa hiyo, ushauri wangu hii miezi mitatu Serikali isamehe kodi kwa wale wote ambao wanatumia maji akiwepo mtu wa chini mpaka mtu wa juu. Hii itatusaidia, watu watapata kidogo matumaini ya kuweza kuwasaidia wengine maji zaidi ya ndoo moja kwa sababu sasa hivi nyumba ambayo ilikuwa inatumia ndoo mbili ya maji au tatu kwa siku, sasa pengine inatumia ndoo zaidi ya kumi au kumi na tano.

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu mwingine kwa Serikali yetu ya CCM, naomba sana kwamba labda hali ikizidi kuwa mbaya basi Serikali ichukue hatua ya kuweza kutuambia kwamba saa mbili za usiku ukiingia ndani mpaka alfajiri saa 12 ndiyo uweze kutoka kwenda kufanya shughuli zako za kiuchumi. Ikiwa hali itazidi kuwa mbaya, huu ni ushauri pia mzuri, wenzetu nchi nyingi duniani wameshaanza kwenda kwenye lock down. Hata juzi Dubai, Mascat na nchi nyingine za Ulaya ambazo tunazijua za Italy, Spain, London na nchi nyingine zimekwenda katika lockdown kabisa twenty four hours. Mimi ushauri wangu iwe ni kuanzia saa mbili za usiku mpaka asubuhi saa 12, hii itasaidia kupunguza haya matatizo ya Corona. Huu ni ushauri.

Mheshimiwa Spika, ushauri mwingine ni naomba Jeshi la Polisi na Uhamiaji wawe makini sana katika hizi njia za panya. Watu watakuwa wanatoka nchi za jirani kuja huku Tanzania wakisema Tanzania Corona bado haijafika asilimia kubwa, watakuja kutuambukiza sisi. Watu wanapita njia za panya, kwa hiyo, Jeshi la Polis na Uhamiaji wawe makini sana katika hizo njia za panya wasije wakatuumiza huku kwa sababu sasa hivi huko nchi za jirani wameshaanza kuchanganyikiwa na masuala ya Corona.

Mheshimiwa Spika, kwa kweli huu ndiyo ushauri wangu na kabla sijamalizia nimpongeze sana Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa anayoifanya. Kwa kweli kila Mtanzania ni shahidi wa anayoyafanya Mheshimiwa Rais kupitia Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi. Mimi nataka niwahakikishie tu Waheshimiwa Wabunge humu ndani tusiwe na wasiwasi. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. IBRAHIM HASSANALI MOHAMMEDALI: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja ahsante sana. (Makofi)