Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Kiteto Zawadi Koshuma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. KITETO Z. KOSHUMA: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kukubali kunipatia tena nafasi hii ili niweze kutoa michango yangu katika Bunge lako Tukufu. Kipekee kabisa ninaomba nikushukuru wewe binafsi kwa namna ambavyo unakuwa ukiwasaidia Waheshimiwa Wabunge na kuwaonesha moyo wa ubinadamu pale wanapokuwa wanapatwa na matatizo mbalimbali hususani ya msiba.

Mheshimiwa Spika, katika hili ninakushukuru wewe, Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Mawaziri na Waheshimiwa Wabunge wote ambao mliungana pamoja nami kipindi chote ambacho nilimuuguza baba yangu mpendwa na hatimaye Mwenyezi Mungu akampenda zaidi, lakini mlikuwa pamoja nami kwa kunifariji, mmenifariji sana na Mungu awabariki sana, ninawaombea kila la kheri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya salamu hizo za utangulizi, ninaomba sasa nirejee katika kuchangia kuhusiana na hotuba ya bajeti ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Spika, katika hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu yameongelewa masuala mengi; imegusa masuala ya afya, maji, majanga mbalimbali na imegusa maeneo mbalimbali ikionesha maendeleo makubwa ambayo yamefanywa na Serikali inayoongozwa na Chama cha Mapinduzi kupitia Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninaipongeza Serikali kwa jitihada ambazo imeendelea kuzifanya katika kuhakikisha kwamba Tanzania inasonga mbele. Tumeyaona maendeleo, tumeona mabadiliko mbalimbali katika sekta mbalimbali na leo ninaomba kuongelea sana katika Sekta ya Afya.

Mheshimiwa Spika, katika Sekta ya Afya Serikali imejitahidi kadri ilivyoweza kwa kuhakikisha kwamba inakarabati Vituo vya Afya, Zahanati, Hospitali za Wilaya, Hospitali za Mikoa lakini pia imeongeza ujenzi wa Vituo vya Afya, Hospitali za Wilaya katika maeneo mbalimbali na hata Hospitali za Mkoa.

Mheshimiwa Spika, kuna changamoto tu chache ambazo napenda kutoa ushauri wangu ili uweze kufanyiwa kazi. Kujenga Hospitali za Wilaya, Hospitali za Mikoa na Vituo vya Afya ni jambo moja, lakini kuweka wataalam ambao wataenda kuhudumia katika Vituo hivyo vya Afya pamoja na Hospitali ni jambo lingine. Naishauri Serikali sasa, nguvu ambayo iliitumia na kuiwekeza katika ujenzi wa Vituo vya Afya, Hospitali za Wilaya na hata Hospitali za Mikoa, nguvu hiyo hiyo ambayo Serikali ilitumia, basi iitumie kuwekeza katika wataalam.

Mheshimiwa Spika, kujenga unaweza kutumia hata mwezi mmoja unapokuwa rasilimali fedha, lakini kuwaandaa wataalam inaweza ikakuchukuwa takribani miaka mitano ili kuwapata wataalam kuweza kutoa huduma za kiafya.

Mheshimiwa Spika, katika huduma za kiafya, tuna- deal na afya za wanadamu. Kwa maana hiyo, ninaishauri sana Serikali sasa iwekeze nguvu katika kuhakikisha kwamba inaandaa wataalam ili waweze kutoa huduma bora za kiafya na siyo bora huduma.

Mheshimiwa Spika, pia waliopo, wale wataalamu tulionao, basi naiomba Serikali itoe kibali ili iweze kutoa ajira katika Sekta hii ya Afya kwa sababu ninaamini kabisa yako maeneo mbalimbali na kwa sababu hapa tunajadili bajeti ya Waziri Mkuu ambayo inagusa maeneo mbalimbali katika nchi ya Tanzania, sitapenda tu nijikite katika mkoa wangu wa mwanza ambao nao pia unahitaji wataalam katika sehemu mbalimbali. Kwa hiyo, ninaomba Serikali iwekeze katika kuandaa wataalam ili waweze kuzihudumia sehemu hizo ambazo nimezitaja.

Mheshimiwa Spika, katika Sekta hiyo hiyo ya Afya kuna suala la hospitali hizi za kikanda, nilikuwa naishauri Serikali iwekeze nguvu kuhakikisha kwamba tunapata hospitali zenye hadhi ya kikanda sawa na Hospitali ya Muhimbili. Tunayo Hospitali ya KCMC ambayo iko Moshi, nashauri kwamba Serikali iweke nguvu ili hospitali hii na yenyewe iweze kuwa na hadhi zawa na Muhimbili ili kuondoa msongamano katika Hospitali ile ya Muhimbili.

Mheshimiwa Spika, vile vile kuna Hospitali ya Kanda ya Bungando; na yenyewe pia naomba ifanyiwe hivyo hivyo. Pia kuna Hospitali ya Mbeya, Hospitali ya Dodoma General; naomba hospitali hizi ambazo nimezitaja, Serikali iwekeze katika hospitali hizi ili na zenyewe ziweze kutoa huduma sawa sawa na huduma zinazotolewa Muhimbili.

Mheshimiwa Spika, Madaktari bingwa wanaishia kuwepo tu Muhimbili. Ukiwapeleka katika hizo Hospitali ambazo nimekwambia, wanaona kwamba utaalamu wao hauwezi kutumika kwa sababu hospitali zile hazina hadhi sawa na Hospitali ya Muhimbili. Kwa hiyo, ninaomba sana Serikali ijikite katika eneo hilo ili basi tuweze kuboresha huduma za afya katika nchi yetu hii ya Tanzania.

Mheshimiwa Spika, vile vile, katika Vituo vyetu vya Afya na Zahanati zetu tunakosa wataalam wa meno na wataalam wa mionzi. Ninaomba pia Serikali iwekeze katika wataalam hao pamoja na wataalam wengine, lakini ijikite basi katika wataalam wa mionzi na wataalam wa meno ili kuendelea kuboresha huduma za afya.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa naongelea suala la afya na vile vile katika hotuba ya Waziri Mkuu ameongelea suala la janga hili la Corona, nami naomba niungane na Waheshimiwa Wabunge kuendelea kuwasihi Watanzania kwamba tuweze kuzingatia yale maelekezo ambayo tunapewa na Wizara yetu ya Afya ili tusiweze kueneza ugonjwa huu wa Corona.

Mheshimia Spika, naomba niishauri Serikali na ninaamini kwa ushauri huu wataweza kunisikiliza na kuufanyia kazi. Pamoja na kwamba tumeendelea kutoa maelekezo mbalimbali, lakini ninaangalia sehemu ambazo kuna misongamano mikubwa ya watu, pale kukitokea mlipuko, hali itakuwa ni mbaya sana.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano kwenye public transport, ukiangalia pale Dar es Salaam katika haya mabasi ya mwendo kasi, msongamano ambao unakuwepo katika yale mabasi ni mkubwa na ni hatari sana. Ninashauri basi Serikali iangalie namna bora aidha kusitisha hizi public transport hasa ambazo zina msongamano mkubwa na kuangalia njia mbadala ambayo Watanzania wataitumia katika kusafiri kila siku kwenda kufanya majukumu yao mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, sehemu nyingine yenye msongamano mkubwa ni sehemu ya feri pale Dar es Salaam napo pia kuna msongamano mkubwa. Sehemu kama vile la soko la Kariakoo naomba sana Serikali yangu sikivu iangalie maeneo hayo na iweze kutoa tamko ambalo litaweza likawasaidia watanzania na kusaidia kupunguza spreading hii ya ugonjwa huu wa Corona na hata kuzuia vifo.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hiyo naomba sasa niongelee suala la maji,suala la maji limekuwa likipigiwa kelele sana na Wabunge wengi hapa ndani, wakati wa kipindi cha maswali na majibu utaona wakati wa maswali ya nyongeza Wabunge wote husimama kuweza kuulizia masuala ya maji. Lakini pamoja na kwamba Serikali imejitahidi kuchukua mawazo ya Wabunge na kuanzisha wakala wa huduma za maji vijijini yaani RUASA na pia uko mfuko wa maji ambao mfuko huu chanzo chake cha fedha kinatokana na shilingi 50 ya kila lita moja ya petroli.

Mheshimiwa Spika, tumekuwa tukiiomba sana Serikali kwamba iongeze kiwango hiki cha tozo ya shilingi 50 hadi shilingi 100 nia ni njema sana. Nitaongea kama ifuatavyo nia na madhumuni tuweze kufikia walau mfuko huu kuwa na shilingi bilioni 300 zikipatikana shilingi bilioni 300 ina maana kila jimbo lina uwezo wa kupata shilingi bilioni 10. Kigugumizi kinatoka wapi, ninaiomba Serikali yangu kwa kuwa ni Serikali sikivu basi iliangalie na hili ili tuweze kumtua mwanamke ndoo kichwani lazima tuongee kwa vitendo na kwa sababu Waheshimiwa Wabunge tumeendelea kutoa ushauri huu wa kuongeza tozo hii ya shilingi 50 hadi 100 ili lengo letu la kufikia shilingi bilioni 300 na hatimaye kila jimbo kupata bilioni 10.Ninaamini kabisa hakuna mtu ambaye atasimama katika Bunge kulalamikia suala la maji, ninaamini kila jimbo litaweza kufanikiwa kuangalia kwamba masuala ya maji yametatuliwa.

SPIKA: Ahsante sana, Mheshimiwa Kiteto.

MHE. KITETO Z. KOSHUMA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana kwa kunipatia nafasi hii na naamini kabisa kwamba ushauri ambao nimeutoa Serikali yangu sikivu itaweza kuuchukua nashukuru na naunga mkono hoja ahsante sana.(Makofi)