Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Jumanne Kibera Kishimba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kahama Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. JUMANNE K. KISHIMBA: Mheshimwa Spika, yeah, ahsante sana, naungana na Wabunge wenzangu kuchangia Wizara hii ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Kwanza nichukue nafasi hii kumpata pole Mheshimiwa Mbowe kwa ugonjwa wa mtoto wake huu wa corona ambao ulimpata. Nampongeza Mheshimiwa kwa busara kubwa sana aliyotumia kupambana na hili janga la corona, hasa kwa kuzingatia watu wetu ni matabaka mbalimbali, tuna wafugaji, tuna wakulima, tuna wavuvi, tuna wafanyabiashara, na tuna watu wa hali ya chini sana, Mheshimiwa Rais alichotumia kama asingetumia hekima leo nchi yetu ingekuwa na disaster kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mfano mdogo tu kwa sisi wafugaji au wakulima ukiambiwa kwamba usimtoe ng’ombe kwenda kuchunga ingekuwa kazi ngumu sana maana yake ng’ombe hata kama wewe mwenyewe umefariki ng’ombe lazima waende wakale. (Makofi/Kicheko)

Mheshimwa Spika, sisi tunalima mpunga…

SPIKA: Mheshimiwa Kishimba unavunja kanuni kumfikiria kwamba Spika amefariki. (Kicheko)

MHE. JUMANNE K. KISHIMBA: Mheshimwa Spika, hapana. (Kicheko)

SPIKA: Endelea kuchangia Mheshimiwa.

MHE. JUMANNE K. KISHIMBA: Mheshimwa Spika, tuna wakulima wa mpunga, wa mtama ambao lazima waende shambani kwenda kuangalia ndege ingawaje kama watu hawataruhiwa kutoka basi chakula chote kitakuwa sikukuu ya ndege. Kwa hiyo, nampongeza sana Mheshimiwa Rais, Makamu wa Rais, Mheshimiwa Waziri Mkuu na Mawaziri wote na Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia tunaishukuru sana Serikali kwa kuondoa tozo la maiti kwenye hospitali wakati mtu amefariki akiwa anadaiwa, ingawaje baadhi ya hospitali bado wanakataa wakisema kwamba hawajapata waraka. Tunaomba Mheshimiwa Naibu Waziri wa Afya kwenye majumuisho yake ajaribu kutueleza vizuri au atoe waraka huo au atamke ili Sheria hiyo iweze kuanza kutumika hasa wakati huu mgumu sana wa watu wetu wanaokutana nao. (Makofi)

Mheshimwa Spika, tungeomba pia wenzetu wa hospitali na zahanati za binafsi wapunguze au hapa nusu mtu anapofariki, hali kule vijijini ni mbaya sana, sorry. Mwenendo wa ugonjwa huu wa corona ni hatari sana tungeomba Serikali kama inaweza kuwasamehe madaktari walioko Magerezani na Wauguzi wa afya ili waje tuungane nao watusaidie wakati huu. Vilevile kama inaweza Serikali madaktari na wauguzi waliostaafu kama inaweza kuwapa mkataba wa muda inaweza ikatusaidia sana maana yake wapiganaji wetu sasa hivi kwenye hii vita ni wauguzi wa afya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunaomba vilevile wenzetu wa Idara ya Afya kuna zahanati au hospitali ambazo wamezifungwa tungewaomba sana kama wanaweza muda huu wakarekebisha masharti ili hospitali hizo na zahanati ziendelee kuhudumia watu, itatusaidia sana maana yake hali ilivyo kama vile kama siyo watu wetu wa afya na Wizara ya Afya kufanya udhibiti ni vizuri watusaidia sana. (Makofi)

Mheshimwa Spika, napenda vile kuungana na wewe juzi hapa wakati wa mchango na Mheshimiwa mama Prof. Tibaijuka na Mheshimiwa Ngeleja waliliongea sana suala la dawa za kiejeji. Ni kweli tumekuwqa tukipambambana na mafua kwa muda mrefu sana na wenyeji wanaoutalaam wa mafua sitaki kusema kwamba ni corona, lakini ni vizuri wenzetu wa Wizara ya Afya wakafikiria sana suala la kuongea na wenyeji ili kupata mahala pa kuanzia tutegemea tu kwamba tunategemea kwamba lazima dawa ipatikane Ulaya, au chanjo ni kazi ngumu sana ni vizuri wataalam wetu waungane na wenyeji ambao wamekuwa wakipambana na mafua kwa muda mrefu sana kabla ya dawa za kizungu hazijaja, itatusaidia sana kupambana na hili tatizo najua wote tunakuwa na maeneo yanayoongewa mitaani ni kwamba inawezekana watu weusi wanaweza wakajidhibiti wenyewe au nini.

Mheshimiwa Spika, ni vizuri wataalam wa afya wasiogope, na wasiogope kabisa kutamka kwamba kitu hiki kiko hivi kwa kuogopa kwamba labla watavunja wataalam wao, hapana ni vizuri watamke kabisa kwamba kitu hiki kinaweza kuwa hivi, kitu hiki kinaweza kuwa hivi, itatusaidia sana sasa hivi kuna mkakanganyiko mkubwa sana kila mtu anaamuka na la kwake matokeo yake watu wetu wanakuwa kwenye wakati mgumu sana ni vizuri watu wa Wizara ya Afya wawe na msimamo ambao utatuendesha vizuri kukumbana na hili tatizo.

Mheshimwa Spika, kuna hizi mashine za oxygen, tungeomba wataalum wetu wa afya watoe relief kidogo kama mtu anaweza kutengeneza hata kama ina capacity ndogo waruhusiwe kama za zamani zipo zifanyiwe marekebisho, kusema tu kabisa tunahitaji kupata kitu kipya, tunaona wenzetu wa Ulaya ambao wameendelea na ndiyo wanatengeneza wameshindwa kabisa machine hazitoshi, endapo tatizo hili litatokea tunaweza kuwa kwenye wakati mgumu sana. Tunaomba sana wenzetu wa afya Serikali iruhusu kama watu wanaweza kuagiza iwafikirie haraka ili hili tatizo tuweze kukabiliana nalo. Ni kweli kabisa Mheshimiwa Mbowe ameeleza vizuri kwamba suala hili ni bora tukajiandaa nalo hatuna namna yoyote ambayo tunaweza kukabiliana nalo maana yake liko kwa jirani zetu, vilevile linatuathiri kiuchumi.

Mheshimwa Spika, ni vizuri Mheshimiwa Waziri wa Afya akaitisha kongamano ambalo litajumuisha wataalam wote wa pharmacy watengeneza madawa, vilevile na waganga wa tiba za asili ili waweze kukaa pamoja tuweze kupata nini hasa kilichoko ndani ambacho kinaweza kutusaidia wakati tunasubiri dunia ifanye nini.

Mheshimiwa Spika, nachukua nafasi hii kumpongeza Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, amekuwa akifuatilia hoja zetu Bungeni, tulikuja hapa na hoja ya spirit ambayo ni gongo, Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa amechukua gongo ile ameipelekwa kwenye maabara, na kwenye maabara imeonekana inafaa kuliko spirit zilizopo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunamuomba Mheshimiwa Waziri wa Afya sasa kwa kuwa wananchi wetu hawawezi kununua hizi sababu tunazotumia ambazo zina alcohol asilimia 65, atamke basi wananchi kwa muda huu wa dharura wanaweza kunawia gongo? Ili kuzuia hilo suala ya corona. (Kicheko/Makofi)

Mheshimwa Spika, hii sanitizer tunayonawia ina alcohol asilimia 65 na gongo ina alcohol asilimia 55, basi Mheshimiwa Waziri wa Afya kama anaweza kutoa sasa hivi msamaha huo ili iweze kutusaidia…

SPIKA: Jamani anayechangia ni Profesa naomba msikilize vizuri wengine hata hamjui alcohol content ya gongo. (Kicheko)

MHE. JUMANNE K. KISHIMBA: Mheshimwa Spika, nakwenda direct kwenye suala la uwekezaji maana yake najua Ofisi ya Waziri ndiyo inayohusika na uwekezaji, wote tumeuangalia kwenye eneo viwanda, mahoteli na maweneo mbalimbali. Lakini tunaomba Ofisi ya Uwekezaji iruhusu uwekezaji wa mawazo, mimi nafikiri ni uwekezaji mzuri kuliko uwekezaji wowote, nitatoa mfano ingawaje muda mdogo unakimbia. Nikiwa Zimbabwe ndiyo niligundua uchenjuaji wa dhahabu kwenye mchanga na kwa malundo ambayo yamekuwepo hapa ya dhahabu zaidi ya miaka 50 nilivyokujanayo hiyo teknoloji ilinichukua miezi miwili mitatu nikanyang’anywa, lakini kwa kuwa hakuna namna wala kitu unachoweza kudai sikuweza kufanya kitu chochote…(Makofi)

SPIKA: Ni kengele ya mwisho, nakupa dakika mbili umalizie.

MHE. JUMANNE K. KISHIMBA: Mheshimwa Spika, ningeomba Wizara ya Uwekezaji kama itatengeneza kitengo mtu akiwa na wazo kokote aliko ambalo akilileta hapa wananchi wanaruhusiwa kuli-copy, lakini yeye apate per cent kutoka kwenye lile wazo, maana yake wanachokamatilia wao ni wazo ambalo limeshikiliwa kwenye computer, lakini wazo ambalo ukilileta uwezi kuwazuia wananchi, lazima walichukue. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, wenzetu wawekezaji wabadilishe mwelekeo ili tuelekee kwenye eneo lingine eneo la mawazo linaweza kuwa rahisi kuliko leo watu wanasema kwamba huyu kafa na dawa yake, lakini angesema huu mti ni dawa atapanda lini yeye, lakini wenyewe watasema ukitamka mtii huu ni dawa Mheshimiwa Dkt. Karemani ananitazama, wakisema hii ni dawa Mheshimiwa Dkt. Kalemani anayo dawa ya mifupa, kama anaweza kupewa ku-share kwenye kile kinachopatikana ingekuwa bora sana na tusingehangaika na mikutano na kitu chochote, mawazo dunia nzima inayo. (Makofi)

Mheshimwa Spika, kwa kumalizia bei ya dhahabu imeanguka sana, kwenye masoko yetu, lakini kwenye soko la dunia, naomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha anisikilize vizuri sana. Dhahabu imeanguka asilimia 50 mpaka 40 kwenye masoko yetu ya ndani, lakini kwenye soko la dunia haijaanguka, kwanini sasa Benki Kuu isiingie ndani ikanunua hiyo dhahabu kwa wakati huu ili iweze kupata hizo faida maana yake kuna gap kubwa sana kwenye siku kumi kabla ugonjwa haujaanza kudorora, lakini bahati nzuri kama wenyewe wanaogopa Benki Mkuu humu tuna Wabunge zaidi ya watano wanaoijua dhahabu vizuri sana, hata kama ni kuvunja kanuni basi awachukue hao hawa Wabunge waliomo humu ndani wasimamie zoezi hilo la ununuzi wa dhahabu ili Serikali ipate faida, ni vizuri sana wanasema kufa ni kufahana, ni vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana naunga mkono hoja. (Makofi)