Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Peter Joseph Serukamba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigoma Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. PETER J. SERUKAMBA: Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi hii niweze kuchangia hotuba ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Naomba nianze na yafuatayo. Kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi kubwa anayoifanya. Mimi nimepata bahati nimekaa Bungeni hapa muda mrefu kidogo, sijamuona Waziri Mkuu ambaye imekuwa rahisi kwenda kumuona ukiwa na shida na alivyo na uwezo wa kusikiliza. Mungu amjalie sana kwa wema huu na kwa tabia hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikupongeze sana wewe. Kwa miaka hii mitano umetuongoza vyema sana. Wewe ni mnyenyekevu, Job Ndugai niliyemjua mwaka 2005 ndiyo Job Ndugai mpaka leo mwaka 2020. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia na mimi nichukue nafasi hii kuipongeza sana Serikali ya Awamu ya Tano. Rais Magufuli alivyochaguliwa moja ya mambo kama mnakumbuka alianza mwanzoni ilikuwa ni kubana matumizi, safari za nje, watu kunywa chai na kwenda kwenye semina mahotelini. Kwa kawaida watu wengine hawakuelewa, mimi sasa leo baada ya miaka mitano naona faida za kazi kubwa aliyofanya ya kubana matumizi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, amesema Mheshimiwa Nape kuhusu umeme. Tuna vijiji 12,000, tunapofika Juni, 2020 tutakuwa tumeweka umeme katika vijiji 10,000. Maana yake ni nini kwenye uchumi mpana? Maana yake sasa watoto wetu watasoma vizuri mashuleni, afya itawezekana lakini pia ndiyo modernity ya maisha kwamba tunatoka kwenye kipindi ambacho tulidhani ni mtu tajiri ndiye mwenye umeme, sasa Mheshimiwa Magufuli amefanya umeme ni essential kwa maisha ya binadamu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia amefanya kazi kubwa kwenye barabara, aliianza zamani. Naweza nikataja barabara nyingi sana lakini mimi itoshe kusema nampongeza sana kwa barabara ya Kigoma kwenda Nyakanazi. Watu wa Kigoma tunalo deni kwa Mheshimiwa Rais Magufuli. Inawezekana wengine hamjui thamani ya barabara ile, barabara ya Kigoma - Nyakanazi inaenda kutuunganisha watu wote wa Kigoma. Kwa hili, tunayo hakika tutatoa shukurani zetu mwezi Oktoba. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia kwenye afya, kwa bahati nzuri nimekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge hakuna kipindi ambacho nchi hii imefanya kwenye afya kuliko miaka hii mitano ya Mheshimiwa Magufuli. Leo hii Hospitali yetu ya Muhimbili imeanza kutoa huduma ambazo huko nyuma zilikuwa lazima uende India, uende South Africa, uende Ulaya; Mheshimiwa Rais Magufuli amefanikiwa huduma hizo sasa zinapatikana hapa kwetu. Nimpongeze sana Mheshimiwa Magufuli kwa kazi kubwa anayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia kwenye maji, tumeanzisha RUWASA, Waheshimiwa Wabunge mtakubaliana nami ndani ya miaka mitatu ijayo mtaona huduma za maji vijijini zitaongezeka sana kwa sababu ya RUWASA. Leo hii ukiangalia vijijini hata kwangu kule kuna miradi midogomidogo inasimamiwa na RUWASA, inafanya vizuri sana, nimpongeze sana Mheshimiwa Rais na Serikali kwa kazi kubwa waliyoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunaangalia uchumi mkubwa, ukiangalia macro-economic stability ya nchi nawapongeza sana watu wa Wizara ya Fedha, bado inflation imebakia chini kwenye single digit, wameweza ku- control exchange rate, wameweza ku- control uchumi mkubwa ule na ndio maana leo sasa unaweza ukaona tunajenga barabara, madaraja na tunaweka maji; hii ni kwa sababu uchumi mkubwa umesimamiwa vizuri sana. Kwa hili naomba mnikubalie, ni ya kiupendeleo kidogo, lakini nimpongeze kaka yangu Mheshimiwa Dkt. Mpango kwa kazi kubwa. Nataka niwasaidie mwelewe na hilo ndio standard za Kigoma, kwa hiyo Mheshimiwa Magufuli alivyomchagua Mheshimiwa Mpango mnaweza mkaona standard za Kigoma, ndio hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo hii angalia kwa sababu ya uchumi kusimamiwa vizuri tunajenga meli Ziwa Nyasa, Ziwa Victoria na Ziwa Tanganyika; ni kwa sababu ya kazi kubwa ya kusimamia uchumi mkubwa. Leo tunaanza kufanya kazi ya infrastructure ambayo ikiisha ninayo hakika Tanzania ya viwanda sasa itawezekana, leo hii Tanzania inawezekana kwenda digital kwa sababu Tanzania tuna mkongo wa Taifa kila Wilaya, kwa hiyo tunayo hakika Tanzania kama nchi tutakwenda digital muda sio mrefu sana. Kwa hiyo kazi yote hii imefanywa na Serikali ya Awamu ya tano kwa usimamizi wa Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na Mawaziri na Serikali nzima, nawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, natoka Kigoma kuna wavuvi; sasa nataka nimwombe rafiki yangu Mheshimiwa Waziri wa Uvuvi, kuna nyavu za TBS na kuna nyavu za Wizara, wale wavuvi tumewachanganya hawajui hii nyavu ni ya TBS ama hii nyavu ni ya Wizara. Niombe sasa waende wakatoe clarification ili watu wangu wa Mwamgongo, Kagunga na Ziwani waweze kupata hizo nyavu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la mwisho, nataka niongelee suala la corona, ni janga kubwa lakini nimekuja na ushauri nimwombe Mheshimiwa Waziri wa Fedha. Corona ni jambo kubwa baya, lakini tutafute opportunity na sisi kama nchi zinaezoendelea, nimesikia African Union wameanza movement, naombeni na sisi kama Tanzania tuwaombe wakubwa wanaotukopesha, lenders wote wasimamishe sisi kulipa madeni ili fedha ambazo tunalipa deni la Taifa zitumike kwenye athari za uchumi zinazoletwa na corona.

Mheshimiwa Spika, corona naiangalia kwa side mbili; moja ni suala la afya na utabibu, linasimamiwa vizuri sana; upande mwingine ambao ni mbaya zaidi ni upande wa uchumi. Leo hii amesema hapa mtu dhahabu tunayo, hatuna pa kuuza kwa sababu wanunuzi hawawezi kuja. Leo hii tunalima, tutaanza kuvuna mazao yetu ya biashara, tutavuna lakini hatutakuwa na pa kuuza kwa sababu wanunuzi hawawezi kuja, hii ni hatari sana kwa uchumi wetu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo niwaombe leo hii hoteli zinafungwa, migahawa inafungwa, hali ni mbaya ningemwomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha atusaidie aongee na Benki ziwasaidie wafanyabiashara Watanzania hasa wale ambao wamepata matatizo Benki zisimamishe loan repayment kwamba sasa hivi kwa mtu anayeta mizigo toka China, kwa mtu mwenye baa, hoteli, mtu mwenye hoteli, transporter, watu wa mafuta, watu wa biashara za kwenda mfano mtu anayeuza maua leo hana pa kuuza maua, lakini ana mkopo benki lazima aendelee kulipa, kwa hiyo ni wakati mgumu, niiombe Serikali iwaombe Benki angalau kwa miezi mitatu yasimamishe loan repayment, kwa sababu hapa tutapata tatizo jingine tutapata corona ya umaskini , tutapata matatizo makubwa zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuna tatizo la kiafya, lakini tatizo linaloletwa na uchumi linakuwa kubwa sana, kwa hiyo niwaombe watu wa Benki watukubalie kwamba umefika wakati angalau na wao wapate hii pinch wasimamishe loan repayment kwa miezi mitatu tukiangalia hali inavyokwenda.

Mheshimiwa Spika, nimalize kwa kusema tena, nakupongeze sana wewe, Mheshimiwa Waziri Mkuu nampongeza sana kwa kazi kubwa ya kusimamia Serikali, tumeona kazi waliyoifanya pia watuplekee pongezi zetu kwa Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa ya kizalendo, ya kimapinduzi na mtu anayeona mbali. Mheshimiwa Rais Magufuli anaona mbali na ndio maana ya kiongozi na nina hakika Watanzania watamchagua tena mwaka 2015 ili amalizie kipindi chake cha miaka mitano na nina hakika ataipeleka nchi yetu kwenye uchumi wa kati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja ya Mheshimiwa Waziri Mkuu na nakushukuru sana. (Makofi)