Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Dr. Jasmine Tiisekwa Bunga

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Vyuo Vikuu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. DKT. JASMINE T. BUNGA: Mheshimiwa Spika, na mimi napenda kuungana na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kutoa pongezi kwa Serikali ya awamu ya tano chini ya uongozi wa Mheshimiwa Raisi wetu mpendwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri wanayoifanya katika kuhakikisha Watanzania wanaishi kwa amani na utulivu na kuendelea kusimamia kutekeleza Ilani ya CCM kuwaletea wananchi maendeleo endelevu.

Mheshimiwa Spika, napenda pia kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi nzuri anayoifanya pamoja na hotuba nzuri iliyojaa matumaini ya kufikia malengo yetu ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Mheshimiwa Spika, napenda pia kukupongeza kwa kazi nzuri na weledi wa hali ya juu kuhakikisha vikao vya Bunge la Bajeti vinaendelea kwa kuchukua tahadhari zote zinazotakiwa katika kujikinga na ugonjwa wa mapafu ujulikanao “Covid-19”. Nakupongeza pia kwa jinsi ulivyoendelea kuimarisha matumizi ya Bunge Mtandao ambao umeendelea kurahisisha vikao, lakini pia kupunguza gharama kubwa hasa ya kuchapisha marejeo mbalimbali.

Baada ya pongezi hizo naomba sasa kuchangia kwa kutoa ushauri kuhusu Mfuko wa UKIMWI (ATF).

Mheshimiwa Spika, bajeti ya UKIMWI inategemea kwa zaidi ya asilimia 90 fedha kutoka kwa wafadhili wa nje. Lakini tumeshuhudia wafadhili hawa wameanza kutuwekea masharti ambayo hayaendani na utamaduni wetu na kutishia kuondoa ufadhili kwenye suala la UKIMWI. Lakini pia tunashuhudia nchi zote duniani sasa zikiyumba kiuchumi kutokana na shughuli nyingi za kiuchumi kusimama kutokana na ugonjwa huu wa corona. Kwa mantiki hii, tunategemea kuona wafadhili wakijitoa katika kufadhili miradi mingi ya maendeleo ikiwemo ya UKIMWI.

Mheshimiwa Spika, UKIMWI bado ni tatizo na janga la kitaifa na dunia. Hivyo basi, naungana na wote walioshauri Serikali kuwa ni wakati muafaka sasa kama nchi kuchukua tahadhari mapema kwa kutafuta tozo maalum kwa ajili ya mfuko huu wa UKIMWI. Asilimia 4.7 ya maambukizi kitaifa bado ni kubwa na tishio, hivyo tutoe kipaumbele kwa mfuko huu kuhakikisha tunapata chanzo endelevu cha fedha kwa ajili ya ATF.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.